Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama katika Bunge hili Tukufu na kuchangia machache kwa maandishi, hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Pia, nachukua nafasi hii kumpa pongezi Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wataalam wa Wizara nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya mambo mengi mazuri, hasa kuhusu mambo ya afya ikiwepo ujenzi wa vituo vya afya na upatikanaji wa dawa. Natoa shukrani kwa Hospitali yetu ya Mkoa/Rufaa Morogoro kwa kutupatia X-ray ya kidigitali, tunashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa Hospitali ya Rufaa Morogoro, tunaleta ombi letu kuhusu kupewa mashine ya CT-Scan ambayo ni muhimu sana. Hii ni kukumbushia ahadi ambayo ilitolewa hapo awali na viongozi wetu wa taifa wakati wa ziara Morogoro. Nashukuru kwa yote mazuri yaliyotendeka kwa kutupatia gari la wagonjwa na X- ray, kwa imani hii naamini hata CT-Scan tutapewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri na naomba Hospitali za Wilaya za Mkoa wetu za Gairo, Ifakara, Morogoro Vijijini na Mjini ziendelee kupewa fedha na kujengwa na kukamilika. Mheshimiwa Waziri nasema haya kwa sababu Hospitali ya Mkoa inazidiwa na wagonjwa (mrundikano wa wagonjwa) kwani Wilaya za Mkoa hazina hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Mikumi, majengo ni mazuri na hivi karibuni kitaanza kutumika. Mpaka sasa ameletwa daktari mmoja, naomba na kushauri waletwe wataalam wengine zaidi kusudi wananchi wapate matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo nililoliona katika kituo hiki ni ukosefu wa jengo la mortuary. Ujenzi mzima unaendelea kukamilika ila hakuna mpango wa mortuary. Naiomba Serikali yangu ifikirie jambo hili kwani Mikumi, hususan Wilaya ya Kilosa, kuna watu wengi na hivyo hata jengo hili ni muhimu ingawaje watu hatutaki kusikia kifo.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kwa vituo vya afya vinavyoendelea kujengwa. Nashauri mpango huu uendelee kuvifikia vituo vya afya ambavyo wananchi wamejenga na kuachia ngazi ya maboma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa Vituo vya Afya Dutumi na kumalizia majengo yaliyokaa muda mrefu, hilo ni ombi letu wananchi wa Morogoro Vijijini. Katika ziara zangu Zahanati ya Hembeti ambayo inatumika pia kama Kituo cha Afya kwenye Kata ya Hembeti, Wilaya ya Mvomero, majengo yake yamechakaa sana tena sana. Naiomba Serikali zahanati/kituo cha afya hiki kikarabatiwe. Pia, hakuna wataalam wa kutosha kuanzia madaktari hadi manesi. Kituo hiki nashauri kiangaliwe vizuri ili kizidi kutoa huduma nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina tatizo la utapiamlo na hasa udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano. Tatizo kubwa ninaloliona ni elimu kwa wananchi. Nashauri elimu ya lishe ya mkakati na ya vitendo itolewe zaidi. Wananchi wakipata elimu ya kutosha kuhusu mambo ya lishe hasa kwa akina mama wajawazito na akina mama wanaonyonyesha utapiamlo utapungua au utakwisha kabisa hapa nchini Tanzania kwani kwa ujumla vyakula vya kutosha tunavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vituo vya maendeleo ya jamii. Naomba na kushauri ukarabati wa vituo hivi. Ni kweli wataalam wa maendeleo ya jamii wanatakiwa sana na muhimu kwa kusukuma maendeleo ya jamii yetu hapa nchini. Watumishi hawa ni muhimu sana kwa kusukuma maendeleo. Nashauri kila kijiji kiweze kupata Afisa Maendeleo ya Jamii ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ndoa. Na mimi naungana na Wabunge wenzangu kusema kuwa kutokana na hali na maendeleo tuliyonayo sheria hii ni ya muda mrefu na imepitwa na wakati. Nashauri iletwe humu Bungeni ili ibadilishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ugonjwa wa malaria udhibiti wake uangaliwe kwa undani.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuchangia hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.