Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kwa rehema zake nyingi ametujali afya njema na kutuwezesha kukutana katika Bunge hili Tukufu la Bajeti ili kuweza kukamilisha kazi tuliyoianza tarehe 9 Mei 2019 ambapo niliwasilisha hoja hii.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge na Katibu wa Bunge kwa kusimamia kwa ufanisi mkubwa majadiliano yote kwenye Mkutano huu wa Kumi na Tano wa Bunge hili tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee napenda pia kumpongeza Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mbunge), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake anaoendelea kutuonyesha wasaidizi wake katika majukumu yetu ya kila siku Bungeni.

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii pia kuwashukuru Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati zote za Bunge kwa kufanya kazi kwa karibu na Wizara yangu. Kipekee nimshukuru Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Kakoso, pamoja na Wajumbe wake ambao wameiongoza Wizara vizuri katika utekelezaji wa miradi ambayo imeainishwa kwenye Sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Ninaahidi kwamba Wizara ninayoiongoza itafayafanyia kazi masuala yote yaliyoshauriwa na Kamati hizo.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kumshukuru Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa maoni, ushauri na mapendekezo yake kuhusu bajeti ya Wizara yangu.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwatambua Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika bajeti yangu. Waheshimiwa Wabunge 18 walichangia wakati wa majadiliano ya hoja ya Waziri Mkuu, Waheshimiwa Wabunge 91 wamechangia kwa kuzungumza katika bajeti hii inayoendelea na Waheshimiwa Wabunge 66 wamechangia kwa maandishi wakati wa majadiliano ya hoja ya Wizara yangu. Nawashukuru sana kwa michango yao.

Mheshimiwa Spika, hivi punde Waheshimiwa Naibu Mawaziri wa Wizara yangu wameanza kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia maeneo ya kisekta (sekta ya ujenzi na sekta ya mawasiliano na uchukuzi). Niwashukuru sana kwa jinsi ambavyo wamejibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, naomba nihitimishe kwa kujibu hoja za kisera pamoja na kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizojitokeza. Naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Wizara itajibu hoja zote za Wabunge kwa maandishi na kuwapatia Waheshimiwa Wabunge wote majibu ya hoja hizo kwa njia ya kitabu kitakachoandaliwa kabla ya hitimisho la Mkutano huu wa Bunge la Bajeti.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo wote tunafahamu, mkataba wa miaka mitano kati ya wananchi na Serikali waliyoichagua ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 ambayo itahitimishwa mwaka 2020. Baadhi ya ahadi zilizomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ni pamoja na ujenzi wa reli ya SGR, ukarabati wa reli ya kati, ukarabati wa bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, ufufuaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), ukamilishwaji wa barabara zinazounganisha mikoa, uboreshaji wa mawasiliano nchini na ufufuaji wa Kampuni ya Meli. Ahadi hizi zinatokana na kilio cha muda mrefu cha Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili tukufu ambao wamekuwa wakiishauri na kuitaka Serikali kuwa na miradi ya vipaumbele na kuitekeleza ili nchi iweze kupiga hatua za haraka kuelekea kwenye uchumi wa kati.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hayo, ndiyo maana sehemu kubwa ya bajeti ya maendeleo imeelekezwa kwenye Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na hata leo ameongeza zaidi ya shilingi bilioni 90 kwenye Wizara hii. Hii ni kutokana na majukumu makubwa ambayo Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeyabeba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa inakaribia kukamilisha ahadi ilizozitoa kupitia Ilani yake ya Uchaguzi. Napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba, nikiwa mwakilishi wa Mheshimiwa Rais kwenye eneo la Sekta za Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kushirikiana na Naibu Mawaziri pamoja na Wataalam wa Wizara tutaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na ahadi alizozitoa Mheshimiwa Rais zinazohusu Sekta hii ili kufikia mwisho wa mwaka 2020 ziwe zimekamilika.

Mheshimiwa Spika, aidha, tutaendelea kupambana na kuzitatua kero za wananchi zitakazojitokeza wakati tukiendelea na utekelezaji wa Ilani hii.

Mheshimiwa Spika, kuhusu deni la makandarasi, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2018 madeni ya makandarasi na Wahandisi Washauri yalikuwa shilingi bilioni 833 ambayo yalivuka na kuingia mwaka wa fedha 2018/2019. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 makandarasi waliendelea kutekeleza miradi na kuzalisha hati za madai mpya, Serikali imekuwa ikiendelea kulipa madeni ya makandarasi na wahandisi elekezi ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2019 deni lilikuwa shilingi bilioni 962.

Mheshimiwa Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba Wizara ya Fedha na Mipango hadi mwezi huu Mei itakuwa imelipa shilingi bilioni 609. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa jinsi ambavyo ameitikia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ili kuhakikisha kwamba katika mwaka huu wa fedha, tutakapoingia mwaka mpya wa fedha tena hatutavuka na deni kubwa, na kwa jinsi hiyo basi miradi yote ambayo tumeiainisha kuanza katika mwaka ujao wa fedha tutaanza kuitekeleza bila wasiwasi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia sana kuhusu deni la TAZARA, lakini pia kwenye Taarifa ya Kambi ya Upinzani walizungumzia deni la TAZARA ambalo linaonekana kufikia shilingi bilioni 434. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha amejaribu kulifafanua deni hili, lakini moja tu nizungumzie kwamba, Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge deni hili unapolizungumzia ni deni la nchi mbili, ni deni la Tanzania pamoja na Zambia. Katika deni hili ukiliangalia shilingi bilioni 237 ni deni ambalo limetokana na Itifaki ya Serikali ya China, kwa hiyo, itifaki hii inahusisha pia upande wa Zambia, lakini nishukuru kwa madeni ambayo yanatuhusu sisi huku yakiwepo malipo ya wastaafu Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameyaelezea vizuri.

Mheshimiwa Spika, katika michango ya Wabunge, wamezungumzia kwa uchungu sana kuhusiana na utaratibu wa majadiliano yanayoendelea kati ya Serikali na Mwekezaji wa Bandari ya Bagamoyo. Nilichojifunza kwa Waheshimiwa Wabunge ni kwamba Serikali ifanye haraka kuhakikisha kwamba majadiliano hayo yanakamilika.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa kwamba majadiliano yangali yanaendelea, lakini kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walisema kwamba Serikali imekataa, sina taarifa ya hilo. Na baada ya kumaliza Bunge nilijaribu kuwasiliana na Mamlaka kuulizia kama majadiliano yameshafikia ukomo lakini ni kwamba majadiliano yanaendelea. Ila ni kweli kwamba yamechelewa kutokana na masharti ambayo yanaonekana hayana manufaa kwa upande wa Serikai ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba Waheshimiwa Wabunge waridhie kwamba Serikali bado inaendelea na majadiliano na Bunge lako tukufu limekuwa muda mrefu linaishauri Serikali isije ikaingia mikataba ambayo haina maslahi kwa umma. Kwa hiyo, Serikali inaendelea na pale itakapokuwa imefikia ukomo wa yale majadiliano, nikuahidi tu kwamba Serikali itatoa taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge ili na wao waweze kutoa mawazo yako. Kwa hiyo, niseme tu kwamba bado tunaendelea na majadiliano kuhusiana na uwekezaji wa bandari ya Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 15 wa kitabu cha bajeti ulizungumzia kuhusu ujenzi wa barabara (express way) ya Dar es Salaam – Chalinze. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia TANROADS ilimwajiri Mhandisi Mwelekezi (Transaction Adviser) kutoka Korea. Transaction Adviser huyu aliajiri makampuni mengine 11 yenye uzoefu na utaalam na miradi ya PPP kutoka duniani kote ili kuishauri Serikali namna bora ya kutekeleza mradi wa Dar es Salaam – Chalinze (express way) kwa utaratibu wa Public Private Partnership, alimaliza kazi hiyo mwezi Desemba, 2016.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya PPP Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa idhini tuendelee na hatua zingine za utekelezaji tarehe 22 Mei, 2017. Aidha, wakati idhini ya Wizara ya Fedha na Mpango inatolewa tayari Serikali ilishaanza juhudi za kupunguza msongamano katika bandari ya Dar es Salaam, ambazo ni ujenzi wa bandari kavu ya Ruvu, ukarabati wa reli ya meter gauge na ujenzi wa reli ya SGR. Hivyo, busara ya Serikali zilipelekea kuamua kufanya mapitio upya ya taarifa ya upembezi yakinifu ili kupunguza madhara (risk) ambayo yangehamia upande wa Serikali kumlipa mwelekezi ambaye angejitokeza kuwekeza katika mradi huu kwa kuwa magari ya kubeba mizigo yangeanzia Ruvu badala ya kuanzia bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa usanifu wa mradi huu wa express way ilikuwa ni kwamba barabara inakwenda kuanzia bandari ya Dar es Salaam na kwamba ilikuwa inategemea tozo sasa za magari ambayo yatakuwa yanabeba mzigo kuanzia bandari ya Dar es Salaam. Lakini sasa hapa katika kwa sababu study zote zilikuwa zinaendelea, SGR na baada ya kuonekana kwamba bandari ya Dar es Salaam sasa imekuwa na mizigo mingi uwezo wake utapungua ndiyo tukaamua kujenga bandari ya Kwara. Ukiangalia study hiyo sasa inabidi irudiwe kwa sababu kama mwekezaji alikuwa anategemea tozo zake azipate kutoka kwenye magari ni lazima hiyo iweze kurudiwa ili kuona kama bado tunaweza tukachukua mkopo kwa mwekezaji na kwamba mkopo huu utalipwa katika muda unaostahiki.

Mheshimiwa Spika, hilo ndiyo ambalo limefanya kwamba, kwa sababu tunaendelea na ujenzi wa SGR na ambao tunategemea itabeba zaidi ya tani milioni 17 kwa mwaka, wakati huo huo tumejenga dry port ya Kwara na kwamba SGR ikishafika Morogoro tunatarajia kujenga tena dry port nyingine Morogoro kwa hiyo, ikiwa kwamba zile parameters ambazo zilikuwa zimetumika, wakati wa kusanifu huo mradi wa express way ziweze kurejewa tena ili tuweze kupata mradi ambao utakuwa na manufaa. Sambamba na hilo, Serikali imefanya maamuzi inajenge Kilometa 19.2 barabara nane ambao na tayari mradi umeshaanza, kwa hiyo, yote hayo inabidi yarejewe ili kuona kwamba kama mradi huo tutautekeleza utaendelea kuwa na manufaa.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia pia kuhusu ujenzi wa viwanja wa ndege vya Kigoma, Sumbawanga, Tabora na Shinyanga. Mikataba ya ujenzi wa viwanja vya ndege vya Sumbawanga, Tabora, Shinyanga na Kigoma ilisainiwa tarehe 30 Juni, 2017 kati ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na wakandarasi wa ujenzi chini ya ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya. Utekelezaji wa miradi hii umechelewa kuanza kwa kuwa baada ya Serikali kuhamisha miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege kupeleka Wakala wa Barabara, mambo yafuatayo yalijitokeza na ambayo yamechelewesha utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Spika, moja, mfadhili ambaye ni Benki ya Uwekezaji ya Ulaya alitaka kujua taarifa juu ya mtekelezaji mpya wa mradi huu yaani TANROADS. Serikali ilielekeza kuwa TANROADS ni Idara ya Serikali inayoaminika Serikali na imetekeleza miradi mbalimbali ya wafadhili, pia imepata Hati safi za ukaguzi kwa miaka saba mfululizo. TANROADS imekuwa ikifanya manunuzi makubwa ya Taasisi nyingine kama vile TACAIDS na ujenzi wa zahanati zinazofadhiliwa na washirika mbalimbali wa maendeleo. Baada ya maelezo hayo ya Serikali, mfadhili alielewa na kukubali kwamba kazi ile sasa isimamiwe na Wakala wa Barabara.

Mheshimiwa Spika, kinachoendelea sasa hivi imebidi ku-review sasa ile Financing Agreement ili kuondoa TAA na kuweka TANROADS ili sasa no objection iweze kutoka. Sasa hivi kwa mujibu wa taarifa za Hazina ni kwamba shughuli hii ya ku-draft hiyo document ya Financial Agreement kwa kuweka TANROADS na kuondoa TAA iko kwenye hatua za mwisho kwa sababu taratibu hizi za mikopo zina taasisi nyingi za kupitia ndiyo maana uchelewaji umekuwa mkubwa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge hasa kwenye haya maeneo ambayo yamekuwa earmarked Shinyanga, Tabora, Kigoma, Sumbawanga kwamba miradi hii Waheshimiwa Wabunge itatekelezwa tuko kwenye hatua ya mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia kwamba katika miaka mitatu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miundombinu ya kimkakati. Wakataka kujua sasa kwanza impact ya utekelezaji huo, nishukuru kwamba jibu hilo amelijibu Mheshimiwa Waziri wa Fedha alipopewa zile dakika zake 10. Ziko faida nyingi siwezi kuzirudia lakini Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameshazizungumzia.

Mheshimiwa Spika, nitaomba nizungumzie kidogo kuhusu local content. Katika mradi wa SGR makubaliano kati ya Serikali na mkandarasi kuhusu ujenzi wa mradi huu, ni kwamba asilimia 35 ya malipo yanayolipwa kwa mkandarasi yafanyike kwa fedha za ndani. Lengo ni kuhakikisha kwamba, mkandarasi anatumia siyo chini ya asilimia 35 ya fedha zote za mradi katika matumizi ya rasilimali za ndani.

Mheshimiwa Spika, malighafi kama kokoto, mchanga, nondo na saruji anavyovitumia mkandarasi vyote ni vya ndani ya nchi. Aidha, matengenezo na uzalishaji wa mataruma ya zege unaofanyika hapa nchini katika Kambi za Soga na Kilosa unatumia malighafi za humu nchini. Kiasi cha saruji kinachotarajiwa kutumika katika kipande cha Dar es Salaam hadi Makutopora kwa mujibu wa mkataba ni mifuko ya cement au ya saruji 9,200,000 sawa na tani 460,000 za saruji. Kwa upande wa chuma, kiasi tani 115,000 zitatumika kutoka viwanda vya ndani. Chuma cha reli kinachotoka Japan ni asilimia 5.2 tu ya thamani ya mradi na hii ndiyo fedha ambayo tunaitoa kwenda kupeleka nje kwa hiyo ni asilimia 5.2, kwa hiyo asilimia kubwa inabaki hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, mradi utatumia mataruma 1,204,000 ambayo ni asilimia 5.6 ya thamani ya mradi wote wa malighafi zake zote zinatoka hapa nchini na zinazalishwa hapa nchini maana yake zinatumia nondo za hapa nchini, zinatumia mchanga hapa nchini, cement hapa nchini pamoja na kokoto ni hapa hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati kadhaa za Bunge lako tukufu zimetembelea maeneo haya na kujionea uzalishaji unavyofanyika kwa kutumia malighafi zinazozalishwa ndani ya nchi. Licha ya malighafi karibu zote zinazotumika katika mradi huu kuwa za ndani ya nchi ukitoa reli yenyewe ambayo inaagizwa kutoka Japan kwenye kiwanda pekee kinachotoa reli za viwango vya juu, asilimia 20 ya wataalam wabobezi katika mradi huu ni wazawa, na kwamba asilimia 80 ya wataalam wa kati na nguvu kazi ni Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa jumla ya wazawa 14,140 wamepatiwa ajira katika mradi huu ambapo asilimia 90 ni Watanzania. Ukiacha wananchi wengine wanaojihusisha na shughuli zisizo rasmi katika maeneo ya mradi, hii ina maana kwamba malipo ya watumishi hawa kiasi cha shilingi bilioni 5.2 kwa mwezi, sawa na shilingi bilioni 62 kwa mwaka ni fedha zinazotumika ndani ya nchi moja kwa moja kutoka kwa watu ambao wameajiriwa kwenye mradi. Aidha, wakandarasi zaidi ya 500 wadogo wadogo wa ndani wamepewa kazi katika mradi huu, baadhi ya kazi hizo ni pamoja na za ujenzi, ugavi na utoaji wa huduma mbalimbali ambapo wote hawa wanalipwa na fedha za mradi huo.

Mheshimiwa Spika, mbali ya faida zilizoanza kuonekana katika hatua ya ujenzi, manufaa makubwa ya mradi yataanza kupatikana baada ya ujenzi kukamilika. Mradi wa SGR unatarajiwa kuhudumia tani milioni 17 za mizigo kwa mwaka, mizigo hii ni pamoja na ile ya nchi za jirani zisizo na bandari za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kwa upande wa miradi ya barabara, viwanja vya ndege, majengo na vivuko katika mwaka wa fedha 2015/2016 hadi mwaka 2017/2018 jumla ya miradi 4,816 imetekelezwa na makandarasi wazawa na miradi 116 imetekelezwa na makandarasi wa nje. Aidha, jumla ya ajira 362,854 zilizalishwa katika sekta ya ujenzi katika miaka hiyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka 2016/2017 jumla ya ajira 109,846, mwaka 2017/2018 jumla ya ajira 116,864 na mwaka 2018/2019 jumla ya ajira 136,144 zimezalishwa katika maeneo mbalimbali ya ujenzi ikiwemo miradi ya barabara, miradi ya viwanja vya ndege, miradi ya vivuko na miradi ya ujenzi wa majengo ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nizungumzie kuhusu Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), mpaka sasa Serikali inatoa huduma kwa kutumia ndege mpya sita (6) zilizonunuliwa na Serikali kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, ndege tatu aina ya Bombadier Q4100-8 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja, ndege mbili (2) aina ya Air Bus A2200-300 zenye uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja na ndege moja aina ya Boing 787-8 Dream Liner yenye uwezo wa kubeba abiria 262. Aidha, ATCL imekabidhiwa na Mheshimiwa Rais ndege mbili zifuatazo; moja aina ya Foker 50 yenye uwezo wa kubeba abiria 44 na ya pili aina Foker 28 yenye uwezo wa kubeba abiria 70.

Mheshimiwa Spika, pia ATCL inatarajia kupokea ndege aina ya Bombader–8 mwezi Novemba mwaka huu 2019 na Boeing 787 Dream liner ambayo inatarajiwa kupokelewa Januari, 2020. Ili kuendelea kuiongezea uwezo ATCL, Serikali imetenga fedha katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2019/2020 kununua ndege nyingine moja aina ya Bombardier Q4100-8 na ndege mbili aina ya Airbus. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ATCL kwa kutumia ndege sita zinazotoa huduma kutoka Dar es Salaam kwenda katika vituo 10 ndani ya nchi vikiwemo Bukoba, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Kigoma, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Tabora, Zanzibar na vituo vitano nje ya nchi ambavyo ni Bujumbura, Entebbe, ….Harare na Lusaka. Aidha, ATCL inatarajia kufungua kituo cha Johannesburg mwezi Juni, 2019, Mumbai mwezi Julai, 2019 na Kituo cha Guangzhou kabla ya mwisho wa mwaka wa 2019. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa kuwa na safari zinazounganisha Mji wa Dodoma na sehemu nyingine za nchi, ATCL kufuatia maombi ya Waheshimiwa Wabunge imeamua kuifanya Dodoma kuwa sub-hub. Aidha, ATCL inaangalia sasa uwezekano wa kuanzisha safari za kutoka Dodoma kwenda KIA, kutoka Dodoma kwenda Mbeya, kutoka Dodoma kwenda Mwanza na kutoka Dodoma kwenda Zanzibar. Sambamba na vituo hivyo, ATCL ipo kwenye maandalizi ya mwisho ya safari za kwenda Mkoa wa Katavi Mji wa Mpanda na kuangalia uwezekano wa kuanzisha safari kati ya Dar es Salaam na Tanga kupitia Pemba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamekuwepo na dhana kwamba ununuzi wa ndege na gharama za awali na uwekezaji katika mifumo, mitambo na miundombinu zimehamishiwa kwenye Fungu 20, yaani Ikulu. Suala hili siyo la kweli kwa sababu gharama hizo zimetengewa fedha katika Fungu 62 ambalo ni la Sekta ya Uchukuzi. Aidha, gharama za uendeshaji wa ATCL zinatokana na mapato ya ndani ya kampuni kama inavyooneshwa katika hesabu za ATCL zinazokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Spika, ununuzi wote wa ndege unafanywa na Wizara yangu ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na ni Fungu 62 ambalo linapitishwa na Bunge lako Tukufu; na hata katika bajeti hii tunaomba mpitishe shilingi bilioni 500 ili tuweze kununua ndege nyingine tatu ambapo moja itakuwa ni Bombardier na mbili ni Airbus. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa wataalam marubani, ni kweli kwamba uwiano wa marubani wenye leseni katika nchi yetu kwa sasa ni asilimia 49:51 ambapo wazawa ni asilimia 49 na wageni ni asilimia 51. Hata hivyo, Serikali ina mikakati ya kuongeza marubani wazawa kwa kuwasomesha hapa nchini katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kupitia Mradi wa East African Skills for Transformation and Regional Integration Program. Mradi huu utatekelezwa kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 21.5 kutoka Benki ya Dunia na utaanza kutekelezwa rasmi mwezi Juni, 2019. Nitoe tu taarifa kwamba fedha hizi, financial agreement imeshasainiwa, tayari tunazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupitia mradi huu, chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kusomesha marubani 10 kwa mwaka. Aidha, Wizara yangu inafanya mawasiliano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu iweze kuwakopesha wanafunzi wa kozi ya Urubani. Kwa sasa ili rubani aweze kuingia katika soko la ajira atatakiwa kusoma na kupata leseni ya biashara kwa gharama ya shilingi milioni 132.6.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia ina Mfuko wa Kusomesha Marubani ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA ambao una uwezo wa kusomesha takriban marubani watano hadi 10 kwa mwaka kulingana na makusanyo katika mwaka husika. Mfuko huu mpaka sasa umesomesha wanafunzi watano ambao wameshahitimu na kuajiriwa kwenye sekta. Aidha, wanafunzi 10 wataanza masomo mwezi Oktoba, 2019. Serikali itaendelea kuhakikisha inaongeza idadi ya marubani na wahandisi wazawa katika kipindi kijacho.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia Bandari ya Mtwara na hasa Kamati yangu ya Miundombinu. Serikali ilibuni mradi wa kuboresha Bandari ya Mtwara kwa lengo la kuboresha huduma zake za sasa na wakati ujao na baadaye katika ukanda wa Mtwara. Katika kutekeleza hili, kumekuwepo na hoja ya kujengwa na kuchimbwa kwa urefu wa kina cha mita 13 badala ya 15 na urefu kati ya maji yanapojaa na sakafu ya gati ya mita tano badala ya mita 5.5.

Mheshimiwa Spika, vipimo vilivyozingatiwa wakati wa kujenga na kuchimba Bandari ya Mtwara vilitokana na ushauri wa awali uliotolewa na Mtaalam Mshauri MSURS kutoka Uingereza ambao ni urefu wa kina wa mita 13 na urefu kati ya maji yanapojaa na sakafu ya gati ya mita tano. Aidha, uchambuzi wa kina wa kitaalam unaonesha kuwa vipimo hivyo vinavyotumika ni sahihi kwa meli na shehena tarajiwa katika bandari hiyo.

Mheshimiwa Spika, Bandari ya Mtwara kutoka kwenye kina ambacho ni low tide inajaa mpaka mita nne. Kwa hiyo, ukichimba draft ya mita 13 wakati maji yamejaa, yatafika mpaka mita 17. Kwa hiyo, meli ya aina yoyote ni lazima ita- dock kwenye Bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Nditiye amezungumzia suala la usajili wa laini za simu, lakini naomba nitoe taarifa kwamba takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2018 idadi ya wananchi nchini ilikadiriwa kuwa milioni 54.2 ambapo watu 52.6 wanaishi Tanzania Bara na wananchi milioni 1.6 wanaishi Tanzania Visiwani. Aidha, asilimia 50 ya Watanzania wana umri chini ya miaka 18. Kwa kuwa zoezi la usajili wa laini za simu linamalizika mwezi Desemba, 2019 Serikali itahakikisha wananchi wenye kustahili kusajiliwa na NIDA wanasajiliwa ili kuwezesha wananchi kuendelea kupata huduma za mawasiliano zilizo salama. Kuna Waheshimiwa Wabunge walionesha kwamba pengine kuna baadhi ya vitambulisho ambavyo havitumiki, lakini nashukuru kwamba Mheshimiwa Eng. Nditiye amelizungumzia vizuri.

Mheshimiwa Spika, tunatambua uwepo wa uhitaji wa vitambulisho vingine vyenye biometria vinavyotumika kwa sasa kusajili laini za simu ikiwa ni pamoja na pasi za kusafiria, leseni za udereva, kitambulisho cha Mpiga Kura pamoja na Zan ID. Hivi vyote vinatumika katika kusajili laini za simu. Sasa hivi kuna kamati maalum ambayo inafanyia kazi. Kitu kinachotakiwa ni kwamba laini zote kwa kutumia vitambulisho vyote vinavyosajiliwa lazima visomane na lazima visomane pamoja na kitambulisho cha Taifa na hili litatusaidia kukwepa madhara tunayoyapata ya wananchi kuibiwa.

Mheshimiwa Spika, lengo letu tunataka kila laini ya simu, kila mtumiaji awe anafahamika. Kwa hiyo, kwa sasa ni vitambulisho vyote vinatumika na wataalam wapo wanaendelea na kuhakikisha kwamba wanafanya utafiti ili kwamba vitambulisho vyote hivi viweze kusomana pamoja na kitambulisho cha Taifa.

Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa na Serikali kuiongezea mtaji TTCL. Naomba pia kutoa kutoa ufafanuzi kuhusu jitihada zilizochukuliwa na Serikali katika kutoa mtaji kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania. Serikali inaendelea kutekeleza mikakati yake madhubuti ya kuboresha mashirika yaliyokuwa yamebinafsishwa lakini yakashindwa kujiendesha kwa ufanisi. Kwa msingi huo, imetunga Sheria Na. 12 ya mwaka 2017 ya kuanzisha Shirika la TTCL likiwa linamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeendelea na juhudi za kuhakikisha kwamba TTCL sasa inapewa mtaji. TTCL ilipewa kibali cha kukopa jumla ya shilingi bilioni 96 na ilishakopa shilingi bilioni 66. Sasa hivi iko kwenye process ya kumalizia kukopa shilingi bilioni 30 ili iweze kuwekeza na TTCL iwe ni Taasisi ambayo inaweza ikajitegemea. Nashukuru kwamba kwa muda mchache mwaka 2019 iliweza kutoa gawio na mwaka huu tayari imeshajipanga kutoa gawio.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetengeneza corridor tatu; ya kwanza ni ya kutoka Dar es Salaam kupitia Tanzam highway kwenda mpaka Zambia, corridor ya pili ni ile ambayo inakwenda Central Corridor na ndiyo maana tunajenga SGR, lakini tunayo corridor ya tatu ambayo inatoka Mtwara kwenda mpaka Mbambabay na ninashukuru kwamba Serikali tayari imeshakamilisha barabara ya lami kutoka Mtwara kwenda mpaka Songea na kwenda mpaka Mbinga na sasa hivi tunajenga kilometa 66 zilizobaki.

Mheshimiwa Spika, corridor hii ikishakamilika na kwa sababu sasa hivi tunanunua flow meter ili ziweze kufungwa Bandari ya Mtwara na flow meter zifungwe Bandari ya Dar es Salaam pamoja na Bandari ya Tanga, tunataka tuwezeshe corridor zote hizi ili ziweze kuhudumia nchi jirani na kujiongezea mapato.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Bandari ya Tanga tayari muda wowote mkataba utasainiwa. Nilitembelea Tanga, Tanga ilikuwa imeshakwenda chini sana, lakini tunahakikisha sasa kwamba Tanga inaamka. Kwa sababu yale magati mawili yaliyojengwa yamejengwa kwenye draft ambayo ni ndogo, maji ya kina cha mita tatu mpaka nne. Mikataba tutakayosaini tunataka tufanye dredging ili kuongeza kina kwa sababu kwa Tanga sasa hivi meli ilikuwa ikifika inakwenda kupaki mita 1,400 halafu mizigo sasa inapakiwa na matishari kuleta kwenye magati huku ambayo yanaweza yakatembea kwenye kina kidogo. Matokeo yake ilikuwa ina-discourage wenye meli kuja kuleta meli zao Tanga.

Mheshimiwa Spika, hilo tunaliondoa na hiyo ndiyo ambayo Waheshimiwa Wabunge mlikuwa mnaizungumzia. Tunapambana na Bandari majirani. Tunataka tufanye dredging na kwa mujibu wa taarifa ambayo ninayo, TPA mmeipongeza, wanatarajia mpaka itakapofika mwezi wa Tatu mwakani dredging itakuwa imekamilika. Ikishafika mwezi wa tisa wataongeza tena magati mawili yenye ukubwa wa mita 300, 300. Hii itawezesha sasa Bandari ya Tanga iweze ku-compete na bandari nyingine za jirani.

Mheshimiwa Spika, tukiwa na Bandari ya Tanga na wakati huo huo tunaendelea kukarabati Bandari ya Dar es Salaam ambayo tunafanya dredging kwenda mita 15 na gati Na.1 limeshakamilika, utaona kwa wale wanaopita Dar es Salaam sasa hivi hata kule meli zinaanza kupungua, lakini kwa ujumla, meli zinaongezeka kwa Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, malengo yetu ni kwamba tunataka tuboreshe bandari zetu na tunajenga gati lingine la shilingi bilioni 137 kwa upande wa Mtwara. Tunataka tuhakikishe kwamba meli nyingi sasa zinakuja kupaki katika Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Tanga pamoja na Bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza kuhakikisha kwamba inafufua usafiri kwenye maziwa. Upande wa Ziwa Nyasa tayari kuna meli tatu na zinafanya kazi. Upande wa Ziwa Victoria tumeshasaini mkataba wa meli moja kubwa itakayobeba abiria 1,200 na tani 400 pamoja na ujenzi wa chelezo, tunakarabati na zile meli za zamani; Mv Victoria na Mv Butiama. Kwa upande wa Kigoma tunatarajia kusaini tena meli moja mpya ambayo itakuwa inabeba abiria pamoja na mizigo na kukarabati meli ya MV Liemba. Taratibu za manunuzi zimekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachotarajia sasa hivi ni muda wowote tutasaini mkataba kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2019. Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba maziwa yote sasa yanatumika kiuchumi. Niseme tu kwamba Mkoa wa Katavi tayari tumeshapata mfanyabiashara mmoja ambaye ananunua tani 1,200 kila mwezi tutakuwa tunampelekea Congo.

Mheshimiwa Spika, pia kuna madini ambayo yamepatikana upande wa Kongo ambayo yatakuwa yanapitisha tani 2,000,000 kwa mwaka. Ndiyo maana tayari tunaendelea na mazungumzo ya pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili tuwe na matishari ya kutosha pia katika Bandari ya Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda naona unanitupa mkono, nimalizie kwa kutoa taarifa pia kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba meter gauge kutoka Dar es Salaam kwenda Isaka inaendelea na ukarabati, inafufuliwa. Meli yetu hii ya meter gauge kwenye usanifu wake ilikuwa imesanifiwa kubeba tani milioni tano kwa mwaka, lakini ilikuwa imeshuka mpaka inabeba tani 300,000. Baada ya ukarabati huo, tutarudisha sasa kwenda kwenye hizo tani zinazotakiwa.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa ushauri ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge kwamba tuangalie namna ya kuikodisha TRC ili iweze kuhudumia pamoja na reli ya TAZARA. Nimshukuru sana na Mheshimiwa Turky, leo kazungumza kitu ambacho nimewahi kukisikia mara ya mwisho wakati alipotembelea yule Waziri wa Ethiopia aliyejiuzulu. Nao nchi yao waliipeleka vizuri kutokana na hizi bond. Kwa hiyo, ushauri wako Mheshimiwa Turky nimeupokea.

Mheshimiwa Spika, baada ya haya machache, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako lipitishe kifungu kwa kifungu na lipitishe bajeti ya Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, naomba kuta hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.