Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ni muhimu sana ukitoka Wizara ya Elimu. Hii ni Wizara yenye kushikilia maisha ya Watanzania. Bila kuimarisha Wizara hii, hakuna Serikali ya Viwanda wala Tanzania ya Viwanda kwani afya ni kila kitu. Watanzania wakiwa na afya bora ndiyo shughuli za kiuchumi zitakuwa na maendeleo, kwani mwenye kuleta maendeleo ni wananchi wenye afya bora na nguvu kazi ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nitoe maoni yangu katika Wizara hii. Kwanza ni upungufu wa rasilimali watu katika Wizara hii ya Afya. Sekta hii ina upungufu mkubwa wa rasilimali watu. Sekta hii ina upungufu wa watumishi kwa asilimia 49 katika mwaka wa fedha 2016/2017. Tunaomba Serikali itoe hitaji la watumishi wa sekta hii ya afya ili wananchi wapate matibabu kwa wakati na kwa ubora wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Mheshimiwa Waziri aone kilio cha Watanzania juu ya hitaji hili muhimu. Imekuwa na usumbufu kwa wananchi wanapohitaji matibabu wanachukua muda mrefu hospitalini, mtu anakwenda saa 12.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni ndiyo anapata matibabu kutokana na uhaba wa wahudumu. Mhudumu ana daktari mmoja, huyo anahitajika zaidi ya vitengo vitatu kwa wakati mmoja. Hii ni shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ituambie ni lini itatatua tatizo hili la upungufu wa watumishi katika sekta hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitazungumzia hali ya maambukizi ya VVU na UKIMWI nchini Tanzania. Hali hii inaendelea kukua kwa kasi zaidi kinyume na hali iliyotarajiwa. Dhana nzima ya 90 – 90 – 90 iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kuhusu HIV/AIDS mwaka 2013 kwamba ili kufikia mwaka 2020 kusiwepo na maambukizi ya UKIMWI Duniani. Kwa maana, kutambulika, waliotambulika wako kwenye matibabu ya ARV na wenye matumizi ya ARV, virusi vitakuwa vimefubaa na hakutakuwa na maambukizi mapya. Hii ndiyo azma ya 90 – 90 – 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Tanzania, hatujafikia hatua hii, ni hatari sana na ndiyo kwanza maambukizi yanazidi. Kwa mfano, vijana kati ya miaka 15 - 49 ndiyo rika hatari zaidi na wenye kuleta maambukizi zaidi. Hawa ni vijana ambao wako shuleni na vyuoni kwa asilimia 46. Je, Tanzania tumefikia wapi katika kufikia lengo la 90 – 90 – 90 na tukizingatia umebaki mwaka mmoja na nusu kufikia muda uliowekwa na Umoja wa Mataifa? Serikali itufahamishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali na Sekta hii itoe elimu kuhusu HIV/UKIMWI na isione haya kueleza vitu vinavyosababisha maambukizi, bila kificho. Kama Serikali haitaacha kupiga marufuku condom UKIMWI utaendelea kuwepo, kwani hivi ni vichochezi vya zinaa. Vitabu vya dini vinasema tusikaribie zinaa, zikishamiri maradhi yatazidi ama majanga na hili ni janga na siyo maradhi kwani kila maradhi huwa yana tiba ila UKIMWI hauna tiba. Ili UKIMWI uondoke, tuache zinaa tutake tusitake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii inatisha sana hasa tukizingatia maambukizi kwa vijana hawa wadogo. Hii ina maana nguvukazi ya Taifa hii inapungua na kufa pia kwa kasi sana na tusipochukua tahadhari tatizo hili ni zito na kubwa sana, huenda miaka ya mbele tutakosa kabisa vijana wenye afya bora wa kujenga Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia maambukizi mapya na kuweka sheria, kama ni kosa la jinai kufanya zinaa au vitendo hivi bila ya kuwa na ndoa. Kinyume na hayo tutatenga pesa ama fedha nyingi za kutibu na maambukizi yataongezeka na mwisho tutakosa nguvukazi za Taifa na hivyo Tanzania ya Viwanda itabaki kuwa ndoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.