Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Mwanne Ismail Mchemba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii na mimi niweze kuchangia kutoa machache ambayo niliiyokuwa nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kumpongeza Mheshimiwa Profesa Ndalichako, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu, pamoja na watumishi wote wa Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba nimeipitia, sijasoma yote lakini nimeielewa. Pia nishukuru Mungu kwamba leo Mheshimiwa Simbachawene yupo, kwa hiyo, haya nitakayoyasema na yeye pia yatamgusa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora una historia kubwa sana ya suala zima la elimu, ina historia kubwa mno, lakini Tabora inaongoza kwa kuwa na shule zenye vipaji maalum. Shule za vipaji maalum hazijawahi kushika nafasi kumi bora, kwa nini hazijawahi kushika? Shule hizi zimetelekezwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini shule hizi hawasomi wakazi wa Tabora, wanafunzi wa Tabora, ni wanafunzi wa nchi nzima ambao wanapelekwa kusoma kama vipaji maalum lakini wakishuka pale getini vipaji maalum havipo. Kwa sababu Tabora Boys ina historia hata ya Baba wa Taifa, Milambo ina historia ya Baba wa Taifa, Tabora Girls ina historia kubwa mno, viongozi wengi wemetoka Tabora Girls hususani wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mazingira yaliyopo katika shule hizi hayafai, watoto wanaokwenda pale wanateseka, miundombinu ni mibovu. Wanafunzi wanaokwenda pale hata kama walikuwa na shida ya kusoma hawawezi kusoma. Miundombinu ambayo naizungumzia hakuna maji, umeme na miundombinu ya shule zile hazijafanyiwa ukarabati miaka dahari na dahari. Kwa hiyo, wale wazazi wanaowapeleka watoto kwa sababu wako mbali anaambiwa tu mtoto amefaulu anampeleka lakini mazingira ni magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali sasa iangalie kwa nini shule hizi hazipati nafasi ya kushika nafasi kumi bora, lakini kama tutakuwa tunawalaumu walimu hatuwatendei haki. Shule ya Tabora Girls ni ya wasichana, shule ile tumeomba kujenga uzio takribani sijui miaka 30 sasa, shule ile ni pana, wanafunzi wale mabweni ni mabovu, tunajitahidi sana kusema uzio ule ukamilike lakini wanafunzi wanaogopa kwa sababu panapokuwa hakuna uzio usalama wa watoto wa kike ni mdogo. Usalama wa wanafunzi wale kwa sababu ni wanawake wanaogopa na ni kweli wanateseka, kwa sababu ikifika usiku hawawezi kutoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali yangu kwa sababu ni sikivu iangalie usalama wa wale wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana, wanateseka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu, wanapokosa maji, wanafuzi wa kike, wanawake wote mliomo humu mnajua. Mnajua adha ya mtoto wa kike anapofika katika siku zake anavyoteseka kwenda kutafua maji. Wanawake wenzangumimi niombe Wizara hii ilete mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba shule zote nchi nzima ambazo wasichana wanasoma wapewe kipaumbele za taulo. Kwa sababu kwa kweli aah, mimi siwezi kusema mengi lakini wanawake tunajua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule hizi kuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi, hakuna unategemea nini, niombe madamu tunaita shule za vipaji maalum basi Serikali iwape kipaumbele ili walimu hawa wa sayansi waweze kufika huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia madai ya wazabuni. Wazabuni hawa ndio wanaohudumia hawa watoto, shule hizi ni kama za watoto yatima, wanapokosa huduma chakula ni matatizo, hawana mahali pa kushika. Kwa mfano, kuna wadai wa zabuni wanadai tangu mwaka 2011 Mheshimiwa Ndalichako. Na ndio maana nimesema Mheshimiwa Simbachawene alipate hili, mwaka 2011 wazabuni wanadai, mwaka 2013 wanadai, mwaka 2014 wanadai, hawajapewa fedha zao. Hawa watu wengine wanakwenda kwenye mikopo lakini unategemea watawahudumia wanafunzi? Kwa hiyo mimi niombe hili wasipolitolea ufafanzu wa madai ya wazabuni patakuwa hapatoshi hapa, nitashika mshahara wa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora, pia tuna chuo cha elimu cha Walimu, nacho kimetelekezwa, miundombinu hovyo, hivi unategemea mwalimu anayejifunza kwa tabu atakwenda kufundisha huko mnakompeleka? Kwa hiyo ningeomba Chuo cha Ualimu Tabora kiangaliwe na kipewe nafasi ya kukarabati miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu nizungumzie habari ya Chuo cha VETA. Chuo cha VETA ni kikubwa mno na majengo mazuri sana kuliko Chuo cha Chang‟ombe. Lakini VETA Tabora haijatangazika, hakuna, hata ukisoma humu hutapata maelekezo ya Chuo cha VETA Tabora, hakipo. Chuo cha VETA Tabora au nchi nzima watu wengi wanafikiri chuo cha VETA ni wale walioshindwa darasa la saba, sio kweli. Tukiviendeleza vyuo vya VETA nchi nzima tutatoa wataalam wazuri kuliko wa chuo kikuu kwa sababu hawa ni watu ambao wanajituma na hawa watakuwa na uchungu wa maisha. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali yangu iangalie ni jinsi gani itaweza kuwasaidia wanafunzi wanaomaliza VETA kuwapa vitendea kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tusipowapa vitendea kazi anamaliza kusoma akishamaliza kusoma unamwambia nenda kajiajiri, anaenda kujaajiri wapi. Wapewe mikopo, wakishapewa mikopo wanaweza wakafanya kazi nzuri ambayo itasaidia pia na wao kuwaendeleza katika maisha yao. Lakini nishukuru pia Serikali kuunganisha VETA na FDC. FDC nayo ilikuwa imekufa, ilikuwa haipo, lakini ndio ilikuwa inasaidia mpaka vijijini, kwa sababu vyuo vingi viko mjini, lakini FDC ililkuwa inakwenda mpaka vijijini watu wanapata elimu ambayo ilikuwa inawasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI washirikiane kikamilifu kuisaidia Wizara hii ya Elimu ambayo ndio inayotambuliwa ingawa ni mtambuka, lakini kuipeleka TAMISEMI Wizara ya Elimu ni kama kuionea. Kwa sababu kila mtu anayejua ukimwambia habari ya TAMISEMI haelewi, walimu wana madai yao, wana madai mengi kwa sababu TAMISEMI wameelemewa na mzigo mkubwa, afya imeenda huko, elimu imeenda uko, sijui nini wamepelekewa huko, mara wakusanye kodi huko huko, ardhi huko huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa naomba kwa heshima na taadhima Wizara hizi zikae chini na zifanye mambo ambayo watanzania wataridhika, wataelewa, jamani msione hivi walimu wanapata taabu kubwa mno tena kuwe na fungu maalum la kuwakopesha walimu hata magari, hivi Serikali inashindwa kudhamini walimu wakopeshwe magari ambayo watakuwa wanakatwa kwenye mishahara yao, hiyo nayo itatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nyumba za walimu, nyumba za walimu hata hizi shule nazosema za vipaji maalum ziko hovyo, haziko katika mazingira ya kumfanya mwalimu ambaye anastahili kufundisha shule zile. Ahsante nashukuru sana naunga mkono hoja asilimia mia moja.