Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja hii muhimu. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja hii muhimu iliyopo mbele yetu kwa asilimia mia moja. Pia nimshukuru sana Mwenyenzi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa leo. Nimshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa utashi na dhamira yake ya kweli ya kuwajali wanyonge hususan kwa kutengeneza miundombinu bora. Hii miundo mbinu itachangia kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa sababu huduma itakwenda kwa wafanyabiasha, wakulima, huduma za kijamii wafanyakazi na kadhalika.

Mheshimiwa Spika nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu kwa namna anavyosimamia shughuli za Bunge, lakini niruhusu nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi Mhandisi Isack Kamwelwe, kwa ushirikiano na miongozo anayonipa ili kutimiza majukumu yangu. Aidha, namshukuru pacha wangu Mheshimiwa Nditiye kwa namna tunavyoshirikiana katika kufanya kazi. Vile vile niwashukuru watendaji, Katibu Mkuu Arch. Elias Mwakalinga na Makatibu Wakuu wengine wote Leonard Chamuriho, Dkt. Maria Sasabo, Naibu Katibu Mawasiliano, Jim Yonaz na watendaji wengine wa Wizara nawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru wewe mwenyewe, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti namna mnavyotupa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yetu ya Wizara hii ya ujenzi. Pia inaishukuru Kamati yetu ya Miundombinu na Wabunge wote kwa ushirikiano wanaotupa ndani ya Bunge na hata nje ya Bunge. Tunaendelea kupokea maoni na ushauri wa Wabunge na sisi pia inatuboreshea kufanya kazi zetu. Vile vile niwashukuru wapiga kura wa Ushetu. Leo Madiwani wa Ushetu wapo hapa ni mashahidi, Madiwani wote hawa wa Chama cha Mapinduzi tunashirikiana vizuri na mimi kwa u-busy wangu Madiwani hawa kazi nyingi wanazifanya, Ushetu inakimbia kwa speed kubwa. Mwisho, niishukuru familia yangu Dkt. Macelina yupo hapa mke wangu, namshukuru sana kwa ushirikiano anaonipa katika shughuli zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja zilikuwa nyingi lakini ni uhakika kwamba sio rahisi kuzungumza mambo mengi sana hapa, lakini niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge ushauri wao tumeupokea na yote waliyozungumza tutayajibu na kuyawasilisha kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, nizungumze mambo machache; kwanza kwa upande wa barabara; niseme tu kazi kubwa imefanyika, mtandao wa barabara nchi nzima barabara kuu za Kitaifa tuna kilometa 36,258. Kati ya hizo barabara kuu ni kilometa 12,176, barabara za mkoa ni kilometa 24,082, lakini kati ya barabara hizo kilometa 10,061 zipo sasa kwenye matandao wa lami kwa maana barabara kuu kilometa 8,870 na barabara za mkoa ni kilometa 1,756. Niseme tu kwa miradi inayoendelea hadi Aprili ni miradi 34 ambayo itakuwa na urefu wa kilometa 1,505 na hii miradi yote ikikamika ina- commit fedha nyingi kama Wabunge walivyosema trilioni 7.799, ni fedha nyingi, lakini katika bajeti hii tuliyowasilisha kutakuwa na ongezeko, tutakuwa na miradi kama 37 kwa maana tutakwenda kuhudumia barabara kwa ujenzi wa lami kilometa 1,961 na madaraja sita, hii ni achievement kubwa. Nitumie nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais zaidi na kumshukuru Waziri wa Fedha kwa sababu waanaendelea kutuwezesha na kazi kubwa inaendelea kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumze juu ya ujenzi wa viwanja vya ndege kwa ufupi. Waheshimiwa Wabunge wengi walivyokuwa wakichangia wamezungumza juu ya miradi ya fidia, lakini niseme kwamba, mwaka 2018 tulifanya uhuishaji wa uthamini ambao awali ulikuwa umefanyika mwaka 2007. Kwa hiyo, niwahakikishie tu Watanzania kwa ujumla kwamba kwenye maeneo ambayo kwamba tuna compensation kwa mujibu wa sharia, tunahuisha ili kuona tunakwenda kulipa compensation na wananchi wanapata haki yao.

Mheshimiwa Spika, kwa wachangiaji tulikuwa na Uwanja pia huu wa Ndege wa Msalato ambapo wapo waathirika ambao wanapisha ujenzi wa uwanja 1,926. Niwahakikishie kwamba takribani bilioni 14 ambazo tunazifanyia kazi ili waweze kulipwa hawa na kwa vile uelekeo wa kupata fedha ili kujenga uwanja huu upo, kwa hiyo wananchi hawa wa Dodoma husasan eneo la Msalato nao tumejipanga pia pamoja na wengine wa maeneo mengine watapata fidia zao.

Mheshimiwa Spika, yapo maeneo mengi ambao uthamini wa mali umeendelea; Lake Manyara, kule Simiyu, kule uwanja wa ndege wa Nyerere, Musoma na Songea. Katika maeneo haya yote Waheshimiwa Wabunge walichangia, lakini tumejipanga vizuri kuendelea kufanya malipo ya fidia, kwa sababu yapo maeneo mengi pia ambapo malipo yameshafanyika, kwa hiyo, tunaendelea kufanya uhakiki tukipata fedha tuanendea kulipa.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba Waheshimiwa Wabunge pia wameuliza kwamba ni lini Serikali itaweka taa za kuongozea ndege. Kwa ufupi niseme kuwa, maeneo yote ambayo tunafanya maboresho ya viwanja vya ndege tutazingatia hili suala la kuweka taa za kuongozea ndege. Kwa hiyo katika maeneo mbalimbali ambayo tuna mradi kwa mfano kule Mafia na kule Songwe, taratibu za manunuzi zinakamilika mwezi wa tarehe 30 Aprili kwa hiyo tunaendelea kuharakisha ili tuende kufanya maboresho lakini katika maboresho tutazingatia mahitaji na vipaumbele ili viwanja hivi viweze kuwa bora na bora zaidi.

Mheshimiwa Spika, nizungumze pia kwamba uwanja wetu wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Mei, 2019 na miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege vingine katika maeneo mengine tuko kwenye harakati ya kufanya maboresho; Uwanja wa Ndege wa Songea, Uwanja wa Ndege wa Mtwara, ujenzi unaendelea kule Geita, Mwanza Nachingwea na kama nilivyosema pia na upande wa Uwanja wa Songwe tufanya maboresho makubwa ya jengo la abiria. Naona Mheshimiwa Mwakajoka ananiangalia hapa, kwa hiyo tunakwenda vizuri katika uwanja huu ili tuweze kuufanyia maboresho makubwa.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge pia wameuliza kuhusu suala la ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya Ndege vya Haydom, Kilwa Masoko, Lindi, Mafia, Manyara, Musoma, Mwanza na Tanga. Serikali inaendelea kutafuta fedha na pia inafanya mazungumzo na washirika mbalimbali wa maendeleo ikiwa ni pamoja na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na kadhalika kwa ajili ya ujenzi na ukarabari wa viwanja vyote vya ndege hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, nizungumze kidogo juu ya vivuko; ujenzi wa vivuko vipya viwili katika mwaka 2018/2019 umekamilika kwa maana ya Kivuko cha Kigongo- Busisi, MV Mwanza imekamilika na Magogoni - Kigamboni MV Kazi na pia tunaendelea kujenga vivuko vingine, kwa mfano ukarabati wa vivuko vitatu MV Sengerema, MV Kigamboni, MV Utete, lakini pia tunajenga kivuko kipya kitakachofanya huduma kati ya Kayenze na Benzi. Tumepanga vivuko hivi viweze pia ku-move kwenda pande nyingine, kivuko hiki kikikamilika ni cha kisasa, kitaweza kwenda maeneo ya Ukara kule Nansio kitatoa huduma katika maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, miradi mingine ya ujenzi wa maegesho ya Bwina kule Mkoani Geita maegesho ya kivuko kati Lindi na Kitunda, Mkoani Lindi, upanuzi wa maegesho Kigamboni pamoja na upanuzi wa jengo la kupumzika abiria. Kule ng’ambo Kigamboni tunaendelea kufanya maboresho, kuna mchangiaji mmoja hapa Mheshimiwa Mbunge alizungumza kwamba hakuna kinachoendelea, lakini tunaendelea kufanya maboresho, nafikiri labda hakuwepo muda mrefu, anaweza akajionea yeye mwenye kwamba tumejipanga vizuri ili huduma hii iweze kuboreka.

Mheshimiwa Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba amezungumza juu ya Kivuko cha Kome – Nyakalilo, tutafanya itakavyokuwa imewezekana kwa sababu tuna harakati za kujenga vivuko vingi, tunaona namna nzuri ili wananchi wapate huduma ya vivuko kulingana na mahitaji. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Tizeba kwa sababu tulipata ajali ya kivuko wakati tulikuwa tumelenga tumpelekee kivuko kwa sababu ya matatizo yaliyotokea, hivyo avumilie kidogo, tutaona namna nzuri ya ku-reallocate ili tuweze kupata huduma nzuri katika eneo hili la Kome kwenda Nyakalilo.

Mheshimiwa Spika, nizungumze juu ya maboresho makubwa na taasisi yetu ya TEMESA, Wabunge wengi wamezungumza, tunaendelea kuboresha, kumekuwa na changamoto na huduma za TEMESA, nakubaliana nao, lakini kama Wizara tumejipanga kuboresha karakana hii kwa maana ya kuongeza vitendea kazi na kuweka vifaa stahiki. Hata hivyo, kuna baadhi ya maeneo kwenye Wilaya kama kule Ifakara tumepeleka huduma na maeneo mengine tunaendelea kuwasogezea huduma wananchi ambao wanapata huduma hizi hususan taasisi za Serikali ili waweze kuzipata kwa ukaribu zaidi. Tunalenga kwenda kupeleka huduma hii katika Wilaya 25.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie juu ya huduma ya majengo na nyumba za Serikali. Imetolewa hoja kwamba gharama ni kubwa katika ujenzi, lakini nilikuwa nimejaribu kufanya mapitio kwamba pamoja na changamoto nyingi ambazo zipo kwenye TBA, Wizara inaendelea kushughulikia ikiwepo tatizo la wafanyakazi, tunaendelea kuongeza wafanyakazi ili tuweze kuboresha huduma hizi. Tulifanya utafiti kuona kwamba zile huduma za ujenzi bado zipo chini kwa miradi kadhaa, mfano, ujenzi wa mabweni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tulijenga kwa bilioni 10, lakini wengine waliwasilisha gharama za ujenzi kwa bilioni 90. Pia gharama za ujenzi wa shule ya sekondari Ihungo wengine walituletea kwa bilioni 60 hadi 200, lakini Wakala walijenga kwa bilioni 12. Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita bilioni 17 ndio TBA wanajenga, lakini wengine walituwekea bilioni 67. Sasa utaona gharama zipo chini kati ya wastani wa 30% hadi 40%.

Mheshimiwa Spika, niseme jambo moja hapa ambalo Waheshimiwa Wabunge walizungumza juu ya kufanya uchunguzi kuhusu baadhi mikataba ambayo imehusika kwenye ujenzi wa shule kongwe, sisi Wizara tupo tayari tutaunda timu ambayo itahusisha wafanyakazi wa AQRB, CRB na ERB ili kupitia upya mikataba yote na tuweze kupata ushauri kupata ushauri ili tuweze kuchukua hatua stahiki.

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kusema Mheshimiwa Kingu alizungumza kwa uchungu hapa kuhusu barabara za Singida. Kwanza Mheshimiwa Kingu nimpe faraja kwamba katika bajeti hii tutatengezea barabara za mzunguko kwenye Mkoa Singida, kilometa 46 kwa mapendekezo ambayo yapo mbele ya meza. Hata hivyo, nimhakishie kwamba kwenye eneo la kutoka Singida kwenda Mgungila kwamba katika bajeti ya mwaka huu inayoendelea 2018/2019, tulikuwa tumetenga zaidi ya milioni 150 kwa ajili ya kuboresha, kujenga madaraja katika maeneo ambayo ni korofi na kuweza kuanza kunyanyua tuta. Kiasi cha fedha ambacho kinaonekana hapa ni kwa ajili ya kuendelea kufanya maboresho katika eneo hili na maeneo mengine, muda hautoshi, nafahamu kwamba yapo maeneo mengi ambayo kwenye Mkoa wa Singida kama alivyosema Mheshimiwa Kingu tunaendelea kufanya maboresho mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, ningezungumza kidogo kwa kumalizia kuhusu ule mgawanyo wa fedha wa Mfuko wa Barabara. Niseme tu kwamba mgawanyo wa fedha upo kisheria, ni suala la kuangalia sheria lakini kwa upande wa Wizara kupitia, Bodi Mfuko wa Barabara tumeweka mshauri ili aweze kufanya mapitio tuone namna nzuri wa kufanya mgao huu wa fedha za TARURA na upande wa TANROADS. Hili zoezi linafanyika kwa sababu pale awali mgawo ulikuwa 80% kwa 20% kabla haujaenda 70% kwa 30% kwa mujibu wa sheria ilivyokuwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaendelea kukamilishia hili zoezi ili tuone urefu wa barabara, network nzima ili tuweze kuona matumizi ya barabara kwa sababu ndio bases kwamba ni vyombo vingapi, uzito upi unapita kwenye barabara zetu ili sasa tuweze kuona namna nzuri namna nzuri ya kufanya mgawanyo wa barabara hizi, pia tutazingatia hali ya jiografia. Ili twende vizuri wenzetu Wizara ya Fedha pia wanalifanyia kazi jambo hili na tukiweza kuongea fedha za ujenzi wa barabara tutaendelea kuziboresha barabara zetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana kwa nafasi hii na nimalizie kwa kusema kwamba, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)