Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Saada Salum Mkuya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Welezo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SAADA SALUM MKUYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Naunga mkono hoja na nitakwenda kwenye maeneo mawili matatu specifically.

Mheshimiwa Spika, kwanza naanza na Shirika letu la Ndege, Air Tanzania. Naipongeza sana Serikali kwa uamuzi huu ambao umekuja kuwa implemented katika awamu hii, lakini tumeanza mazungumzo muda mrefu na tumeanza mipango ya kufufua hili shirika katika awamu zilizopita. Mkurugenzi Mkuu wa shirika anafanya kazi nzuri, lakini tunaomba aangalie utaratibu mzuri zaidi wa kupunguza unnecessary delays, hususan katika safari ambayo tunafanya kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma.

Mheshimiwa Spika, ukipanda ndege mara saba, nadhani mara tano tunapata delays; na tunaambiwa mara nyingi kwamba kunakuwa kuna operational problems, lakini kunakuwa kuna delays. Kwa hiyo, hiyo kidogo inapunguza ufanisi wa shirika letu la ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiukweli ni kwamba shirika hili ni la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini toka kuanzishwa shirika hili hatujawahi kuwa na Mjumbe wa Bodi anayetoka upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maana ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, asije akaniambia napandikiza, namwambia kwamba hakujawahi kuwa na Mjumbe wa Bodi na hili ni shirika letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nataka tu anijibu kwa nini hakujawahi kuwa na huyo Mjumbe wa Bodi na kuna matatizo gani hasa? Kwa nini asikuwepo? Lini atakuwepo Mjumbe huyu wa Bodi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, tunaipongeza sana Mamlaka ya TCRA kwa kuendesha zoezi hili la usajili wa line za simu. Hoja yangu kubwa hapa ni kwamba hili ni zoezi zuri na litatusaidia kama Taifa, hususan kupunguza uhalifu kwa njia ya mitandao, lakini wakati zoezi hili linaendelea, kitambulisho kikanachotakiwa ni kitambulisho cha NIDA. Kule Zanzibar wengi tuna vitambulisho vya Mzanzibari (Zan ID), hivi kwa nini TCRA haikubali mtu asajili line yake kwa kutumia Zan ID ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetumia pesa nyingi sana kuwekeza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule Zanzibar sisi huwezi kuishi, maisha yako hayatakwenda kama huna Zan ID. Sasa tukija kwenye TCRA ambayo tunajua ni Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nini haitambui Zan ID kwa mtu ambaye hana kitambulisho cha NIDA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba atakapokuja Mheshimiwa Waziri atuambie ni kwa sababu gani TCRA haikubali mtu asajili line yake kwa kutumia kitambulisho chake cha Mzanzibari ambacho kwetu katika miamala yote, katika matukio yote, katika kila unalofanya Zan ID lazima iwepo? Kwa hiyo, naomba hilo lizingatiwe na tuje kupata majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, tunapongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kuendelea kabisa kuona kwamba inatekeleza kazi zake kwa ufanisi. Kuna maeneo kadhaa ambayo katika mwaka 2019/2020 itaendelea kutekeleza ikiwa ni pamoja na kuendelea kutekeleza mradi wa kuanzisha vituo 10 vya TEHAMA.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie hivi huu mradi wa vituo 10 vya TEHAMA, wapi na wapi utatekelezwa na tuone kwamba kwa upande wa Zanzibar vituo hivyo vitajengwa wapi au vitatekelezwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusiana na ndege zetu hizi ndogo. Mara nyingi sisi wa visiwani tunatumia sana ndege hizi ndogo, lakini tunachokiona mara nyingi ni kwamba, badala ya kuwepo marubani wawili kunakuwa kuna rubani mmoja.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2018 au mwaka 2017 wakati lilitokea tatizo kupitia ndege hii ya Coast Airline, nakumbuka Serikali ilitoa tamko kwamba, ni lazima tuhakikishe kwamba ndege zetu hizi ziwe na marubani wawili, lakini umekuwa utaratibu wa kawaida, hata kama tunapanda hizo ndege, tunatoka Dar es Salaam tunakuja Dodoma, rubani anakuwa mmoja.

Mheshimiwa Spika, sasa tunaomba Serikali i-literate yale mazungumzo yake ama tamko lake, tuone kwamba hizi ndege ndogo zinapunguza sana matokeo ambayo hatutarajii, lakini sababu isiwe kwamba kunakuwa kuna rubani mmoja. Hili jambo lipo na limezungumzwa, lakini sasa hivi naona linatoweka na halipewi msisitizo ambao unahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, otherwise nashukuru sana kwa kupata nafasi hii. Naomba sana Bodi ya Shirika la Air Tanzania tuone Zanzibar na yenyewe inakuwepo. Nashukuru. (Makofi)