Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, kupitia njia ya maandishi nichangie bajeti ya Wizara hii muhimu katika ujenzi wa Taifa imara. Rejea ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kwa sekta zote inaonyesha dhahiri kuwa ujenzi wa uchumi wa viwanda uko kwenye uelekeo sahihi na kasi inayotakiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba na kushauri TPA wakamilishe ujenzi wa mradi wa gati la Kyamkwikwi. Ukamilishaji wa mradi huu utawezesha sekta binafsi kujua mipaka ya mradi na kuweza kuendeleza eneo lililobaki.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Tano, kupitia Wizara hii kwa uwekezaji katika vivuko. Naomba Wizara ifikirie maombi ya kupatiwa vivuko (pantoni/ferry).

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2012 nimekuwa nikiomba kivuko kwa ajili ya visiwa vya Bumbiile, Kelebe na Goziba. Kutokana na jitihada na mafanikio ya TPA kukamilisha ujenzi wa gati Kyamkwikwi, ni busara kijamii na kiuchumi kuweka vivuko ili tusaidie na kuokoa wananchi wanaosafiri ziwani.

Mheshimiwa Spika, Tanzania upande wa Mkoa wa Kagera tunayo mahitaji ya uwanja wa ndege mkubwa. Tunaomba na kushauri Serikali kwa njia zote isaidie uchumi wa mkoa huu kwa kuwekeza katika upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba au tujenge uwanja mpya sehemu ya Omukajunguti. Hoja hapa ni kuwa na uwanja wa ndege ambao utawezesha ndege za mizigo kutua. Kagera ina fursa ya kuvutia; viwanda vya samaki na uzalishaji wa matunda na mboga kiurahisi kipindi chote cha mwaka.

Mheshimiwa Spika, nitoe pongezi na maombi kwa TANROADS kupitia kwa Mheshimiwa Waziri na watendaji wake wote. Barabara ya Muhutwe – Kamachumu – Muleba ujenzi unaendelea, hasa sehemu hii ya Muhutwe – Kamachumu. Naomba sehemu hii ya Muhutwe mpaka Kamachumu isimamiwe ili ikamilike kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Spika, vile vile kipande cha Kamachumu/ Ibuga mpaka Rutenge tunaomba kipigwe lami hasa ile sehemu ya Kamachumu Islamic School ambacho ni eneo korofi.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwaomba TANROADS kupitia Wizara kuboresha barabara za TANROADS za Rutenge – Bulyakashaju – Rubale – Izimbya – Kara. Barabara hii ni muhimu kwa kuwa inaunga Wilaya ya Muleba, Bukoba na Karagwe. Eneo ipitapo barabara hii ni mkanda muhimu kiuchumi kwani inalengwa kuwekeza ufugaji wa ng’ombe wa kisasa na kilimo.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuipongeza TPA kwa utendaji wa bandari wa sasa. Bandari hii kwa sasa inafanya kazi masaa 24 kwa siku, siku saba za juma. Ushauri ni Serikali kuhakikisha jamii yote za bandari (Port Community) kushirikiana ili kuongeza ufanisi mkubwa. Eneo moja dogo la kutolea mfano ni ukosefu wa ushirikiano wa TPA na TANROAD katika kupima mizigo, hali inayopelekea foleni eneo la Kurasini.

Mheshimiwa Spika, ni rahisi magari yanayotoka bandarini yapimwe yote uzito ndani ya eneo la bandari. Kazi hii inaweza kufanyika chini ya wadau wote wenye maslahi ikiwemo TANROADS na baada ya hapo magari yasipimwe au kusimamishwa mpaka yatoke eneo la jiji. Faida moja kubwa ni kuondoa foleni hali ambayo itaongeza kasi.

Mheshimiwa Spika, yapo madai kuwa bandari za Nakura, Beira, Durban na hata njia za Angola ni washindani wa bandari za Tanzania hasa Dar es Salaam. Kimsingi wateja wote wanaopita njia hizo wamelazimika kupitia huko baada ya njia ya Tanzania kuwa na vikwazo. Nashauri Serikali ziangalie maslahi mapana na kwa pamoja naomba vikwazo hivyo ili kuchangamka kwa biashara ya TPA kulete neema kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.