Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawawiliano.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nashukuru kwa ujenzi wa Gati la Nyamisati lililogharimu shilingi bilioni 14 na kazi inaenda vizuri sana. Nina kila sababu ya kujivunia Serikali yangu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi yake nzuri. Kweli huyu ni mzalendo namba moja kwa kujali wananchi wa hali ya chini, wanyonge, kwani gati hili likikamilika litatua changamoto za usafiri kwa wananchi wa Wilaya ya Mafia na Kibiti.

Mheshimiwa Spika, lakini kila penye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto. Barabara yetu ya Bungu- Nyamisati, naomba ijengwe kwa kiwango cha lami kwani kipindi cha mvua huwa haipitiki kabisa kwa hiyo huwaletea usumbufu wananchi hasa wa Wilaya ya Mafia na Kibiti. Naiomba Serikali yangu sikivu ituangalie kwa jicho la huruma. Vilevile, barabara ya kutoka Muhoro - Mbwera nayo ifanyiwe ukarabati wa kiwango cha changarawe kwani ina manufaa makubwa ukizingatia sasa kuna ujenzi mkubwa wa Kituo cha Afya-Mbwera.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kibiti lina jumla ya kata 16, vijiji 58 na vitongoji 272. Kati ya hivyo, baadhi yake vipo kwenye visima/delta au pembezoni mwa Bahari ya Hindi ambavyo vina jumla ya kata 5, vijiji 17 na vitongoji 42. Moja ya changamoto ya maeneo hayo ni kutokufikika kwa urahisi, miundombinu yake ya barabara siyo mzuri kabisa kama maeneo ya Kata za Msala, Mbuchi, Kiongoroni, Salale na Maparoni. Naiomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ituangalie kwa jicho la pekee ili tupate magati madogo madogo sambamba na barabara zake ili kufikike kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya jambo lenye manufaa kwa wananchi waishio vijijini kwa kuunda chombo ambacho kinakwenda kutatua kero za wananchi waishio vijijini cha TARURA. Naomba sasa chombo hiki kiongezewe nguvu za kifedha na ikama ya watumishi ili wakatekeleze wajibu wao bila ya kupata kikwazo cha aina yoyote sambamba na kuongezewa vitendea kazi kama magari na maboti ya kuendea site.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali yangu sikivu ituongezee fedha katika Jimbo langu la Kibiti ili tuweze kukamilisha baadhi ya barabara zetu za lami kama kutoka Kibiti kwenda Makao Makuu ya Wilaya. Kazi imeshaanza lakini inasuasua kutokana na uhaba wa fedha.

Mheshimiwa Spika, naomba barabara za mitaa zichongwe ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa mifereji. Mfano barabara ya Kibiti Mjini, Bungu Mjini, Jaribu Mpakani Mjini, Nyamisati Mjini, barabara hizi za mitaa miundombinu yake siyo rafiki kupitika wakati wote na ukizingatia miji hii inakua kwa kasi na ina wakazi wengi sana. Barabara ya kwenda Makima ambayo ina jumla ya kilomita 32 tayari kilomita 17 zimeshachongwa bado kilomita 15. Tunaomba chombo chetu cha TARURA kipewa fedha za kutosha ili kutatua changamoto hizo.

Mheshimiwa Spika, yapo maeneo yenye mito ambayo kipindi cha mvua huwa hayapitiki kwa urahisi. Maeneo hayo ni kama Kibanga Hodi, Mkelele Mkumbwa, Kipoka, Nyafeda na Daraja la Mbwera Mjini. Naomba maeneo haya yaangaliwe kwa jicho la pekee.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Kibiti hadi leo kuna maeneo hayana mawasiliano ambapo ni jumla ya vijiji 24 kwenye maeneo ya nchi kavu. Vijiji hivyo ni Nyambunda, Nyambili, Majawa, Nyamatanga, Mchukwi A&B, Ngondae, Machepe, Nyamwimbe, Nyakinyo, Tomoni, Kingunguri, Mkenda, Kivinja A&B, Msindaji, Muyuyu, Ruaruke, Mbawa na Kilolatambwe. Kwenye visiwa (Delta – Rufiji) vijiji ambavyo havina mawasiliano ya simu ni Kiomboni, Mfisini, Salale, Mchinga, Ruma, Kiomboni, Pombwe, Jafa, Mbuchi, Mbwera Magharibi na Mbwera Mashariki, Maparoni, Kechulu, Msala, Tuwasalie na Kiasi. Upatikanaji wa mawasiliano utaongeza kipato kwa wanafamilia, kutoa taarifa kwa haraka pindi majanga yanapotokea kama ya wahalifu na mauaji ya watu wasiojulikana.