Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kwanza kabisa niungane na hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie maeneo machache katika Wizara hii ya Afya, nianze na eneo la maboma wazi katika maeneo yetu ya vituo vya afya. Tuna maboma wazi katika maeneo mengi nchini na maboma wazi haya yamejengwa na wananchi, lakini Serikali haipeleki hela kwa kile kiwango ambacho kimeridhiwa kwamba, wananchi wanajenga maboma na Serikali inamalizia. Mpaka sasa kuna maboma zaidi ya 3000 nchi nzima ambayo hayajaezekwa na ni nguvu za wananchi zinapotea bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na miradi isiyokidhi hadhi. Miradi hii ipo mingi, lakini unaenda kwenye zahanati unaenda kukagua zahanati unakuta kuna mapungufu mengi na zahanati nyingi zimejengwa chini ya viwango, huu ni ubadhirifu wa pesa za umma. Tunaomba Wizara iangalie ni jinsi gani wanaweza kwenda mbele zaidi kwa kutafuta wakandarasi wenye elimu na wenye utaalam mzuri katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo la ukusanyaji wa damu salama. Katika maeneo mengi ya mikoa kulianzishwa vituo vya ukusanyaji damu salama, lakini tangu mwaka 2015 mfadhili aliyekuwa wa mradi huu alikabidhi magari ya Red Cross Serikalini, lakini magari hayo mpaka sasa hayajawahi kufanya kazi, jambo ambalo linasababisha vifo vingi kwa sababu vituo hivi vimeshindwa kukusanya damu salama katika maeneo mengi. Mfano mzuri ni Mkoa wa Kagera na Mkoa wangu wa Manyara damu salama haiko kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo la ustawi wa jamii. Kumekuwa na tabia ya ukatili wa watoto katika maeneo mengi, lakini tuna mabaraza yanayohusika katika maeneo mengi, kwenye kata kwenye mikoa kwa ajili ya kusikiliza hizi kesi za watoto, lakini mabaraza hayo hayafanyi kazi vizuri. Tuna kesi nyingi ambazo hazitatuliwi kwa wakati, lakini nyingi zinazimwa na watoto tayari wameshapata madhara makubwa. Sasa Wizara ituambie wana mpango gani wa kuwawezesha maafisa maendeleo ya jamii katika maeneo mengi nchini, ili waende sasa wakafanye hii kazi kwa weledi?

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wengi wameathirika na wamefanyiwa vitendo vya kikatili. Mfano mzuri ni Hanang ambapo ni Basutu, Balangalalu na Babati pia wapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo la utatuzi wa migororo ya ndoa na matunzo ya watoto. Kila siku hapa Bungeni tunalia na hali ya kusema watoto wa mitaani. Watoto wa mitaani tunawatengeneza sisi wenyewe, kwa nini tunawatengeneza sisi wenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii inayotakiwa isimamie unakuta kesi nyingi zinaendeshwa, lakini kwa sababu unakuta mama au mzazi mmojawapo hana uwezo mzuri kesi tayari imepelekwa Mahakamani, kesi inaamuliwa mtoto aende kwa upande mmoja wa mzazi mmoja. Matokeo yake ule mgogoro kama haukutatuliwa vizuri ndio maana unaona unasikia kesho mkoa fulani watoto wamechinjwa, mkoa fulani baba ameuwa mtoto, haya ni mambo yanayoumiza Taifa, lazima yaangaliwe kwa wakati na lazima yasimamiwe na wizara husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumechoka kusikia vifo vya watoto kila siku watoto wanachinjwa, Tanzania nzima hakuna siku mtoto hachinjwi ni kwa sababu ya ubadhirifu wa kutokutumia sheria. Hongo zinatembea huko, mzazi anasema ana uwezo wa kumchukua mtoto wake, anamchukua anampeleka kwa mama wa kambo, yule mtoto anaendelea kunyanyasika, mwisho wa siku kisaikolojia anaathirika halafu tunasema tuna watoto wa mtaani, hiyo haiwezekani. Nendeni mkakae mliangalie hili namna ya ku-solve watoto wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo la vyumba vya wagonjwa mahututi. Hospitali nyingi za wilaya hazina vyumba ambavyo vinakidhi mahitaji ya mgonjwa mahututi; mfano mzuri ni Hospitali ya Mrara chumba cha wagonjwa mahututi ni sawa na gereji ya magari. Nendeni mkaangalie pale Babati, mkashuhudie hili ninalozungumza, boresheni hizi huduma mtusaidie, tuwasaidie Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie eneo moja ambalo nafikiri litakuwa ni la mwisho. Maeneo mengi ukienda kwenye hospitali za wilaya, kila unapomfikisha mgonjwa, hasa wale wagonjwa wanaopata ajali wanasema damu haipo. Sasa kwenye hotuba ya Waziri ameandika amesema damu sijui lita elfu ngapi hizi, hizi damu kwa nchi nzima hazitoshi na tunasema tunachangia damu salama kwa hiyari, ile kampeni endelezeni, ili tusaidie Watanzania walio wengi. Hii idadi ya damu uliyoandika hapa Mheshimiwa Waziri haitoshi kwa nchi nzima Tanzania kila siku watu wanahitaji damu salama na wanahitaji kuongezewa damu kupitia magonjwa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru wewe kwa haya machache niliyochangia. Kuna eneo hili la maendeleo na uwezeshaji wa wanawake. Eneo hili sidhani kama Wizara inafuatilia vizuri katika maeneo yake. Hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye maeneo yao wamekuwa miungu watu. Hii mikopo mnayosema namna ya kuwezesha wanawake VICOBA, hawa watu hawafanyi hii kazi kwa weledi. Afisa Maendeleo anataka rushwa ili mradi tu wanawake wapate mkopo. Hii siyo sahihi! Hii ni haki yao ya msingi akina mama kupata huu mkopo na upo kwenye sera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, angalieni hivi vitu ambavyo vinagusa jamii. Kila siku tunaimba hapa issue ya dawa lakini kuna mambo ambayo tukiyasimamia mambo mengine yanaweza yakaenda sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)