Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukizi na Mawasiliano. Kabla sijachangia, napenda kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametupa uzima hata kuwepo siku hii ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika nchi nyingine na hata nchi yetu ya Tanzania ni muhimu sana kwa uchumi wetu wa Tanzania. Pia nianze kwa kumpongeza na kuwashukuru sana Mawaziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu pamoja na Manaibu Katibu Wakuu wote katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwanza kwa kuzungumzia suala la barabara ambayo nimekuwa nikiizungumza humu Bungeni kwa muda mrefu, barabara ya Katumba – Lwangwa – Mbambo yenye urefu wa kilometa 83 na hii barabara ni mkombozi mkubwa sana kwa Jimbo langu la Busokelo pamoja na Majimbo jirani ikiwemo Kyela pamoja na Rungwe. Ni barabara pekee ambayo imeandikwa kwenye Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi kwa zaidi ya vitabu vitatu. Iliandikwa 2005, ikaandikwa 2010, iliandikwa 2015.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana kipekee Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivi karibuni tarehe 29 mwezi huu wa Tano alitembelea Halmashauri yetu ya Busokelo na kuahidi tena; na kuagiza Wizara kwamba sasa hii barabara itengenezwe kwa kiwango cha lami kwa kilomita zote 81.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Busokelo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na wewe Mheshimiwa Naibu Spika ulikuwepo, ulishuhudia hali ya hewa ilivyokuwa, mvua zilikuwa ni nyingi na umuhimu wa barabara hii, kwa maana wananchi wote wanategemea barabara hii kwa sababu kule tuna viwanda vya chai, tuna viwanda mbalimbali ikiwemo gesi asilia (carbondioxide) lakini tunazalisha mazao ya kila aina, kwa sababu msimu wa mvua ni zaidi ya milimita 2000 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na barabara hiyo, kuna barabara nyingine ambayo inaunganisha Jimbo langu la Busokelo na Mkoa wa Njombe kupitia Makete na barabara hii nakumbuka mwaka 2018 Mheshimiwa Naibu Waziri, Eng. Kwandikwa alikuwa amekubali kwamba ataunga juhudi za wananchi wale kulima kwa jembe la mkono, lakini kwa bahati mbaya naona hakupata fursa hiyo. Naamini alikubali ili aiweke kwenye Bajeti ya Serikali ili sasa iweze nayo kuwa katika mpango mzima wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha ajabu, bado sijaiona kwenye kitabu chetu hiki na ninaamini atakapokuja ku-wind up basi atakumbuka ile ahadi lakini na namna ambavyo wananchi wale walimwomba alivyokuja kutembelea ile barabara ya Mwakaleli mpaka kule Kandete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na suala la barabara kuna jambo zima la miundombinu hasa upande wa uwanja wa Songwe wa Kimataifa. Uwanja huu shida kubwa na changamoto kubwa iliyopo pale ni suala la taa za kuongozea ndege. Nimeona kwenye kitabu hiki wameweka shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kumalizia jengo la abiria pamoja na kuweka taa za kuongozea ndege wakati wa usiku na wakati wa mchana hasa wakati wa ukungu kipindi kama hiki, kwamba Mkoa wetu wa Mbeya mara nyingi unakuwa na shida ya ukungu muda mrefu. Kwa hiyo, ndege zinapata wakati mgumu kutua kipindi kama hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka mwaka 2018 pia mliweka kwenye bajeti haikutekelezeka, mwaka juzi iliwekwa haikutekelezeka. Naomba sana, hii shilingi bilioni 3.6 ambayo imewekwa sasa iweze kutekelezeka katika kipindi hiki. Nakumbuka mwaka huu alipokuja Mheshimiwa Rais kuzindua Kiwanda cha Maparachichi (Avocado Company) ambacho ni mkombozi mkubwa sana kwa wakulima wa Mkoa wa Mbeya pamoja na Wilaya ya Rungwe kwa ujumla, lakini maparachichi yale yanasafirishwa kwa njia ya malori mpaka Dar es Salaam ili yaweze kusafirishwa kwenda nje ya nchi. Siyo hivyo tu, yanasafirishwa mpaka Mombasa kwa sababu uwanja wetu wa Kimataifa wa Songwe hauna vigezo vya kufanya ndege za mizigo ziweze kutua pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kukamilika kwa kiwanja hiki cha Songwe kitafungua malango mengi sana ya fursa za kiuchumi kwa Mikoa ya Nyanda za juu Kusini lakini pamoja na Nchi za SADC kwa maana ya zilizo chini ya jangwa la Sahara na nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna suala zima la hizi hizi ndege ambazo sasa hivi tunapanda, wenzetu wanasema pengine hazina faida kwa sasa, lakini kawaida sekta moja inaweza ikawa na multiplier effect kwa sekta nyingine. Kwa hiyo, uchumi hauwezi kubadilika kwa sasa mara moja, pengine baada ya miaka mitano, 10, 20, 30 ndipo tutakapoona umuhimu wa hizi ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara kwamba ikifungua malango kwa kufungua njia nyingine mpya za route kutoka hapa Dodoma kwenda Mbeya pamoja na Nyanda nyingine za juu Kusini ili mtu atoke Mbeya moja kwa moja kuja Dodoma na atoke Dodoma aende Dar es Salaam na maeneo mengine, lakini sasa hivi maana yake inakulazimu uende Dar es Salaam, uende Iringa then uende Mbeya ama utoke Dodoma uende Dar es Salaam then uende Mbeya moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)