Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Godfrey William Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitambue kazi nzuri ambayo anafanya Engineer Mfugale, kazi nzuri anayofanya Engineer Kindole wa pale Iringa na Ma-engineer wote wa TANROADS Tanzania nzima ninawapongeza sana kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya yote namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Manaibu wake wawili wote kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kufanya. Juu ya yote, namshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na kubwa ambayo anaendelea kuifanya kwa ajili ya mabadiliko ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kwa kuzungumzia suala la Uwanja wa Ndege wa Nduli. Uwanja huu upo Mkoani Iringa. Naipongeza sana Serikali kwamba kipindi hiki cha bajeti ya 2019/2020, tumetengewa jumla ya zaidi ya shilingi bilioni tisa kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa uwanja huu wa ndege. Uwanja huu wa ndege, kwa kweli ukifika sasa hivi pale Iringa ni burudani tupu. Tunajiandaa kwa ajili ya upanuzi na kuelekea sasa kwenye utalii katika upande wa Nyanda za Juu Kusini. Kwa hiyo, tumejipanga na tunaishukuru Serikali kwamba kazi inaonekana na tunaendelea kuipongeza Serikali kwa ajili ya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza pia juu ya takwimu ambazo zimetolewa na Kamati ambayo inahusu masuala ya SUMATRA na ajali kwa ujumla. Ni jambo la kusikitisha sana kwamba unaona ajali kwa kipindi hiki cha mwaka 2018/2019 bajeti iliyopita, unakuta inasema makosa ya kibinadamu kwenye ajali ilikuwa asilimia 76. Ubovu wa magari asilimia 16, miundombinu na mazingira ni 8%. Sasa mimi nataka nijikite kwa 8%. Tuna barabara mbalimbali ambazo zinajengwa na zimeendelea kuboreshwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza barabara inayotoka Dodoma kuelekea Iringa ambayo imekamilika miaka minne iliyopita. Barabara hii ukiiangalia katika kipindi kifupi imeharibika na haitamaniki tena. Sasa unajiuliza, ni kwa nini tunawatafuta Wakandarasi ambao sio waaminifu? Barabara ile ukipita sasa hivi ina makorongo, ina mashimo na ndiyo inayosababisha ajali kubwa katika maeneo mbalimbali hasa katika njia hii kutoka Dodoma kuelekea Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda pia kuishauri Serikali kwamba tunapotafuta Wakandarasi, basi tutafute Wakandarasi wenye viwango na tuwaadabishe Wakandarasi wote ambao wanafanya kazi bila kujali maslahi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisemi kwamba kuwe na Wakandarasi wa nje au wa ndani, lakini ninachokisema ni kwamba Wakandarasi waweze kutazamwa kwa namna ya tofauti, kwa sababu fedha nyingi zinatumika lakini matokeo yanakuwa ni mabovu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza pia suala moja kubwa sana ambalo lipo katika Mkoa wangu wa Iringa kwa barabara ambayo inatoka Iringa Mjini kuelekea Ruaha National Park, ambayo hata juzi niliongea. Barabara hii ni ya muhimu sana; na umuhimu wake ni kule kwenye mbuga za wanyama za Ruaha National Park. Mbuga hii ya Ruaha National Park, ndiyo mbuga kubwa katika nchi yetu ya Tanzania. Vilevile katika ukanda wa Afrika Mashariki ni mbuga yenye maslahi makubwa sana, ni mbuga ambayo ingetuingizia fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitakwimu Ngorongoro kwa mwaka inaingiza watalii 400,000, Serengeti 150,000, Mikumi 70,000, Ruaha National Park ambayo ndiyo mbuga kubwa ina watalii 35,000. Sasa sioni kama kuna sababu ya kuendelea kutoijenga barabara hii ya Ruaha National Park, kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park ambayo ni kilometa 104. Tumetengewa shilingi milioni 650 tu. Hili jambo lina umuhimu, litatuingizia kipato kikubwa nchi yetu ya Tanzania kama tutakuwa makini kuiangalia kwa namna nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nikumbushe kwamba kuna maeneo mbalimbali katika Jimbo langu la Kalenga ambayo hayana mawasiliano ya kutosha. Kijiji cha Lyamgungwe, Kijiji cha Kihanga, Kijiji cha Magunga, Sadani, Kikombwe, Makota, Ulata, Mwambao, Ikungwe, Kidilo, Kaning’ombe, Makombe, Malagosi, Kihanzi na Lyasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Wizara iweze kutazama kwa jicho la kipekee tuweze kupata mawasiliano ya simu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba niseme yafuatayo. Naomba ninukuu Biblia Takatifu, Luka 11:9 inasema hivi, “Nami nawaambieni ombeni nanyi mtapewa.”

MBUNGE FULANI: Kweli.

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeomba. Inasema, “tafuteni nanyi mtaona,” nimetafuta; sasa naamini nitapata. “Bisheni nanyi mtafunguliwa,” nimebisha naamini Mheshimiwa Waziri utafungua milango.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho mstari wa 10 inasema: “kwa kuwa kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa,” jamani naombeni mnifungulie. Mstari wa 11 unasema: “maana ni yupi kwenu aliye baba ambaye mwanaye akimwomba mkate atampa jiwe au samaki? Badala ya samaki atampa nyoka? Au akiomba yai, atampa ng’e.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeomba barabara inayotoka Iringa Mjini kuelekea Ruaha National Park. Haya yote naomba yaweze kunukuliwa na Mheshimiwa Waziri muweze kuyafanyia kazi, Iringa tuweze kupata barabara ya Ruaha National Park.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, Mungu awabariki, tuko pamoja sana. Ahsanteni sana. (Kicheko/ Makofi)