Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi asubuhi hii nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda niishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Wizara hii imeweza kufanya mambo makubwa katika Sekta zote hizi za Uchukuzi, Mawasiliano na Ujenzi, hasa katika ununuzi wa ndege, upanuzi wa viwanja vya ndege, ujenzi wa reli ya kisasa na mengineyo. Kwa ujumla naomba niwashukuru na niwapongeze viongozi wote wa Wizara kuanzia Waziri na Watendaji wake ambao siyo rahisi kuwataja mmoja mmoja, lakini kwa umoja wao wameweza kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na suala la barabara ya Tabora mpaka Mpanda. Naiongelea hii barabara kwa sababu imeanza kusemwa toka mwaka 2005 mpaka leo hii. Nami nafahamu kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi, alishaiombea fedha kupitia Benki ya Afrika. Sasa sielewi kunasuasua nini? Kwa sababu ukiangalia kila kipande kipande kina viasilimia; kuna asilimia 12 Kasinde - Mpanda, kuna asilimia 18; Urila kuna asilimia 15.9.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizi asilimia hatujui tunazipimaje na hatuelewi hii barabara pamoja na kwamba ilishapata fedha, itakwisha lini ili iweze kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Katavi, Tabora, Rukwa, Mbeya na wote watakaopita ile njia pamoja na wananchi wangu wa Jimbo la Katavi, Jimbo la Kavuu, (samahani Jimbo la Katavi ni la Mheshimiwa Waziri), Jimbo la Kavuu na Wajimbo la Katavi wenyewe kupitia Inyonga ili waweze kupita kwenda mpaka Mwanza, mpaka Kahama waweze kufanya biashara zao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naomba niongelee suala la Mfuko wa USCAF. Napenda niwashukuru mfuko huu wameweza kufanya kazi kwa uwazi na kwa namna ambavyo wananchi wameweza kuuelewa sasa, kwa sababu mwanzo walikuwa hawauelewi lakini leo wananchi wanaelewa chini ya Eng. Ulanga na wengineo wote wanaofanya nao kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kawaida yangu ndani ya Jimbo la Kavuu, lazima niombe masuala yote yanayohusu maendeleo. Kupitia Mfuko huu wa USCAF naomba Kata nzima ya Maji Moto na vitongoji vyake na vijiji vyake iweze kupata mawasiliano ya uhakika. Naomba Kijiji cha Mawiti, Kabunde, Mainda, Lunguya, Ikupa, Luchima, Kanindi, Minyoso, Kwamsisi, kote naomba niweze kupata mawasiliano. Ni vijiji ambavyo havina mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Watendaji wako hapa na Mheshimiwa unapafahamu huko kote, naomba wananchi hawa wapate mawasiliano ili tueweze na sisi kwenda kisasa, tuweze kufanya biashara za kupitia mitandao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudi kwenye suala la Shirika la Reli. kwenye suala la Shirika la Reli, mimi toka nimeingia humu nimekuwa nikiongelea Shirika la Reli hasa kwa usafiri wa kutoka Mpanda – Tabora, Tabora – Dodoma, mpaka Dar es Salaam. Jamani, kuna kipindi alikuwa Mheshimiwa Waziri Mwakyembe, nikamwambia kule siyo mabehewa ya kukaa binadamu. Nilishaongea mwaka 2017 kwamba basi waangalie namna bora ya kubadilisha hata mabehewa, wananchi wale waweze kuingia kwenye mabehewa safi na salama. Mabehewa yale ni machafu, yemechoka. Kwa nini yaletwe Mpanda? Kama yamechoka, yakawekwe Morogoro, mtuletee mabehewa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongee kuhusu mpango wa anuani za makazi wa Post Card; mpango huu ni mzuri sana. Tumetenga fedha nyingi sana. Nawaomba Watendaji tufanye vizuri. Leo ukitoka hapo nje ukienda Chuo cha CBE, ile tuliyoweka pale imeshang’oka. Sasa tuweke imara zaidi. Ni mpango mzuri unaoweza kutambulisha nchi yetu vizuri na ni kwa utaratibu wa maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niwaombe, hebu tuongeze ile value for money katika huu mradi kwa sababu hauna impact, hata ukitembea hapa kwenda hapo stand Kimbinyiko. Bado haijakaa vizuri. Kwa hiyo, naomba sana tuboreshe hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudi katika barabara ya Kibaoni – Maji Moto – Inyonga, bado inafanyiwa upembuzi yakinifu na nini. Naomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu. Hii pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kutoka Maji Moto mpaka Inyonga kwa kiwango cha lami, lakini pia kutoka Kibaoni; siyo Kibaoni tu mpaka Inyonga, mpaka Kansansa, Klyamatundu.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua tumejenga daraja la Momba, Serikali yangu imefanya vizuri, nashukuru tunaipongeza, lakini hii barabara pia lazima tuifungue ili wananchi hawa wa Jimbo langu la Kavuu waweze kutoka Kansansa ama Maji Moto, ama Kibaoni mpaka waweze kufika Mbeya, Mbeya waweze kwenda Kalambo, Kalambo waweze kwenda Kasesha, Kasesha waweze kwenda Mpulungu, waingie Zambia, waingie Mozambique waweze kufanya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku naliongea hili. Lazima tuangalie sasa ni namna gani tutatanua wigo wa kutoka Tunduma na wa kutoka Kalambo ili tuingie mpaka Mozambique. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudi niongelee sasa daraja langu la Msadya. Daraja hili naomba Waziri anisikilize vizuri, nimekwishapeleka maombi, najua linahudumiwa na Ofisi ya TAMISEMI kupitia TARURA, lakini TARURA hawa ni Wizara hii ndiyo wanawapatia pesa. Leo ni mwaka wa tatu wananchi wangu wa Kata ya Mbebe, Mwamapuli, Chamalendi mpaka wanaotoka Kibaoni hawawezi kufika Usevya ambako kuna kituo cha afya nilichosimamia mwenyewe na Mkurugenzi wangu cha mfano! Pia Mheshimiwa Ummy alishafika pale akakiangalia, ni cha mfano, niwaombe sana wanitengee pesa kwa ajili ya hili daraja ili wananchi wangu waweze kupata huduma pale. Hawapati huduma mpaka sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la barabara ya Mpanda mpaka Kahama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga. Ahsante sana.

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na naomba yote haya niliyoyaeleza yachukuliwe kwa umuhimu wake. Ahsante. (Makofi)