Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kwanza, nianze kwa kuwapongeza Waziri na Naibu Mawaziri wawili wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi uliopita niliuliza swali hapa Bungeni kuhusu barabara ya kilometa 149 inayoanzia Tabora kupitia Mambali – Bukene- Itobo na hatimaye Kagongwa. Barabara hii ndiyo barabara pekee iliyo bado kwenye hali ya changarawe inayotoka Tabora mpaka Kahama na barabara hii kwanza ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na pili, imo kwenye Ilani yetu ya uchaguzi. Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kutupatia milioni 789 ambazo zimekamilisha usanifu wa awali na mwezi uliopita Waziri alijibu swali langu kwamba mwezi wa sita ule usanifu wa kina unakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwamba Wizara ijitahidi kwamba kama ilivyoahidi (commit) kwamba ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza kabla ya 2020 wakati ambako tutaingia kwenye uchaguzi. Kwa hiyo, nina imani na Serikali yangu najua hili litafanyika lakini ni wajibu wangu kulikumbushia.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii wakati tunasubiri iweze kujengwa kwa kiwango cha lami, inapaswa iwe inapitika wakati wote. Ninaipongeza Wizara kwamba nimeangalia kwenye kitabu cha hotuba ya Waziri kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya kuhakikisha barabara hii wakati wote inapitika. Fedha hizo zipo kwenye mafungu mawili; fungu la kwanza ni fedha zinazotoka Mfuko wa Barabara na fungu la pili ni fedha zinazotoka Mfuko wa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa Mfuko wa Barabara, barabara hii imepangiwa milioni 332 na upande wa fedha zinazotoka Serikali Kuu, barabara hii pia imepangiwa milioni 330. Ni rai yangu kwa Wizara kwamba fedha hizi zilizotengwa zipatikane na zipelekwe ili barabara hii iweze kuwa inatengenezwa kila wakati na hasa yale matengenezo ya muda maalum (periodic maintenance) wakati wa mvua barabara hii huwa inaharibika vibaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fedha ambazo zimepangwa kwa ajili ya Mkoa mzima wa Tabora kama bilioni 2.4 kwa ajili ya kutengeneza kilometa 1180. Sasa hoja yangu hapo ni kwamba fedha hizi zimepelekwa kwa ujumla, zinasema tu ni za Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kutengeneza kilometa 1180 lakini Mkoa wa Tabora una Wilaya 7 na zote zina barabara hizi za changarawe. Kwa hiyo, hotuba ya Waziri haijaainisha kwamba ni kiasi gani kitatengeneza barabara zilizopo Nzega, kiasi gani Sikonge, Kaliua au Urambo. Kwa hiyo, imewekwa jumla na hatari yake ni kwamba fedha zote zinaweza zikaelekezwa Wilaya 1 au 2 halafu zingine zikakosa. Kwa hiyo, tuainishiwe kabisa hizi bilioni 2 ni kiasi gani kitakwenda kila Wilaya ili angalau tuwe tunajua ufuatiliaji utakuwaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Miaka miwili nyuma hapa niliomba minara ya simu ya Kata 4; Kata ya Kahamahalanga, Kata ya Karitu, Isagehe na Semembela lakini ni kata mbili tu ambazo zimepata hiyo minara ya simu; Kata ya semehembela na Kata ya Karitu bado hazijapata ingawa zilikuwa kwenye orodha ambayo Mheshimiwa Waziri aliitoa ya kata ambazo zitapatiwa minara ya simu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunajua kwamba sasa hivi maisha ya sasa ni mawasiliano ya simu, kwa hiyo, kunapokuwa na maeneo tunayaacha bila kuyapatia mawasiliano ya simu za mkononi kama ilivyo Semembela na Karitu, maana yake ni kwamba tunawaacha nyuma ya ulimwengu wa kisasa. Sasa hivi maisha ya kisasa kwa sehemu kubwa simu za mkononi zinachangia, ukiwa na simu za mkononi utaweza kulipa ada za watoto, ankara au madai mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunapeleka umeme vijijini, tunataka wananchi wetu wa vijijini waweze kulipia LUKU na bili za umeme huko huko wakiwa vijijini. Kwa hiyo, kuna umuhimu sana wa maeneo ambayo hayana minara ya simu yaweze kupatiwa minara ya simu. Nitumie nafasi hii kuikumbusha Wizara kwamba Kata ya Semembela na Kata ya Karitu ambayo tangu miaka miwili nyuma ipo kwenye orodha, safari hii na yenyewe kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iweze kupata mawasiliano hayo muhimu sana ya simu za mkononi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja asilimia mia moja, asante sana. (Makofi)