Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli pamoja na wanaomsaidia kazi, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu yuko hapa ambaye kila wakati tunamweleza matatizo ya maeneo yetu na Mawaziri wote wanaotusaidia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimshukuru Waziri, Mheshimiwa Ummy pamoja na Naibu Waziri wake na Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI kwa maboresho waliyofanya ndani ya sekta ya afya. Wanafanya kazi nzuri nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na Jimbo langu la Makambako, nilipewa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Lyamkena, shughuli ya ujenzi imeshakamilika tangu Desemba, 2018. Tunaomba sasa tupatiwe vifaa tiba na waganga ili kituo kile kiweze kuanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, tunaomba kituo mama ambacho kilikuwa kama ni hospitali ya mji wa Makambako ambacho ni Kituo cha Afya cha Makambako ambacho kinafanya kazi nzuri lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa X-ray na Utra Sound. Mheshimiwa Rais alivyokuja tulimueleza matatizo yetu na nashukuru aliwaagiza watendaji ikiwemo Wizara ya Afya na TAMISEMI na bahati nzuri nilipokutana na Waziri wa Afya ambaye ni Mheshimiwa Ummy Mwalimu nilikueleza juu ya jambo hili na uliniahidi kwamba utanipa X-ray. Nakushukuru kwa dhati kabisa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Makambako. Vilevile niombe sasa atakapotupa X-ray usisahau muwasiliane na wenzako wa TAMISEMI angalau tupate Utra Sound ili vifaa tiba hivi viweze kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaiomba Serikali angalau tupate fedha za kujenga wodi ya akina baba. Mlitupa fedha za kujengea wodi ya akina mama na watoto imeshakamilika na inafanya kazi katika Kituo hiki cha Afya Makambako bado wodi ya akina baba.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tupate wodi ya akina baba kwa sababu jengo lililopo ambalo lilijengwa kwa ajili ya kuweka vifaa tiba vya X-ray na Utra Sound ndiyo vyumba kadhaa vimegawiwa vinafanya kazi kama wodi. Kwa hiyo, tunaomba tupate fedha kwa ajili ya kujenga wodi ya akina baba.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali kwa kutupa fedha za kujenga hospitali ya halmashauri yetu shilingi bilioni moja na milioni mia tano. Kwa dhati nakushukuru sana kwamba sasa tunakwenda kupata ukombozi wa tiba kwa wananchi wetu wa Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna zahanati nyingi ambazo tumezijenga katika halmashauri yetu. Halmashauri yetu kwa kushirikiana na wananchi, mimi Mbunge, Waheshimiwa Madiwani na wadau wengine zimejengwa zahanati zaidi ya 13. Tulitegemea katika bajeti hii ambayo tunaendelea nayo angalau tungepata fedha kiasi ili zahanati kadha kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 ziweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefikia mahali pazuri, zimeshapigwa lipu na kadhalika. Zimeshakamilika vimebaki vitu vidogo tu. Tumeshaanza kujenga nyumba za waganga katika zahanati hizo. Naomba Serikali ione umuhimu wa kutupatia fedha mwaka huu wa 2019/2020 ili baadhi ya zahanati hizi ziweze kukamilika. Hata hivyo, naishukuru Serikali kwa kuongeza fedha kwa ajili ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nimwombe Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Kituo cha Afya mama cha Makambako kipo katika center kubwa ya Makambako, kwenda Njombe, Mbeya, Iringa na sehemu nyingine, mtuongezee dawa kwa sababu tunapata kwa kiwango kidogo sana wakati kituo hiki kilikuwa kama hospitali kabla ya kutupa fedha za kujenga hospitali. Nikuombe sana uone namna ya kutuongezea dawa ili kukidhi kuwahudumia wananchi wa Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)