Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Kamwelwe, Manaibu Waziri Mheshimiwa Kwandikwa na Mheshimiwa Nditiye. Naishukuru Serikali kwa utekelezaji wa ujenzi wa Gati la Nyamisati. Gati hili ujenzi wake unakaribia kwisha na matarajio ni kufikia mwezi Juni mwaka huu. Tunashukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Spika, pia naishukuru Serikali kwa kutenga fedha za kujenga kivuko kipya kati ya Nyamisati na Kilindoni pamoja na ukweli kuwa kivuko hiki kilishatengewa fedha katika mwaka wa fedha 2018/2019 na mchakato wa kumpata mkandarasi ukaanza, lakini kwa masikitiko, kandarasi hii imefutwa kutokana na matatizo ya kisheria. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atupie macho utendaji wa Wakala wa Ufundi Umeme na Mitambo (TEMESA), wahakikishe mchakato wa ujenzi wa kivuko hiki cha Nyamisati na Kilindoni.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kivuko cha muda tulichopewa na Serikali kivuko kinachomilikiwa na Chuo cha Mabaharia (DMI), mpaka ninapoandika hapa bado hakijaanza kazi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri atie msukumo wa kuhakikisha boti hii inaanza kazi mara moja na hasa ukizingatia Gati la Nyamisati linakaribia kumalizika.

Mheshimiwa Spika, Gati la Kilindoni lipo katika hali mbaya sana, mbao zimechoka na ngazi ya kupanda na kushuka inakatikakatika mara kwa mara na kuhatarisha usalama wa abiria na mali zao. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) walishaahidi kufanya matengenezo makubwa ya gati hili. Kukamilika kwa Gati la Nyamisati itakuwa hakuna maana kama Gati la Kilindoni litakuwa bado bovu.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi kilomita 45 ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na imo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020. Mpaka sasa upembuzi wa kina na usanifu umeshakamilika, bado kutengewa fedha za ujenzi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri chonde chonde ujenzi wa matengenezo ya muda wa (periodical) maintenance) unakuwa mgumu kwani udongo wa kufanyia matengenezo unakaribia kwisha. Hivyo ni bora barabara hii ikajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, Uwanja wa Ndege wa Mafia; tunaomba uongezwe urefu sambamba na kuwekwa taa ili kuwezesha ndege kubwa za Kimataifa kutua moja kwa moja na kukuza utalii sambamba na ujenzi wa jengo la abiria (Terminal building)

Mheshimiwa Spika, suala la mawasiliano katika Kisiwa cha Mafia bado ni changamoto katika Vijiji vya Miburani, Banja, Kitohi na Chemchemi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.