Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niunge mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, ndoto ya uchumi na viwanda haitawezekana bila kuwa na barabara, reli, mawasiliano, bandari na viwanja vya ndege na ndege zenyewe. Kwa hiyo mimi nishukuru, Mheshimiwa Waziri ujue kwamba unadhamana kubwa ya kututoa tulipo ya kutupeleka kwenye nchi ya uchumi ya viwanda, kama hutofanya vizuri kwenye Wizara hii/hamtofanya vizuri mjue kwenye hiyo ndoto ya kwenda kwenye uchumi wa viwanda itakuwa haiwezekani, kwahiyo mnatakiwa mfanye kazi kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Spika, mimi niwapongeze baadhi ya sekta ambazo zimekuwa zikifanya vizuri, lakini sitaki kuchukuwa muda mwingi kuchanganua hii kwa sababu muda niliopewa ni mdogo.

Mheshimiwa Spika, nirudi jimboni kwangu, ninapozungumza sasa hivi mvua zinanyesha, barabara zote zote zinakufa. Kwa hiyo, mimi niombe kitu kimoja kwamba kwa kuwa tunakubali na tumepitisha Sheria ya TAKUKURU wenyewe, sasa basi tuangalie uwezekano wa kutusaidia, kuna maeneo, kuna Wilaya na Mikoa ambayo ni ya kiuchumi, mikoa ambayo inachangia pato la Taifa kwenye nchi mojawapo ikiwa ni Kilolo.

Mimi nishukuru sana Mheshimiwa Rais alifika Kilolo mwaka jana, akaahidi kutujengea barabara na ninashukuru Mheshimiwa Kamwelwe tumekuwa tukiongea kila siku na umenihakikishia kwamba barabara hiyo itajengwa ya kuanzia Iringa Mjini kwenda Kilolo na bahati nzuri kwa heshima ya pekee tumeipa jina la Engineer Mfugale kama vile ambavyo Mheshimiwa Rais ametoa daraja na sisi tumempa heshima ndugu yetu Mfugale kwanza anatoka Kilolo, lakini pia huwezi kuwa daraja bila kuwa na barabara, kwa hiyo, tumempa na barabara, kwa hiyo najua itajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo na Mheshimiwa Kamwelwe pia kuna barabara tunategemea kukupa, kwa hiyo na wewe umeolea kule Iringa, kwa hiyo kwa heshima ya pekee lazima uhakikishe kwamba barabara ya Kilolo zinapatikana.

Mheshimiwa Spika, barabara za kiuchumi ni pamoja na Kongwa. Kongwa ni sehemu ambayo tumesema tutaweka maazimisho yote kule, kwa hiyo lazima ijengwe kama vile itajengwa Kilolo, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa ile ahadi ya Rais usimwangushe na barabara ambazo ni barabara ya Mkoa kutoka Iringa - Dabaga - Edete inaunganika na barabara ya kwenda Mlimba; kwa kuwa barabara ile mmeipeleka TARURA, lakini TARURA awana fedha naomba hiyo barabara muikamilishe wenyewe kwa sababu Wilaya ya Kilolo kama nilivyosema safari hii kitaifa kuchangia pato tumekuwa watu wanne na kutokana na kuchangia vizuri tumeinua Mkoa wa Iringa umekuwa Mkoa wa kwanza kuchangia pato la Taifa na Mkoa wa pili umekuwa Geita, kwa hiyo niombe msituangushe.

Mheshimiwa Spika, kuna barabara ya kuanzia Kitoo - Pomerini - Kihesa - Mgagao - Mwatasi sasa hivi haipitika, mimi nikuombe Mheshimiwa jungu kuu halikosi ukoko, toa fedha hizo za tahadhari au za emergence ziweze kwenda kuwasaidia wananchi kule wanapata taabu. Wilaya ya Kilolo ndiko ambako nguzo za barabarani za umeme zinatoka, Wilaya ya Kilolo ndiko mbao nyingi zinatoka sasa hivi zinazojenga Makao Makuu, Wilaya ya Kilolo ndiko ambako tunazalisha pareto kwa wingi, inakuwaje mnaisahau?

Mheshimiwa Spika, mimi niombe mfanye kila jitihada ili zile barabara zijengwe na niombe pia barabara ile ambayo inaunganisha kama nilivyosema mkoa kwa mkoa na iko kwenye ilani ijengwe, na nimshukuru sana Engineer wa Mkoa Bwana Kindole ni mtu ambaye anatupa ushirikiano mzuri, kwa hiyo nishukuru sana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna barabara ya Busega - Nyasuga - Ngasamo kwa ndugu yangu Chegeni, mimi naomba mumsaidie kwa sababu huyu ni mkongwe mwenzangu, tulitoka kwa ajili ya kukosa hizo barabara, sasa mmetupa matumaini tumerudi, sasa msituondoe tena kwa sababu bado tunapenda kuwatumikia Watanzania na wananchi wa majimbo yetu, ahsante. (Makofi)