Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kutumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kufika mahali hapa nami niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, kama inavyojieleza, hotuba hii inakwenda kutatua changamoto mbalimbali na kutekeleza miradi ya kimaendeleo inayogusa sekta husika za ujenzi, uchukuzi na mawasiliano. Aidha, inakwenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoainishwa. Pia nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kuandaa hotuba nzuri yenye malengo chanya.

Mheshimiwa Spika, napenda kuanza kuchangia kwa kuipongeza Serikali katika jitihada zake za kuendelea kuhakikisha nchi yetu inakua na barabra nzuri zinazopitika wakati wote. Lengo kuu la Serikali ni kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami ili kuimarisha na kurahisisha mawasiliano ya usafiri na usafirishaji wa watu, bidhaa na mazao mbalimbali. Ni jambo la kujivunia sana kwani hadi kufikia Februari 2019, jumla ya kilomita 266.78 za barabara kuu za mikoa zimekamilika na kilomita 392.2 zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami. Vilevile katika jitihada zilezile Serikali imekamilisha ujenzi wa madaraja matano katika Mto Lukuledi (Lindi), Mara (Mara), Sibiti (Singida), Momba (Rukwa na Songwe) na Mlalakuwa (Dar es Salaam) na ujenzi wa madaraja 8 unaendelea katika sehemu mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miradi hii, utatoa fursa mbalimbali kwa wananchi kupata ajira pamoja na kupata soko kwa bidhaa na mazao yao. Aidha, utasaidia sana kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini ikizingatiwa miundombinu yetu ni mizuri.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, bado naendelea kuipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza ujenzi wa miradi ya barabra inayolenga kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa barabara kuwezesha mradi wa kuzalisha umeme wa Stigler’s Gorge kwa kiwango cha changarawe kutoka Ubena Zomozi mpaka Selous kilomita 177.6 na ukarabati wa barabara ya kutoka Kibiti - Mloka – Selous – Mpenda (Km 370), Makutano – Natta – Magumu - Liliondo (Km 239) na Loliondo - Lumecha (Km 464). Haya yote kwa ujumla yamefanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi yenye viongozi imara wenye kutekeleza yale yote yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ikiongozwa na Rais wetu shupavu na mpenda maendeleo.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa awamu ya kwanza wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kwa asilimia 42.8 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2019. Hali kadhalika, ujenzi wa awamu ya pili wa reli hiyo ya kisasa kutoka Morogoro - Makutupora Jijini Dodoma umefikia asilimia 6.07. Hadi sasa mradi kutoka Dar es Salaam - Makutupora umeshaajiri wafanyakazi wazawa wapatao 6,335 sawa na asilimia 90 ya wafanyakazi wote. Ni jambo la kupongezwa kwani limezalisha ajira kwa watu wetu na kuna faida kubwa mradi husika utakapokamilika.

Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa reli mpya ya kisasa, Serikali katika mwaka 2018/2019 imeendelea na kazi ya kuboresha, kujenga na kukarabati miundombinu ya reli ya kati kwa kuondoa reli zote nyepesi na kuweka reli mpya zenye uzani wa paundi 80 kwa yadi kati ya stesheni ya Dar es Salaam na Isaka. Aidha, kazi ya ukarabati wa reli ya Tanga- Arusha imekamilika kwa sehemu ya Tanga – Same (Km 199). Hata hivyo, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea na kazi ya ujenzi wa reli ya kisasa, ukarabati wa ujenzi wa reli ya kati na nyingine ikiwemo ya Tanga – Arusha ili kuimarisha huduma za usafirishaji na biashara kwa ujumla. Miradi hii inatekelezwa chini ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Rais wetu anayetekeleza Ilani ya Chama.

Mheshimiwa Spika, tumeendelea kuwa na changamoto ya msongamano katika Jiji letu la Dar es Salaam na imejitokeza pia katika baadhi ya miji, lakini Serikali imefanya na inaendelea kufanya jitihada kubwa kutekeleza miradi ya kuondoa msongamano wa magari kwenye Jiji la Dar es Salaam ili kurahisisha usafiri na usafirishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi kwani Jiji hili lina bandari kuu ambayo huchangia pato la nchi kwa kiasi kikubwa. Hivyo, jitihada hizi zinafanyika kulingana na hali halisi iliyopo.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa mradi wa barabara ya juu ya Mfugale na miradi mingine inayoendelea. Miradi ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya Ubungo (Ubungo Interchange), upanuzi wa barabara ya Kimara Mwisho - Kiluvya (Km 19.2) kutoka njia mbili kuwa nane. Katika mradi huu upanuzi wa hii barabara ya njia nane, naishauri Serikali mradi huu uweze kuishia mizani ya Vigwaza. Kwa kufanya hivyo kutasaidia sana kupunguza msongamano ambao sasa pia umeanza kujitokeza katika Mkoa wetu wa Pwani hasa Kibaha.

Mheshimiwa Spika, aidha, pongezi hizi pia zinakwenda katika mradi mpya wa daraja jipya la Salender na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka awamu ya II na III. Hata hivyo, katika mradi wa mabasi yaendayo haraka kwa awamu ya kwanza kumejitokeza changamoto mbalimbali na za muda mrefu ambazo wananchi wamekuwa wakizilalamikia za uhaba wa mabasi, abiria kujaa kwa wingi na kwa muda mrefu kwenye vituo vya mabasi hayo. Pia changamoto ya uwepo wa baadhi ya mabasi ya express, mabasi haya ya express hayana tija kwa kuwa miundombinu ya mabasi haya yenyewe yanajitosheleza kufika kwa haraka. Kero ya mabasi haya ni pale yanapoacha abiria vituoni ili hali kuna uhitaji, athari zake ni abiria kuzidi kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kama ifuatavyo, mabasi yote ya express yarudishwe katika hali ya kawaida ili kukidhi mahitaji kwa sababu hivi sasa mradi unakabiliwa na uhaba wa mabasi. Kufanya hivyo, kutasaidia kupunguza mlundikano wa abiria katika vituo vya mabasi. Aidha, naishauri Serikali katika mradi huu wa mabasi yaendayo haraka awamu ya pili ufike mpaka Kibaha. Kuleta mradi mpaka Kibaha kutarahisisha usafiri kwa wananchi kwani mkoa wetu sasa umekua hasa Kibaha tunaongezeko kubwa la watu wanaokuja kuishi na kufanya shughuli zao mbalimbali, pia ni eneo ambalo linakua kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kuanzisha treni ya moja kwa moja kutoka Posta hadi Mlandizi. Uwepo wa treni hii utakuwa na tija kwani treni inabeba abiria wengi kwa wakati mmoja ukilinganisha na usafiri mwingine. Mfano tumeona mabasi yetu yanayotumika katika mradi wa mabasi yaendayo haraka, mabasi haya ni ya gharama kubwa, utunzaji wake pia ni wa gharama pamoja na vipuri vyake. Hali hiyo inapelekea mabasi haya yanapoharibika kuchukua muda mrefu kukarabatiwa na hivyo kupunguza ufanisi wa mradi huu lakini tutakapokuja na treni itatusaidia sana kupunguza adha hii ya usafiri.

Mheshimiwa Spika, aidha katika mradi huo wa treni, naishauri Serikali kwenye kila kituo treni itakaposimama kujengwe maegesho ya magari ya kulipia ili wananchi wanapotoka katika maeneo yao wanaacha magari yao hapo na kupanda treni. Hii itasaidia kuingiza kipato katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine inayotukabili wana Kibaha Vijijini ni kukosekana kwa mawasiliano ya uhakika. Kuna maeneo hakuna minara na hivyo kuifanya dhana nzima ya uchumi wa viwanda kuwa ngumu, kwani mawasiliano ya simu ni muhimu, yanakwenda sawia na dhana nzima ya uchumi wa viwanda. Maeneo hayo ni Ruvu Station, Ruvu kwa Dosa, Kipangege, Miande, Dutuni, Madege, Lukunga, Videte, Boko Mpiji, Kwala, Mperamumbi Msua na Waya.

Mheshimiwa Spika, hapana shaka yoyote juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara kama nilivyokwishapongeza hapo awali. Katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa mikoa ambayo haijaunganishwa na barabara kuu za lami. Kibaha Vijijini tuna changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara, tuna bandari kavu Kwala ambayo kwa kiasi kikubwa inakwenda kuleta mapinduzi makubwa sana lakini barabara zake haziridhishi. Naiomba Serikali kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Vigwaza- Kwala kwani ikiwa katika kiwango cha lami itavutia wawekezaji kuja kuwekeza eneo hili na kurahisisha uchukuaji wa mizigo.

Mheshimiwa Spika, aidha, tuna changamoto ya barabara za Chalinze – Magindu, tunaomba ijengwe kwa kiwango cha lami. Hata hivyo, kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa SGR lakini barabara hii inayoelekea katika mradi huo kuanzia Kongowe – Soga ilipo karakana tunaomba ijengwe kwa kiwango cha lami. Kwa sasa maeneo yale kutokana na mradi huu shughuli za kiuchumi zimekua kwa kiasi kikubwa, kujengwa njia hii kwa kiwango cha lami kutazidisha kasi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Makofia- Mlandizi - Mzenga ni ya muda mrefu. Barabara hii imeongelewa hapa Bungeni tangu Mbunge wa kwanza hadi awamu yangu nimekuwa nikiisema hapa Bungeni ijengwe kwa kiwango cha lami lakini hadi leo hatujapata majibu ya kuridhisha ama utekelezaji. Barabara hii ina umuhimu mkubwa kwani inaunganisha Majimbo takribani manne ya Bagamoyo, Mkuranga, Kibaha Vijijini na Kibaha Mji. Kwa umuhimu wake, hakika barabara hii inahitaji ijengwe kwa kiwango cha lami hasa ikizingatiwa kila Mbunge aliyewahi kuongoza Jimbo hili amewahi kuizungumzia.

Mheshimiwa Spika, wakati wa kipindi cha kampeni mgombea wa nafasi ya Urais wakati huo ambaye hivi sasa ndio Rais wetu, alituahidi wana Kibaha Vijijini kujengewa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 10. Hii ni ahadi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo mpaka leo hii tumebakiza takribani mwaka na nusu wa kumaliza kipindi cha miaka mitano haijatekelezwa. Ni aibu kwa Chama kwani tukirudi tena kuomba ridhaa kwa wananchi hawa tutawaambia nini? Ni vema ahadi zote za Mheshimiwa Rais alizoahidi kutekelezwa kwa wakati kabla hajamaliza muda wake. Namuomba Mheshimiwa Waziri wakati wa majumuisho atupatie majibu ya hoja hizi ili nasi wana Kibaha Vijijini tuwe na matumaini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.