Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii kuchangia hoja hii ambayo ni muhimu sana katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri Kamwelwe na Manaibu Mawaziri, Mheshimiwa Kwandikwa na Mheshimiwa Nditiye (Mzee wa Minara), Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote pamoja na Wakurugenzi wa ATCL, TTCL, TCRA, TANROADS na wengine wote. Nawashukuru sana kwa sababu Wizara hii kazi ambazo inazofanya ni nzuri sana na nafikiri kila mtu anaziona, katika sekta zote ambazo nimezitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii imebeba Wizara nyingi sana na imefukia mashimo ya Wizara nyingi kutokana na kazi zake nzuri ambazo wanazifanya. Siyo siri kwamba miradi hii mikubwa imeipa sifa sana nchi yetu na ni miradi ambayo itabadilisha kabisa taswira ya Tanzania. Ni Wizara ambayo inatakiwa ipongezwe kwa sababu kwanza, Mawaziri na viongozi wake sasa hivi wanafanya kazi kubwa sana. Mawaziri hawa wametembea nchi nzima na wameona miradi ambayo iko kwenye mikoa yetu na wamejitahidi kwa kadri ya uwezo kutatua changamoto zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuzungumzia Jimboni hasahasa barabara yangu ya Amani - Muheza kilomita 36. Barabara hii imekuwa inatengewa fedha tangu mwaka juzi, shilingi bilioni 3, mwaka jana shilingi bilioni 5, mwaka huu karibu shilingi bilioni 2 lakini tatizo ambalo lipo ni la mkandarasi kutopatikana. Najua Meneja wa TANROADS Mr. Ndumbaro anafanya juu chini lakini kila ukimuuliza anakwambia hapana, bado kidogo, kuna mchakato wa mzabuni. Zabuni hii imetangazwa mara tatu, mara ya kwanza mkandarasi hakupatikana, mara ya pili mkandarasi hakupatikana na hii mara ya tatu ndiyo naambiwa sijui kama atapatikana na naambiwa mambo yote yako kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ndiyo uchumi wa Muheza. Muheza tunategemea barabara hii iwe kwenye kiwango cha lami ili iweze kuteremsha mazao kutoka Amani kwenda Mjini Muheza mpaka Dar es Salaam kwa ajili ya mauzo. Kwa hiyo, naomba uitolee maamuzi ili kabla mwaka huu wa fedha kuisha basi mkandarasi awe site. Nakumbuka Mheshimiwa Waziri nilikuona na nikakuomba kwamba fedha ambazo zimewekwa mwaka huu ni kidogo na ujaribu kuangalia namna ya kuweza kuziongeza. Nakushukuru sana kwa kupokea ombi hilo ambalo naamini utalishughilikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na matatizo haya ya barabara ya Amani pia tuna matatizo ambayo tumeomba katika miaka hii miwili, mitatu iliyopita, kufanyiwa upembuzi yakinifu katikati ya barabara ya Pangani, junction ya Boza mpaka Muheza (kilomita 42) pamoja na Muheza – Maramba (kilomita 45) kwa matayarisho ya kuwekewa lami. Sikuona kwenye kitabu lakini naomba uangalie uwezekano ili ziweze kufanyiwa upembuzi yakinifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni mawasiliano. Nimewasiliana sana na Mheshimiwa Nditiye, Naibu Waziri anayeshughulika na mawasiliano, kwa sababu mpaka wakati huu kiwango hiki tulichokifikia kuwa na sehemu ambazo hakuna mawasiliano ni tatizo kubwa sana. Tarafa ya Amani mawasiliano ni tabu sana, ukiangalia Kata zote za Amani yenyewe, Mbomole, Zirai, Kwezitu, Misarai, Magoroto pamoja na sehemu za Kwebada mawasiliano ni mabovu sana. Jana tu nilikuwa naongea na wewe Mheshimiwa Naibu Waziri na ukanihakikishia kwamba utashughulikia. Napenda niliongelee hilo ulishughulikie ili na wananchi wa maeneo ya Amani waweze kusikia kwamba kweli suala hilo linashughulikiwa na mawasiliano hivi karibuni yatakuwa ni mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la SGR, nimeona hapa kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kwamba mpango wa kuweka SGR kutoka Reli ya Tanga - Dar es Salaam - Arusha – Msoma upembuzi yakinifu ulishafanyika na sasa hivi mikakati inafanyika ya kumtafuta mkandarasi kwa njia ya PPP ili na sisi reli ya Tanga tuweze kuwa na SGR. Suala hili ni la muhimu sana kwa sababu suala la PPP marekebisho yake tulishayafanya kipindi kilichopita na tunategemea kwamba suala hili lingeanza sasa hivi kutangazwa kwa sababu upembuzi yakinifu umeshafanyika ili tuweze kupata SGR Tanga line. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwamba Bandari ya Tanga inaendelea kufanyiwa ukarabati. Kwa hiyo, suala hilo ni muhimu sana liendelee na liweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la ndege kwenda Tanga - Pemba, tulisikia kwamba sasa hivi bombardier itatua Tanga na itakwenda Pemba na kurudi Dar es Salaam. Mpango huo mpaka sasa hivi naona kimya, ningeshukuru sana kama Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa ku-wind up, basi utuambie kwamba na sisi Mkoa wa Tanga hii ndege ya bombardier itaweza kutua kwenye uwanja wetu kwa sababu sasa hivi kiuchumi tunakwenda kwa kasi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo nataka kuongelea ni suala la express way, hili suala ni la msingi sana. Kila mwaka naongelea kwa nini hatuanzishi road toll kwenye barabara zetu. Ulimwengu mzima sasa hivi unakwenda na road toll, hakuna nchi ambayo utakwenda usikute imefungwa inatengenezewa road toll au kuna watu ambao wanalipa road toll. Hii ni njia mojawapo ya kuinua uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tulikuwa Kampala, tumeteremka Entebbe pale, Entebbe mpaka Mjini Kampala kuna express way wameshatengeneza wenzetu, mtu anachagua apite kwenye express way au aende kwenye barabara ya kawaida. Hivi vitu ni vya msingi na ni muhimu sana sijui kwa nini hii barabara ya Chalinze tusianzishe express way? Kama atapatikana mtu ambaye ana uwezo wa kutengeneza, akaweka road toll yake, kwa nini tunakataa vitu kama hivi? Nashauri sasa hivi tuangalia umuhimu wa kuanzisha road toll, express ways ni muhimu sana kwa maendeleo ya miji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la SGR ambalo mwenzangu Mheshimiwa Silinde hapa amelizungumzia lakini tunajua kwamba hawa watu wetu wenye viwanda vya vyuma, kweli hivi vyuma vilikuwa vinatoka nje lakini wewe mwenyewe Mheshimiwa Silinde utakubali kwamba wamekuja tangu juzi kwenye Budget Committee na wamekiri wameanza kupewa kazi hizo za kuweza ku-supply vyuma kwenye reli hii ya SGR. Hayo ni mafanikio kwamba sasa hivi wameanza na unajua kabisa kwamba Kamati ya Bajeti sasa hivi inashughulikia namna ya kufufua Mchuchuma-Liganga na jana tulikuwa na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)