Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, kimsingi, nataka tu niongee mambo matatu, kwanza, ni suala linalohusiana na Reli ya Kusini kwa maana ya Mtwara-Mbambabay. Pili, ni suala linalohusiana na masuala ya barabara ya uchumi ya Mtwara – Newala – Masasi - Nachingwea lakini tunaomba ikiwezekana iongezwe Liwale -Morogoro kwa sababu tunafahamu sasa hivi Makao Makuu ya nchi yetu yamehamishiwa Dodoma. Sisi wakazi wa Mtwara tunakwenda Dar es Salaam kufauata huduma na siyo lazima tufike pale, tungeweza moja kwa moja kutokea huko tunakokutaja tukaja hapa Dodoma straight. Kwa hiyo, tunataka na hii Serikali nayo tuishauri.

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho kabisa, nitapenda pia niihoji Serikali kwa sababu mpaka sasa kwenye Wizara hii na idara zake mbalimbali wameshatengewa na pesa zimeshatumika almost trilioni 18 lakini hatujaona kimsingi athari yake kiuchumi ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la barabara hii niliyoitaja ya Mtwara – Mnivata -Newala – Masasi. Ukisoma kwenye hotuba ya Waziri, ukurasa wa 278, kipengele cha tano, wanasema: “Ujenzi wa barabaraya Mtwara –Newala - Masasi”.

Mheshimiwa Spika, barabara hii ina jumla ya kilometa 221. Kama ambavyo Mheshimiwa Serukamba pale amesema tuangalie value for money. Barabara yenye urefu wa kilometa 221 imetengewa shilingi bilioni 3.4 tu. Kwa wastani wa sasa wa kilometa 1 ya barabara kutengenezwa kwa shilingi bilioni 1, wanatuambia kwamba katika mwaka huu wa fedha watakwenda kujenga barabara hii kwa kilometa 3 tu. Sasa tunampa mkandarasi barabara ya kilometa 221.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameikagua barabara hii akasema tunaomba hii barabara ijengwe kwa haraka sana kwa sababu ni barabara ya uchumi lakini katika hali ya kushangaza Wizara wanatenga shilingi bilioni 3.4 peke yake, wanamkwamisha sana Mheshimiwa Rais. Hawa wasaidizi wake wakati fulani wanashindwa labda kumpa ushauri unaotakiwa.

Mheshimiwa Spika, kimsingi barabara hii ni ya uchumi na ni ndefu, hauwezi kutenga shilingi bilioni 3.4 pekee kwenye barabara yenye urefu wa kilometa 221. Kwa hiyo, tuiombe Wizara ikiwezekana warekebishe fungu hili au waone namna ya kufanya ili kuweza kutekeleza ile ahadi ya Rais.

Mheshimiwa Spika, Rais alipokuja alisema barabara hii atahakikisha wanawekwa wakandarasi watatu mpaka wanne kwa urefu wa kilometa hamsini hamsini kila mmoja. Mpaka sasa barabara inayojengwa ni Mtwara -Mnivata lakini ni asilimia 36 tu ambazo zimeshatekelezwa na sasa ni mwaka wa tatu. Kwa hiyo, tunaiomba Wizara itusaidie, kero ya barabara hii ni kubwa sana na nia yetu sisi ni kusafirisha watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine hapa, suala la Reli ya Kusini. Kwa muda mrefu sana tumeongea na maeneo mengi watu wanadai fidia ikiwemo maeneo ya Mtama, Ndanda, Masasi na sehemu kubwa sana ya Jimbo la Mtwara Vijijini kwa maana ya kule anapotokea Mheshimiwa Mama Hawa Ghasia.

Mheshimiwa Spika, tatizo lililopo kwenye mradi huu, mpaka sasa haueleweki kwamba ni lini utaanza au Serikali nao wameamua kujiondoa kwenye huu mradi kama walivyofanya miradi ya barabara ya kutoka Dar es Salaam high way mpaka kufikia Chalinze. Kama ni hivyo basi waseme wazi ili wale wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika miradi mikubwa ambayo Serikali ilikuwa inaipangilia ni pamoja na mradi wa Liganga na Mchuchuma. Hakuna mwekezaji yeyote atakayekuja hapa kama hatujaboresha hii miuondombinu.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani chuma kisafirishwe kutoka Liganga kuletwa Bandari ya Mtwara kwa kutumia barabara, siyo reliable na hasara ni kubwa na hii mizigo ni mizito. Barabara hizi tuache watumie watu kama ambavyo wengine wamesema lakini hii miradi mikubwa ya kipaumbele itekelezwe tuweze kuona sasa manufaa ya chuma tulichonacho sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tuliishauri Serikali hata kwenye Kamati yetu ya Viwanda Biashara, kwa nini wasifanye uwekezaji mkubwa pale ili kuokoa forex? Pesa ambayo ingepatikana Mchuchuma ingekwenda kujenga hiyo Reli ya Kati ya Standard Gauge. Chuma ambacho kingepatikana Mchuchuma kingekwenda kusaidia kujenga kwenye reli hiyo pia lakini matokeo yake tunaagiza chuma, tuna viwanda vyetu hapa vya nondo vinaweza kutengeneza lakini bidhaa karibia asilimia 90 zinazotumika kwenye standard gauge ni imported. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huko ndiko tunakomalizia pesa zetu za kigeni na tunashindwa kufanya miradi midogo midogo hii ya kuwasaidia wananchi. Tunaona Wizara ya Maji wanalalamika lakini mpaka sasa hivi nguvu kubwa sana inapelekwa kwenye hii miradi mikubwa ambayo utekelezaji wake nao ni wenye kutia shaka kwa sababu hakujafanyika due diligence wala kuonyesha impact assessment kwenye hii miradi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli hii ni muhimu sana kwa watu wa Kusini kama ilivyo kwa watu wa upande wa Magharibi na kwingine kwenye reli hii ya standard gauge. Sasa Serikali ituambie hapa wazi, wana mpango wowote wa kufanya kazi hapa kwa sababu kwenye hivi vitabu hawaonyeshi waziwazi wanataka kwenda kufanya nini. Kwa hiyo, waje watueleze kama kuna mpango huo na kama haupo basi tuwaeleze wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi kwenye maeneo haya. Hii itakuwa ni failure kubwa sana kwa sababu hakuna mwekezaji atakayekuja kufanya kazi Liganga kama miundombinu hii wezeshi hatujaitekeleza na tunajinasibu kwamba sisi ni nchi ya viwanda na mambo mengine. Kwa hiyo, tuanze kwanza na msingi wa usafirishaji kutoka kule Liganga kuja kuleta Bandarini Mtwara ambayo ni Reli ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Reli ya Kusini ilijengwa mwaka 1949, mwaka 1963/1964 ilindolewa, kwa vyovyote vile inatakiwa pale kufanyike uwekezaji mkubwa. Ni jambo jema kujenga hii standar gauge railway lakini malengo ya Reli ya Kusini iwe ndiyo ya kipaumbele na malengo yake ni makubwa kwa sababu ni sehemu ambako tutakwenda kuongeza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, nigusie kidogo suala la barabara, tukitaja barabara inayoishia Masasi. Ukisoma pia kwenye hiki kitabu, barabara inayotokea Masasi kuelekea Nachingwea na yenyewe ina kilometa 45 wametenga shilingi bilioni 1.3 tu. Tuiombe Wizara itueleze, tunapotenga shilingi bilioni 1.3 kwenye barabara yenye urefu wa kilometa 45 tunakwenda kufanya kazi gani na pesa hizi? Pale Masasi sasa hivi kuna ajali nyingi sana kwa sababu kuna round about kubwa, barabara inayounganisha kwenda Songea, Newala, Nachingwea na kurudi Mtwara Mjini, tunaomba pale katikati ikiwezekana ziwekwe taa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo sisi tumelijadili hata kwenye vikao vyetu ya RCC na Road Board kwamba tunahitaji pale kupata taa kwa sabbau ni junction kubwa na watu wengi sana wamekufa akiwemo Afisa Mkuu wa Maji wa Wilaya yetu sisi ya Msasi, alifia pale na ajali nyingi zinatokea, tunaziona. Kwa hiyo, tunaomba pale ziwekwe taa.

Mheshimiwa Spika, hii barabara tunayoitaja inayokwenda Nachingwea pamoja na pesa ndogo mlizozitenga tuishauri sasa Serikali, tunaomba Mkoa wa Mtwara kupitia Wilaya ya Masasi ifunguliwe sasa isiishie Nachingwea peke yake iende mpaka Liwale, ikitoka Liwale iende mpaka upande wa Morogoro, Malinyi. Safari hii ni fupi sana kutoka Masasi mpaka kufika Morogoro, Malinyi siyo zaidi ya kilometa 300 lakini tunalazimika kutembea kilometa 600 kwanza kufika Dar es Salaam ili tuweze kuondoka Dar es Salaam tuje Makao Makuu ya nchi na wakati mwingine unalazimika kusafiri siku mbili mfululizo. Kwa hiyo, niombe Wizara hii wakafanye kazi kwenye barabara hii waone namna ya kuunganisha Wilaya hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine niligusia kidogo kuhusiana na uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye Wizara hii. Mpaka sasa hivi Wizara hii na Idara zake wametumia almost 18 trillion kwa maana ya kununua ndege, kutengeneza hivyo viwanja vya ndege na kufanya shughuli mbalimbali zinazohusiana na miundombinu ya hivyo vitu ninavyovisema.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sisi tulikuja hapa tukasema tunataka tuone manufaa ya moja kwa moja yanayopatikana kwa wananchi kutokana na miradi hii mikubwa inayofanywa na Wizara hii. Sasa utakapokuja Mheshimiwa Waziri tueleze ni namna gani uwekezaji huu mkubwa mlioufanya umenufaisha wakulima wa maeneo yetu wakiwemo wakulima wa korosho na wengine? Ni namna gani uwekezaji huu mkubwa uliofanywa kwenye Wizara hiyo umenufaisha uwekezaji nchini kwetu? Ni namna gani tumewavutia wawekezaji kwa kununua ndege na ni namna gani tumewavutia wawekezaji kwa kufanya huo uwekezaji mkubwa tunaoutaja hapa, Mheshimiwa Waziri uje hapa utueleze. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mtueleze ni namna gani sekta ya kilimo imenufaika na uwekezaji huu mkubwa unaofanywa. Otherwise na yenyewe tutakuwa tunasema bad timing, hatuna proper value for money. Tuiombe Serikali mwisho kabisa ikubali kufanya utafiti wa kina (impact assessment) ili kuweza kujua uwekezaji huu mkubwa uliofanyika pale umenufaisha wananchi kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa tumewekeza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mwambe.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)