Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, naungana na wote waliotangulia kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Mimi ni shahidi wa kazi inayoendelea barabara ya Sanya Juu - Kamwanga.

Mheshimiwa Spika, naomba baada ya mkataba wa Ujenzi wa barabara ya Kiboriloni –Kikarara, Tsuduni – Kidia kusainiwa, tunaomba sasa ujenzi uanze kwa kasi kabisa baada ya subira ya miaka zaidi ya saba.

Mheshimiwa Spika, vile vile tunaomba sehemu ya barabara ya kutoka Chuo cha Wanyamapori – Mweka hadi lango la Mlima Kilimanjaro ijengwe kwa kiwango cha lami ili kuondoa kero kwa watalii, kwani ni ya charangawe na ni nyembamba sana. Bahati nzuri mvua nazo katika eneo hilo ni nyingi, hivyo kupelekea watalii kusukuma magari badala ya ku-enjoy safari.

Mheshimiwa Spika, pongezi kwa kazi nzuri iliyofanywa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Marangu na Machame kuelekea Mlima Kilimanjaro, imesaidia kuboresha mazingira ya utalii.

Mheshimiwa Spika, ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara ni jambo kubwa na zuri. Ni vizuri ushirikishwaji huu ufanyike kwenye Wilaya zote nchini. Kuna kazi za ujenzi wa barabara katika wilaya zetu zinazoweza kutekelezwa na wanawake. Nashauri mwongozo wa Wizara kuhusu suala hili uelekeze kila Wilaya kutoa mafunzo kwa wanawake na kuweka asilimia ya kazi ambazo lazima zifanywe na wanawake.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha agusie mafunzo ya utunzaji barabara kwa jamii. TANROAD na TARURA watoe mafunzo hayo.

Mheshimiwa Spika, kero kwa wale waliopita barabara ya Arusha - Moshi siku za karibuni watakubaliana nami kuwa hii ni moja ya barabara yenye msongamano mkubwa wa magari. Inachukua muda wa saa tatu kusafiri umbali wa kilometa 85 Tengeru - Himo.

Mheshimiwa Spika, tunaomba mazungumzo kati ya Serikali na JICA yakamilike mapema ili hatimaye upanuzi wa barabara kutoka Tengeru hadi Himo ufanyike kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.