Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu kwa manufaa ya wananchi wa Mkoa wa Mara na Watanzania wote kwa ujumla. Tunaona bajeti kwa miaka mitatu zimetengwa shilingi trilioni 13, nataka Serikali itueleze tunapata ajira kiasi gani na return yake ni nini? Fedha nyingi zinaenda kwenye upembuzi yakinifu, sijui huu upembuzi yakinifu utaisha lini ili ujenzi kamili uweze kuanza kwa sababu Wilaya ya Rorya, TARURA haijapata fedha za maendeleo ya barabara kwa miaka miwili mfululizo sasa.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Musoma – Busekela ni ya kilometa 42, lakini fedha zilizotolewa ni kilometa tano tu, bado kilometa 37. Zitaishaje bila fedha? Naishauri Serikali ipeleke fedha za kumalizia hizo kilometa 37 zilizobakia.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Wanyere – Kitaryo imekatika, hakuna mawasiliano sababu ya daraja. Kwa sababu Wizara hii imetengewa fedha nyingi, naishauri Serikali ifanye jitihada za haraka kuhakikisha inatengeneza barabara hii na daraja ambalo limeshaua watoto zaidi ya 20 ili kunusuru maafa mengine yasitokee.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mara una miradi viporo vingi sana kama vile Bunda – Kisorya, Makutano – Sanzate, Mugumu – Tabora B zinazohitajika fedha ili kuweza kukamilisha miradi hii viporo.

Mheshimiwa Spika, kuna round about ya Tarime inasababisha ajali za mara kwa mara. Naishauri Serikali iondoe hiyo round about badala yake ziwekwe taa za kuongozea kama vile Barabara ya Mwenge kwenda Mikocheni, Kawe, Mjini, Ubungo ili kuepusha ajali zinazotokea mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mara una uwanja wa ndege ambao unapanuliwa (unaongezwa), kitu ambacho kinaathiri wananchi wanaozunguka (waliopakana) na uwanja huo kwani wananchi hawa walishafanyiwa tathmini takribani mwaka na miezi minne, lakini wananchi hawa hadi sasa hawajui hatma yao kwani tathmini imefanyika bila wao kujua nyumba zao zimefanyiwa tathmini ya shilingi ngapi.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ikarudie kufanya tathmini na suala hili liwe shirikishi kwa wananchi wenyewe na Serikali iwatengee (iwape) eneo lingine la kwenda kujenga nyumba nyingine pale ambapo watakuwa wameshalipwa fedha za kupisha uwanja wa ndege.

Mheshimiwa Spika, TBA hawafanyiwi ushindani na makampuni binafsi ndiyo maana kazi za TBA ni substandard (kazi nyingi za Serikali zinafanywa na TBA matokeo yake majengo mengi hayakidhi viwango). Mfano mradi wa nyumba Bunju zinazojengwa na TBA haziko competitive hata kidogo kwani haziwezi kuingia kwenye ushindani kwa vile hazina viwango. Kwanza hazina (hakuna) social services kama vile zahanati, shule, barabara na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nyumba hizi hazinunuliwi? Ni kwa sababu bei iko juu sana kulinganisha na ubora wa nyumba zenyewe, kwani hadi sasa nyumba zilizonunuliwa ni chache sana, nyingi hazijanunuliwa, zimekaa tu na kuendelea kuharibika. Naishauri Serikali, hizi nyumba zipangishwe badala ya zinavyokaa zenyewe bila watu.

Mheshimiwa Spika, lingine katika Sekta ya Ujenzi; kati ya wakandarasi Watanzania asilimia 80, ni wakandarasi asilimia 20 tu ndiyo wanaopata kazi. Ni aibu kwa nchi yetu ya Tanzania. Ushauri wangu ni kwamba Serikali itoe ujuzi kwa Wakandarasi wetu ili tuweze kuwatumia kuokoa pesa zinazokwenda nje.