Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya na uzima na hatimaye nimeweza kusimama na kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa pongezi nyingi kwa Wizara ya Afya, kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wao wote katika Wizara ya Afya. Kazi mnayoifanya ni kubwa na hakika mmeleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Afya. Hongereni sana. Mwenye macho haambiwi tazama, yanaonekana yale yote ambayo mmeyafanya katika Sekta ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza pia kwa uboreshwaji wa huduma katika hospitali zetu maalum; Hospitali ya Ocean Road, Hospitali ya Jakaya Mrisho Kikwete ya kitengo cha Moyo na hospitali zote za mikoa, Wilaya na uboreshwaji wa vituo vya afya. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda ni mfupi, niende moja kwa moja katika Mkoa wangu wa Shinyanga ili niwasemee wananchi walionileta ndani ya ukumbi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuisemea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Mwaka 2018 nilisimama humu ndani nikasema kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Ujenzi huu umeanza bajeti ya mwaka 2013/2014; kuna jengo moja kubwa ambalo limekamilika, jengo la utawala. Jengo hili wanaishi popo, halina kazi yoyote. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, tarehe 24/01/2019 alitembelea ujenzi wa hospitali hii katika Mkoa wa Shinyanga na baada ya kutembelea alitoa ahadi kwamba atatoa fedha, shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya maternity block ili hospitali ile ianze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namkumbusha Mheshimiwa Waziri wa Afya, ahadi yake Wana-Shinyanga tunaisubiri kwa sababu ulisema jengo lile litakamilika na mwishoni mwa mwaka huu hospitali ile itaanza kufanya kazi, sijui umekwamishwa na kitu gani? Nakuomba sana, nakusihi sana, ahadi ni deni. Vitabu vya dini vinasema, ukiahidi halafu bahati mbaya Mwenyezi Mungu ikatokea lolote, umekufa deni. Naomba ahadi hii uitekeleze Wana-Shinyanga tunaisubiri kwa hamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa bajeti mwaka 2018 nilisimama nikasema ubovu wa X-Ray machine katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. Namshukuru Mheshimiwa Waziri pia alipokuja Shinyanga alituahidi wana Shinyanga kwamba atatuletea X-Ray machine ya kisasa, lakini mpaka sasa hivi hatujapata X-Ray machine ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado namkumbusha Mheshimiwa Waziri, aliahidi mwenyewe na Wana-Shinyanga tunasubiri na watendaji wake wanamsikia. Ahadi ni deni, tunasubiri X-Ray machine ya kisasa kwa sababu tuliyonayo ni mbovu na haifanyi kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niendelee kukumbusha ahadi za Serikali. Wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Mkoa wa Shinyanga, nilisimama katika Jimbo la Ushetu nikaomba ambulance kwa ajili ya Jimbo la Ushetu. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokea ombi hilo na akatuahidi kwa Mkoa wa Shinyanga kutuletea ambulance nne na Mheshimiwa Waziri mwenyewe akiwepo. Tunahitaji Ambulance kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Tinde, kwa ajili ya Jimbo la Ushetu, Jimbo la Msalala na Jimbo la Kishapu. Ahadi hizo hazijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusemea kuhusu watumishi katika Mkoa wa Shinyanga. Watumishi wa Idara ya Afya katika Mkoa wa Shinyanga mahitaji ni 3,606, waliopo ni 1,446 na upungufu ni 2,160. Naomba Wizara, tutazameni, mmeboresha vituo vya afya lakini vituo hivi kama havina watumishi bado vitakuwa haviwezi kufanya kazi vizuri. Upungufu tulionao ni mkubwa, watumishi waliopo wanalazimika kufanya kazi kwa shida kwa sababu wanafanya kazi ambazo zinawazidi uwezo. Watumishi ni wachache katika vituo, kwa hiyo, tunawaomba sana fanyeni utaratibu muweze kutuongeza watumishi katika idara ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali katika ujenzi wa vituo vya afya 11 ndani ya Mkoa wa Shinyanga. Vituo hivi vimekamilika, lakini kinachonisikitisha mpaka sasa hivi hatujapata vifaa tiba. Kwa hiyo, niwakumbushe Wizara ya Afya, vituo hivi vinahitaji kufanya kazi ili viende vikatimize lengo ambalo mmelikusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo hili ni zuri na linapendeza hata ukiangalia hali ambayo inaonekana katika vituo vyetu vya afya, lakini haviwezi kufanya kazi kwa sababu lengo lililokusudiwa halijaanza kufanya kazi. Hakuna vifaa ambavyo vimeletwa katika vituo vyetu vyote 11 vilivyopo ndani ya Mkoa wa Shinyanga na hivyo lengo lile la kwenda kufanya upasuaji bado halijaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, niwaumbushe mtuletee vifaa tiba katika vituo 11 ambavyo mmetujengea katika Mkoa wetu wa Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie kusema kwamba naipongeza sana Serikali, nilikuwa nikisema sana kuhusu Hospitali ya Wilaya ya Shinyaga, hospitali sasa hivi inaendelea. Nawashukuru sana kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona unanitazama, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)