Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya kuchangia. Naomba nianze kwa kueleza tatizo la kwanza kabisa la nchi hii kwamba ni matatizo yanayohusiana na sera na mipango. Tuna changamoto ya kupanga nini tunataka, tuna changamoto ya kuamua nini tutekeleze na tunapoamua kutekeleza basi ni kwa manufaa ya nani na kwa kipindi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali tuwe waangalifu sana nini tunapanga, nini tunatekeleza, kwa wakati gani na kwa maslahi ya nani. Tuangalie mipango yetu ya maendeleo na vipaumbele tuvipange kadri tunavyoweza kutekeleza. Tumekuwa na vipaumbele vingi kuliko uwezo wetu wa kutekeleza, badala yake tunakuwa na orodha ndefu sana ya miradi ambayo hatuwezi kui-fund, tunatumia mikopo kutoka nje, pesa zinaingia kwenye miradi mikubwa, hiyo miradi haikamiliki, haiondoki ilipo wala haitunufaishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri ni huu wa Bandari ya Bagamoyo ambayo watu wengi wameizungumzia, ukurasa wa 99. Ziko kazi nyingi sana ambazo zimeshafanyika pale na pesa nyingi sana za walipa kodi zimeingia pale, leo yanakuja maelezo mepesi kweli kweli yanayosema eti wameshindwa kuelewana majadiliano na wawekezaji, ukurasa wa 99, naomba ninukuu inasema:

“Mradi umeshindwa kwa sababu wawekezaji hao kuweka masharti yasiyokuwa na maslahi kwa Taifa, masharti hayo ni pamoja na wawekezaji hao kudai kuachiwa jukumu la kupanga viwango vya tozo na kutoruhusu wawekezaji wengine katika eneo la kati ya Bagamoyo na Tanga.”

Mheshimiwa Spika, haya ni mambo ambayo yangeweza kujadiliwa, haya ni maelezo ya kitoto kabisa kwamba eti tumeahirisha utekelezaji wa mradi wa Bagamoyo kwa sababu eti wawekezaji wameweka masharti, hatuna wataalam wa kujadili mambo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nishangae pia kwamba sasa Serikali inarudi kushika hatamu za huduma za kimiundombinu wakati ni kati ya eneo ambalo lingeweza kuvutia wawekezaji na ni miradi ambayo ingeweza kutekelezwa kwa mfumo kama alivyosema Mheshimiwa Turky hapa aidha wa hisa ama kupata wadau na wachangiaji wengine katika maeneo hayo ili kuboresha huduma zetu za kimiundombinu ili moja, tuweze kutanuka, lakini pili, tutoe huduma, tatu, tuweze kutoa ajira. Kwa nini Serikali sasa ndiyo mmiliki wa SGR, ndege za Serikali, Serikali ndiye sasa hivi mjenga Stiegler’s Gorge, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye danadana za ATCL. Mwaka jana nilisimama nikashauri, nikasema miaka michache ijayo of course nilitaja mitano, nafurahi kwamba hata hatufiki mitano tunakaa tena hapa leo kujadiliana namna ambavyo ATCL haisaidii nchi hii, haipigi hatua na imeshindwa kabisa ku-perform. Nilishauri kwamba tuanze kwanza na kuimarisha mtandao wa ndani wa ndege, mpaka sasa hivi hatua zilizochukuliwa ni dhaifu mno. Tunang’ang’ana kufikiria kwenda Uchina kuchukua abiria katika mipango ambayo siyo ya kudumu, si endelevu na wala haitaisaidia nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndege ambazo tumezinunua tulizinunua kwa maana ya lengo la kufufua ATCL, lakini kwa bahati mbaya hizo ndege zilipewa Wakala wa Serikali na sasa hivi tunavyozungumza kwa bahati mbaya nyingine tena, ndege hizo zimehamishiwa Ikulu. Sasa sielewi kwamba Ikulu imedhamiria kufanya biashara na bahati mbaya nyingine zaidi ni kwamba bado suala la ndege za Serikali tunazipa fedha kupitia bajeti ya Vote 62 lakini zinakwenda kuhudumiwa na Vote 20; pana kizungumkuti hapo tunaomba Waziri mhusika atatusaidia kuchambua jambo hilo ni kitu gani.

Mheshimiwa Spika, nirudi Dar es Salaam; suala la msongamano wa Dar es Salaam ni mkubwa, imekuwa shida na tabu. Sasa hivi Dar es Salaam mvua inanyesha ninyi nyote ni mashahidi, ule mji hautembei. Mradi wa mwendokasi tuliofikiria kwamba ungetupa suluhisho nao umekuwa shida, umekuwa tatizo sugu; mwendokasi hau-perform, lakini kibaya kuliko vyote kumekuwa na changamoto ya ununuzi na uuzaji wa tiketi. Scanner za pale hazifanyi kazi kwa hiyo, pesa zinatolewa na kuhifadhiwa kiholela na sijui zinakuwa reported namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine kibaya kuliko vyote, sasa hivi pale kwenye mradi wa mwendokasi hakuna chenji, ukidai chenji ya 200, 150 hupati. Kwa hiyo, kuna makusanyo mengine ya mapato yamezaliwa pale katika mradi wa mwendokasi na kuwanyang’anya wananchi na abiria wa Dar es Salaam fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la ujenzi wa gati na maegesho eneo la abiria Ferry ya Kigamboni. Mwaka 2016/ 2017 na mwaka 2017/2018 tuliizungumza, tukalipangia fedha na 2018/2019 vilevile, lakini mpaka ninavyozungumza hadi leo pale Ferry ya Kigamboni hakuna kinachoendelea, abiria wetu bado wanarundikana kama mizigo, utaratibu wa huduma kama vyoo na huduma nyingine pale bado haujakamilika, utaratibu wa utoaji magari ndani ya vivuko na kuondosha eneo la ferry na kuingia bado ni changamoto.

Mheshimiwa Spika, kibaya kingine sawa kama ilivyo kwenye mwendokasi na zile scanner za tiketi pale ferry nazo hazifanyi kazi, kwa hiyo, sasa hivi tiketi unanunua inapita bure ikiwezekana yule anayekusanya akaamua kuzirudisha tena kule zikauzwa upya, zinauzwa upya; hicho ni chanzo kingine cha wizi wa fedha za Watanzania kupitia ule mradi wa malipo ya ferry pale Kigamboni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Mwaka 2016/2017 tuliwapa jumla ya asilimia 40.3 ya fedha zote za maendeleo sawa na shilingi trilioni 11.8, mwaka 2017/2018 tumewapa asilimia 40.8, mwaka 2018/2019 tumewapa asilimia 34.8, lakini bado unaweza kuona kabisa kwamba Wizara hii haijaleta matokeo tarajiwa ukilinganisha na kiasi cha bajeti kubwa ya maendeleo tunayowapatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante ingawa nilikuwa na dakika kumi, umenipa pungufu ya hapo. (Makofi)