Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo inatekeleza miradi yake ya kimkakati. Nchi zote duniani zilizofanikiwa kiuchumi ni pamoja na kuwekeza katika miundombinu ya reli, baharini kwa maana ya meli pamoja na anga. Hizo nchi zimefanikiwa sana kiuchumi duniani. Jambo hili limefanywa na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na barabara ya Magu – Bukwimba – Ngudu na Hungumalwa. Barabara hii imeelezwa asubuhi na kaka yangu, Mheshimiwa Ndassa hapa, ni barabara ambayo iko kwenye ilani, lakini inafungua uchumi kwa sababu inaunganisha barabara kuu mbili; barabara ya kutoka Mwanza – Shinyanga na barabara kutoka Mwanza – Musoma – Nairobi, kwa hiyo, barabara hii ni muhimu sana kiuchumi. Ni vizuri Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, Waziri, tunajua ni mchapakazi pamoja na Manaibu pamoja na mzee wa TANROADS, Engineer Mfugale. Mfugale kwetu maana yake huwezi kufa haraka, kwa hiyo, ndiyo maana Eng. Mfugale upo hapo, Rais alikuteua, tuone barabara hii unaiweka kwa sababu huwezi kufa haraka kwa maana ya Kisukuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo barabara ya Magu – Mahaha – Itubukilo – Bariadi, inaunganisha Mkoa wa Mwanza na Mkoa wa Simiyu. Pale katikati Itubukilo na Mahaha tunahitaji daraja. Ni vizuri sasa Mheshimiwa Waziri uone, hili nimekuwa nikiomba kila ninapochangia kila mwaka. Naomba sasa kwenye bajeti hii sasa tusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye Daraja la Sukuma, daraja mmeshatangaza na mkandarasi ameshapatikana, tatizo kibali tu Daraja la Sukuma lianze kutengenezwa. Hii nadhani ni ile Sheia ya Msamaha wa VAT, inachelewesha sana kwa sababu documents za nchi nzima zinakwenda Wizarani kurundikana, inachukua muda mrefu sana kibali kwa ajili ya ujenzi kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hizi ambazo tunaziweka Waheshimiwa Wabunge, mimi nishauri tu zile ambazo zinakwamisha kufanya miradi yetu kwenda haraka ni vizuri zikaletwa tukazirekebisha. Kwa sababu hizi sheria zinataka mpaka miradi hii itangazwe kwenye GN na inachukua muda mrefu sana kutangazwa kwa sababu ni miradi ya nchi nzima. Hata linapotokea dharura mhusika hawezi kutangaza kazi iweze kutekelezwa, anachukua muda mrefu kwa sababu ya sheria ambazo tumeziweka, ni vizuri tukazirekebisha sheria hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Mwanangwa – Misasi – Kahama, usanifu tayari umeshafanyika, ni vizuri sasa zikatengwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Pia tunayo barabara muhimu sana ya Nyakato – Igombe TX na barabara ya lami ambayo inatokea airport kuja Nyanguge - Kayenze, hizi ni za ring roads ambazo zinafungua Mji wa Mwanza kuondokana na misongamano ambao upo. Mheshimiwa Eng. Kamwelwe nakuangalia hapo huandiki, andika ili niweze kuona kweli uko serious na jambo hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa kweli unaendelea kubaki nyuma. Nimeona mmetenga fedha, ni vizuri sasa utekelezaji wake ukaanza, hasa jengo la abiria ili kuweza kuchukua abiria wengi kama ilivyotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye hilihili, Mheshimiwa Eng. Kamwelwe na mnaohusika na ndege, hebu wekeni ndege ya kutoka Dodoma - Mwanza, Mwanza – Dodoma, kuna Mikoa mitano ya Shinyanga, Geita, Mara, Simiyu, Mwanza yenyewe, watumishi tu wa Serikali wanaokuja Dodoma kila siku ni wengi sana, wanatumia magari, ni risky. Nawahakikishia mkiweka route hii mtapata abiria wengi sana, hata mara mbili tu kwa wiki. Tusaidie Mheshimiwa Eng. Kamwelwe, hili tumeshakwambia na tumeshalizungumza mara nyingi na Mheshimiwa Ndassa amezungumza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe barabara tatu ambazo zipo kwenye Wilaya yetu ya Magu; barabara ya Kisamba – Sayaka – Salama – Bariadi inaunganisha Mkoa wa Simiyu, Wizara ichukue barabara hizi. Mheshimiwa Eng. Kamwelwe ulipoanza kazi kwenye Wizara hii nilikuomba tutembelee pale, nikuombe tena, kama utamaliza bajeti yako wakati wowote twende tuione barabara ya Kisamba – Sayaka – Salama – Bariadi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo barabara ya Kabila – Isawida ambayo inatoka kwa Mheshimiwa Ndassa, Maligisu na Kabila tuna junction sasa ya kwenda Isawida ambako ni Wilaya ya Itilima, Mkoa wa Simiyu. Hizi ni barabara muhimu sana za kutufungua kiuchumi katika mikoa hii miwili. Niombe Wizara izitilie maanani barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la mawasiliano, Naibu Waziri nimekueleza na nimekuandikia maeneo ambayo Wilaya ya Magu inapata taabu kwa mawasiliano katika Vijiji vya Mwamabanza, Salong’we, Sayaka, Ndagalu, Nobola, Mahaha, Kigangama pamoja na Bundiria. Hebu tusaidie minara hii angalau wananchi waweze kupata mawasiliano na kuingia kwenye uchumi kirahisi zaidi kwa sababu mawasiliano ya simu yanarahisisha ukuaji wa uchumi kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara ya kutoka Nyanguge kwenda border kwa maana ya Musoma, kule Musoma imetengenezwa mpaka Lamadi lakini kipande hiki cha kilometa 80 kutoka Nyanguge mpaka Lamadi ni barabara kama uko kwenye bumps, unaijua vizuri. Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, hebu fanyeni utaratibu wa kuijenga upya barabara hii ili iweze kukamilishwa kama ambavyo Musoma mmeshakamilisha. Nikuombe sana jambo hili ni muhimu, pamoja na Daraja lenyewe la Simiyu, naamini upembuzi yakinifu umeshakamilika. Tunapata adha sana hasa wakati wa masika hakuna mahali popote pa kuweza kupita Mto Simiyu ukiwa umefurika. Hebu daraja hili lijengwe ili angalau watu wa Musoma na Mwanza wasipate adha yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)