Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuwa mwongeaji kwa siku ya leo kwenye hii Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwanza nataka niseme tu kwamba, humu ndani Wabunge tumeingia kila mtu ana fani yake, wako wakulima, wako wafugaji, wako Walimu, tuko wafanyabiashara, wako Wanasheria. Kwa hiyo, kila mtu anaijua sekta yake vizuri, pamoja na kuwa wapo wengine wanajua kila sehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, Wizara ya Viwanda na Biashara, kama inavyoitwa, Waziri wa Wizara hii anachotakiwa ni kuhakikisha kwamba anatengeneza biashara inakwenda vizuri kwenye nchi yetu ya Tanzania, asiwe ni mmoja wa sehemu ya kubomoa biashara kwenye nchi hii. Kwa nini nasema hivyo? Inaonekana kabisa wazi Wizara hii ya Viwanda na Biashara haielewi chochote kuhusu biashara kwenye hii nchi. Kabisa, hili ni suala la wazi, kwenye ukweli lazima tuseme ukweli, na ndiyo maana sasa hivi Rais wetu anapata tabu sana, kila anapokwenda anaelezea mambo, anakuwa yeye ndiye Waziri, yeye ndiye Rais. Kwa kweli, Rais mwishowe atapasuka kichwa, watu aliowaweka hawamsaidii! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwenye ukweli huwa sipindishi maneno, ukweli ni ukweli tu. Hivi, mimi nauliza Wizara ya Biashara, leo hii ukiangalia kodi kila Wizara inaanzisha kodi kuhakikisha kwamba inakomesha biashara au inakomoa biashara, kila Wizara. Leo hii ukienda kwenye Wizara ya Kazi, Vijana na Ajira, unakuta kuna WCF, hawa wanaambiwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, wao wana chaji zao kibao. Ukienda kuna OSHA, (Usalama wa Mahala pa Kazi), wao wana kodi zao nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano mmoja tu wa hawa OSHA, mimi nafanya biashara zote, ya mafuta nafanya na biashara zingine. Nitolee mfano kwenye biashara ya mafuta, wanachukua kodi kwa mwaka laki tano, OSHA. Mwaka huu wanataka milioni tatu na laki tano, kwenye kituo cha kijijini. Kituo cha mjini mpaka milioni sita, kwa mwaka, ada. Sasa imekuwa kila mtu anakusanya fedha na anaona sifa, kwamba akimkomesha, akimfungia mfanyabiashara, yeye anaona sifa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niulize, hapo hapo kuna WCF, wako hivyo hivyo. Ukija Halmashauri kuna service levy, anachukua kwenye mauzo, siyo kwenye faida, kwenye mauzo, 0.3%. Sasa ukiangalia kwenye viduka vidogo, nendeni hapa Dodoma tu, viduka vyote vidogovidogo hivi, mtu anaanzisha kiduka chenyewe kina thamani ya milioni tatu, nne, anapigwa mpaka laki tatu, laki nne, hiyo service levy, halafu sasa Waziri wa Viwanda na Biashara yupo. Sasa yeye biashara yake ni ipi, ni kuua biashara au kukuza biashara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo ukweli, nini biashara ambayo anaitetea, maana yake anatakiwa atetee wafanyabiashara wawe wengi, aingilie kila sehemu ambapo anaona wafanyabishara wanaonewa. Ndiyo maana ya biashara, lakini sasa kila mtu amekuwa sasa mchukua kodi, ukija vipimo, anakwenda dukani mtu wa vipimo, ameshapima ule mzani wa dukani, kagonga na label yake, kila kitu, kwenye duka dogodogo tu linauza mchele na nini, kesho anakuja tena, anasema mbona huu mzani wako unapunja, wakati yeye ndiye kagonga ule muhuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nijue, ndugu yangu, Mheshimiwa Kakunda, maana ya kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara maana yake lazima ahakikishe kwamba anakuza biashara, si kuua biashara. Kwa hiyo, inatakiwa kila sehemu ambako mfanyabiashara anaonewa, yeye aingilie, kutetea, lakini wamejielekeza sana kwenye viwanda, viwanda, viwanda, sawa, kuna kiwanda cha General Tyre, kilikuwa namba moja katika East and Central Africa kwa ajili ya kutengeneza matairi bora. Wote hakuna mtu ambaye hajapenda tyre la General Tyre, mpaka leo hiki kiwanda kipya hakifufuki! Kiwanda cha Serikali, leo hii tunashindwa na firestone ya Kenya, inaingiza mpato makubwa sana kwenye Serikali ya Kenya, lakini sisi General Tyre, tumeingia tu tunapiga siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Mbunge wa kushangilia, kwenye ukweli nitasema ukweli kutetea maslahi ya nchi yangu. General tyre ni muhimu, mimi siwezi kukaa hapa nasema tu haya tu Mheshimiwa Waziri, umeanzisha kiwanda fulani, umeanzisha kiwanda fulani wakati viwanda havipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Yuasa, Yuasa mpaka Uingereza walikuwa wananunua betri za Yuasa, kiwanda cha Serikali, kimebinafsishwa, mpaka leo, wameangalia kinafanya kazi gani! Kuna viwanda vingapi vilibinafsishwa nchi hii, vinafanya kazi gani, watu wamevikalia tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vimekaliwa tu, kwa hiyo, naomba…

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimweleze ndugu yangu, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, asimamie Wizara yake ya Viwanda na Biashara na hasa upande wa biashara, ahakikishe kwamba biashara anaisimamia katika Wizara zote….

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa muhimu.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Sasa wewe naona, ungekaa kwanza kidogo, unanichanganya.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani, taarifa!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby naomba uendelee.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ahsante. Kwa hiyo, ninachoomba, kwamba hatua zichukuliwe, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara aangalie biashara, kila Wizara sasa hivi, wanasema TRA tu, TRA kweli inachukua kodi yake, lakini kuna kodi zingine kubwa kuliko za TRA, tozo zimekuwa nyingi sana sana kuliko hata hizo za TRA. Kwa hiyo, naomba sana waangalie sana na Waziri afanye vikao na wadau ili apate hayo matatizo, siyo kila siku tunamwona tu naangalia tiles, anaangalia mbolea, ajaribu kukaa na wadau wamwambie, wampe changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)