Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nami fursa hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyokuwa mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa uchumi wa viwanda hautafikiwa ikiwa Serikali yenyewe ni kikwazo katika kufikia Tanzania ya viwanda. Nayasema haya kwa sababu mimi nipo katika Kamati ya Viwanda na Biashara, lakini kumekuwa na kusuasua kwa Hazina kupeleka fedha katika Wizara hii kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoishauri ni Serikali itenge fedha ya kutosha katika Wizara hii ili kuweza kufikia hiyo Tanzania ya viwanda. Tunaona takribani miaka mitatu mfululizo mpaka sasa hivi fedha inayotolewa ni kiwango cha chini sana na haikidhi. Licha ya kuwa ni kiwango cha chini, lakini pia haifiki kwa wakati. Kwa hiyo, naishauri Serikali, fedha ambayo inatengwa katika Bunge hili la bajeti ifike kwa wakati ili kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wale wamiliki wa viwanda ambavyo vinatumia sukari ya viwandani. Wamiliki wale wanadai fedha nyingi sana, kwa sababu waingizapo sukari hiyo huwa wanatozwa asilimia 15, lakini mpaka sasa hivi wafanya biashara hao wakubwa wanaidai Serikali shilingi bilioni 43. Hadi sasa hivi ni shilingi bilioni sita tu ambazo wamelipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoshangaa, wakati wanailipa ile asilimia 15 wale wafanyabiashara walikuwa wanalipa hela cash na ile fedha yao ni ya kuweka ili watakapomaliza kuitumia ile sukari watatoa taarifa yao na kurudishwa, lakini wanaporudishiwa wanarudishiwa kidogo kidogo. Sasa naiuliza Serikali, ni kwa nini, wakati wale wafanyabiashara wanalipa cash na hawalipi kidogo kidogo? Mpaka sasa hivi ni mwaka wa nne huu kumekuwa na kusuasua kwa ulipaji wa hiyo fedha. Naishauri Serikali, ili ifikie Tanzania ya viwanda iwasaidie wananchi, iwasaidie hawa wafanyabiashara kulipa fedha hiyo kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusimdanganye Mheshimiwa Rais, Rais anataka Tanzania ifikie katika uchumi wa viwanda na ili kumsaidia, Wizara kama Wizara pamoja na Mheshimiwa Waziri ni kumpa ushirikiano. Wale wenye viwanda wanalalamika mpaka sasa hivi fedha zao wanadai ni mwaka wa nne, wamendika barua nyingi na mpaka sasa hivi fedha zao hawajarudishiwa. Shilingi bilioni 43 mpaka sasa ni mwaka wa nne wamelipwa shilingi bilioni sita na hizo shilingi bilioni sita siyo kwa mfanyabiashara mmoja, kila mtu amelipwa kidogo kidogo. Mwingine shilingi bilioni moja, mwingine bilioni mbili. Kwa hiyo, Serikali yenyewe inakwamisha hii Tanzania kufikia uchumi wa viwanda. Naishauri Serikali iwalipe fedha zao kwa wakati kwa sababu ule ni mtaji wao na ni haki yao kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiyti, kingine ni kwamba viwanda vilibinafsishwa miaka ya 1990 na viwanda vile wakati vinabinafsishwa nia na madhumuni ni kuviendeleza na kuweza kuwapatia ajira wananchi wetu na pia kupata pato la Taifa, lakini kuna wenye viwanda waliomilikishwa, wamechukua viwanda vile na kwenda kukopa fedha na kufanyia miradi mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kamati, tuliomba kuundwe Tume Maalum, kwa sababu, sisi kama Kamati tuliomba tutembelee vile viwanda kuangalia makaratasi, kuwaambia kwamba viwanda vilivyobinafishwa vingine vinafanya kazi vizuri, vingine vimefungwa, vingine vimeuza mitambo yao; lakini haitasaidia endapo sisi wenyewe kama Kamati hatutakwenda kwenye eneo husika na kujua hali halisi. Tumeomba kuvitembelea mpaka sasa hivi, hatujapata nafasi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, ili kufuatilia viwanda vilivyobinafsishwa na viweze kufanya kazi sawa sawa iundwe Tume Maalum ambayo itasaidia kufuatilia vile viwanda vyote vilivyobinafsishwa na kuviangalia kama kweli vinafanya kazi kwa kusuasua na kama vingine havifanyi kazi kabisa ili wapewe wawekezaji wengine ambao wataweza kuviendeleza na kusababisha uzalishaji uwe mwingi na ajira ipatikane kwa wananchi wetu na pia kulipa kodi. Kwa sababu tunajua kuna maeneo mengi kuna viwanda ambavyo vilikuwa ninafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 1985 nilikuwa nasoma Shule ya Sekondari Morogoro, Form One; mwaka ule ukifika Morogoro viwanda vilikuwa vingi, unapata ajira mara moja, lakini ni vigumu sana kupata eneo la kuishi. Kulikuwa na viwanda vya Canvas, Ceramic, Polyster, Moro Shoe, vilikuwa vingi sana lakini viwanda vile vimekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, wakati Serikali inatafuta wawekezaji kwenda kukata mapori na kuanzisha viwanda vingine kwanza vifuatiwe vile viwanda kwa sababu maeneo yapo, majengo yapo kinachotakiwa ni kubadilisha tu miundombinu iliyokuwepo pale na kiuweka ya kisasa ili kuweza kuleta uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ulipishwaji wa kodi kwa wafanyabiashara kabla ya kuanza kufanya biashara. Tumewaona wafanyabiashara wengi ambao wanataka kuanzisha biashara zao hususan mijini kwenye maduka, kwanza ili wapate leseni ni lazima wakalipe mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, itoe muda maalum ambao utamsababisha yule mfanyabiashara anapotaka leseni, natolea mfano kwa Mkoa wa Dar es Salaam, ukitaka kufungua duka lako unakwenda pale Anatoglo (Mnazi mmoja) unataka leseni, hawakupatii leseni wanakwambia kwanza nenda summit tower pale makutano ya Lumumba na Uhuru ili kuweza kupatiwa tax clearance na hiyo tax clearance huwezi kupewa mpaka utoe mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza, mimi biashara ndiyo nakwenda kufanya au mfanyabiashara anataka aanze biashara, unamkadiria mapato; hayo mapato ameuza kitu gani? Hii ndiyo inakwamisha wananchi. Inakwamisha wafanyabiashara kushindwa kuendelea baada ya mwaka mmoja hufunga maduka yao na kuacha kwa sababu Serikali inatakiwa impe muda na kama imempa mashine ya EFD itatumia ile mashine kuweza kukadiria mapato na kuweza kumkadiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, mwananchi atakapofungua biashara kwanza apewe muda maalum angalau miezi mitatu ndipo aanze kulipa mapato, lakini kitendo kinachofanywa na Serikali sasa hivi kupitia TRA kuanza kumpa mtu makato kabla ya kufanya biashara, kusema kweli ni kitendo cha dhuluma na hiki hupelekea wafanyabiashara wengi kufunga maduka yao hususan maeneo ya mijini ninayozungumzia ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia biashara zinazofanywa, wanaolipa kodi ni wachache. Kuna kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais inasema “ukiuza toa risiti na ukinunua dai risiti”, lakini sasa hivi ukifika Mkoa wa Dar es Salaam kuna wafanyabiashara. Hatuwakatai kwamba ni wafanyabiashara ndogo ndogo nao wana wajibu wa kufanya baishara, lakini wanauza mbele ya maduka ambayo wanalipa kodi. Wafanyabiashara wale hawalipi kodi yoyote kwa Serikali na ukiuliza unaambiwa ni wapigakura wetu. Tunaisaidia Serikali au tunaangamiza Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni na madhumuni ni kupata kodi; na kama umempa kitambulisho cha shilingi 20,000/= basi tuwatafutie maeneo maalum. Kwa sababu tendency ya Mwafrika, tendency ya Mtanzania anaona biashara inayouzwa barabarani ni rahisi mno kulikoni ya madukani; na hii ndiyo maana inapelekea wafanyabiashara wengi wanafunga maduka yao kwa sababu hata kama ukiuza wanaona barabarani ndiyo rahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawe mwenyewe ukipita maeneo ya Kariakoo utaona msongamano mkubwa kwenye barabara. Hata barabara ya Msimbazi ni vigumu kupita watu, wafanyabiashara wamepanga biashara zao mpaka milangoni mwa maduka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali itenge maeneo maalum kwa wale wafanyabiashara wanaolipa kodi ili waweze kuwa na uwezo sasa wa kuuza na kuweza kulipa kodi na ikifikia mwisho wa mwaka wasiweze kufungiwa maduka yao. Wale wanaoambiwa kwamba wao ni wapiga kura hawatakiwi kulipa kodi ni kitambulisho tu ambacho kinamwidhinisha afanye biashara, basi watengewe maeneo yao. Naishauri Serikali ifuatilie jambo hili ili kuweza kuwa na mapato zaidi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishauri Serikali itumie malighafi inayopatikana katika viwanda vyetu. Malighafi hiyo itasaidia kukuza kilimo chetu ambacho kitapelekea wananchi kupata kipato na kulima zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara ya Viwanda na Biashara, watendaji wengi wamekaimishwa. Naishauri Serikali sasa ijaze zile nafazi zilizokaimishwa ili wale Watendaji wawe na nafasi ya kuweza kutoa maamuzi yao katika kuendeleza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana. (Makofi)