Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Salim Hassan Turky

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpendae

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SALIM HASSAN TURKY: Mheshimiwa Spika,ahsante sana. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu hasa kwa kufikiria vitu vikubwa na katika vitu hivyo, hivi viwili ni vya kiuchumi kabisa na leo hapa mimi na Mheshimiwa Bashe tunakaa pamoja lakini fikra zetu tofauti kabisa. Mimi nasema uchumi wetu tunatoka kwenye reli na kwenye ndege, tujipangeni; tunajipanga namna gani? Naomba sana, pesa ziko nje nje kwa kuendesha reli hii na ndege. Naomba Serikali itazame namna ya ku-float bonds katika national na international market. Tukitoa share hizi tukaziweka katika stock exchange yetu, tayari watu watanunua shares na shares hizi ndiyo pesa unazipata haraka haraka. Tena hili litakuwa na nguvu zaidi hata kesho Mheshimiwa Rais akimaliza muda wake maana yake sasa tunaingia partnership ya private na Government, tupo pamoja sasa. Kwa hivyo, hata ile management kesho itasimamiwa vizuri sana, mambo haya makubwa hayatofeli maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, naomba sana hili tulipokee kwa nguvu zote Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi. Halafu reli ni moja ambayo haina hata mshindani, Government peke yake, ni monopoly yao, hakuna mtu anayeweza akajenga reli. Kwa hivyo, hii naamini akisema kesho tu atawapata shareholders sisi wengine wote humu tutanunua shares na watu wa nje wengine watakuja watajiunga pesa nje nje, hilo tumemaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili; nashukuru sana bandari inafanya kazi vizuri sana hasa ninavyozungumza Bandari ya Dar es Salaam pale, lakini kuna kitu ambacho kinatakiwa kiboreshwe, nacho ni mizigo inayotoka Zanzibar. Baina ya Bara na Zanzibar ni biashara ya tangu mababu na mababu, japo siku hizi imepewa majina ya ajabu ajabu lakini huwezi ukaamini ukweli kwamba Zanzibar ni kisiwa cha biashara na biashara hii itadumu sisi kama tupo hata tukiondoka naamini biashara hii itaendelea.

Mheshimiwa Spika, pale Dar es Salaam sasa hivi kuna congestion kubwa sana sana ya mizigo ya Zanzibar, nashukuru kwamba tumetoa ushauri kwa bandari kulikuwa na banda lilijengwa ukuta, namshukuru sana pale Port Director tumempa ushauri na ameufanyia kazi mara moja na jana nimepigiwa simu kwamba upo ukuta wa bati pale wa kuweka magari ya godauni umeshaondoshwa na watu wanashusha mizigo yao. Hata hivyo, bado kuna ukiritimba mmoja mkubwa sana ambao unafanyika; nao ni kwamba kuna ZFA, TBS na TRA wanagongana pale, mizigo haitoki ndani ya warehouse. Naomba hili lisimamiwe kwa nguvu sana chini ya bandari yake kwa sababu hawa wote hawana ofisi isipokuwa yeye mwenye bandari ndiyo anawakaribisha mle. Kwa hivyo, wakubwa wa bandari waangalie hilo na walisimamie kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu; Mheshimiwa Rais wetu anataka nchi hii ikue kiuchumi, mimi nashangaa sana mnapokuja na mawazo ya kudumaza uchumi kwa kusema mtu mmoja awe na line moja ya simu au line mbili za simu, akitaka ya pili apate kibali; vitu hivi vya ajabu vinatoka wapi jamani? Huu uchumi leo sisi tunao mobile operators karibu watano kwa sita, kila mmoja anataka aingie sokoni; hapa kuna ajenda gani? Tunataka kumpandisha mtu mmoja, kama ilikuwa wana nia kila mtu awe na simu moja, basi hawa operators ilikuwa tuwanyime leseni hizo. Leo kila mmoja anataka soko, kwa nini anatubana tusiwe na simu? Leo mimi nataka simu ya jimboni kwangu na ya ofisini kwangu; hizi ni simu lazima kila mmoja apewe uhuru wake, huwezi ukanibania mimi ooh uwe na laini moja, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi uchumi huu unatakiwa ukue kwa kasi, huwezi ukabana hizi simu; simu nyingine mimi napokea simu za nje tu, sasa leo unaniambia aah usiwe. Hiyo nazungumza mimi kama Mbunge lakini kuna wafanyabiashara nje, wakulima na watu wote wanataka simu. Naomba hii sera ya kusema kwamba mtu mmoja laini moja, akitaka laini ya pili special pass sijui iende wapi, hiyo kitu inadumaza uchumi wa nchi hii. Naamini Rais akilisikia hili, hawezi akalikubali hata siku moja, tutakuja kuumbuliwa hapa bora tujiumbueni wenyewe, tujiwekeni sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya haya, sina la zaidi ila naipongeza sana Wizara na naunga mkono hoja na pia maendeleo yote yanatofanyika katika nchi hii nayapongeza kwa nguvu sana na naamini 2020 CCM itatisha sana. Ahsanteni sana. (Makofi)