Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ili niweze kuchangia hoja ya Wizara ya Afya. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya katika nchi hii ya kutoa huduma za afya kwa Wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili naiunga mkono hoja hii asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni ujenzi wa zahanati pamoja na Vituo vya Afya. wananchi wamehamasika wanajenga Vituo vya Afya, wanajenga zahanati kila kijiji. Lakini changamoto kubwa ambayo tunayo pamoja na ujenzi wa zahanati na Vituo vya Afya changamoto ambayo inatukabili ni upungufu wa watumishi wa Idara ya Afya kada mbalimbali. Kwa hiyo, nilikuwa naishauri Serikali iongeze watumishi katika vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali za wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya ilikuwa na mpango wa kujenga vyuo kwa ajili ya ku-train wahudumu wa afya, kwa mfano matabibu, hawa clinical officers pamoja na tabibu wasaidizi (clinical assistants), sasa mpango huu uliishia wapi? Kwa sababu, ilikuwa ndio mikakati ya Wizara hii ili kuongeza watumishi katika vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusu Bohari ya Dawa – MSD. Bohari ya Dawa – MSD inafanya kazi nzuri sana; Bohari ya Dawa ndiyo inayosambaza dawa nchi nzima, vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa, hospitali za rufaa. Lakini pamoja na kuongeza fedha za dawa katika bohari ya dawa bado changamoto hiyo inaikabili bohari ya dawa. Sasa Mheshimiwa Waziri je, mwaka huu mmeongeza fedha kiasi gani kwa ajili ya bohari ya dawa kwa sababu, zahanati zinaongezeka, vituo vya afya vinaongezeka, lakini dawa ni zilezile? Sanduku moja la dawa halitoshi kwenye zahanati kwa sababu, sasa kuna ongezeko kubwa sana la wananchi. kwa hiyo, je, mwaka huu mmeongeza fedha kiasi gani kwa ajili ya bohari ya dawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, ni kuhusu vyuo vya maafisa afya. Mpwapwa kuna chuo cha maafisa afya, lakini chuo hiki hakijakarabatiwa, hakina vifaa vya kutosha, walimu ni wachache.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naishauri Serikali kwamba, hivi vyuo vya afya vyote nchini naomba Mheshimiwa Waziri hawa maafisa wa afya vilevile ni watumishi katika idara yako, lakini vyuo hivi sijui Wizara ya afya kama mnaviangalia kwa kweli, kwa sababu hii kada ya maafisa afya ni muhimu sana na hawa ndio wanashughulikia hasa zaidi afya, kinga na ndio wanaopambana na magonjwa ya kuambukiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa vyuo hivi naomba sana Mheshimiwa, kwanza bajeti mnayovitengea ni kidogo sana, halafu vifaa havitoshi, walimu hawatoshi, majengo hayafanyiwi ukarabati, kwa hiyo, nilikuwa nashauri Mheshimiwa Waziri uviangalie kwa huruma vituo hivi vya maafisa afya, na bahati nzuri mimi ni afisa afya mstaafu kwa hiyo, kada hii naifahamu vizuri sana. Hawa ndio wanaopambana na magonjwa ya kuambukiza, kutoa elimu ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kwenye hotuba yako umeelezea mambo ya elimu ya afya kwa umma (Health Education), elimu ya afya ni muhimu kweli. Katika Wizara ya Afya tuna kinga na tiba, sasa tunasema kinga ni bora kuliko tiba kwa sababu, kinga ni gharama ndogo, lakini tiba ni gharama kubwa. Kwa hiyo, nadhani kada hii ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri ungeiangalia kwa huruma zaidi, ili waweze kupata maslahi ya kutosha, vyuo hivi mdahili wanafunzi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ni upungufu wa watumishi katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa. Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Mpwapwa ni kubwa, ina wananchi zaidi ya 400,000 na tuna vituo vingi kama nilivyosema, lakini tuna upungufu wa watumishi kama 450 wa kada mbalimbali za afya. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Idara ya Utumishi, Wizara ya Utumishi, tukiomba tukipeleka maombi yetu pale kutaka watumishi tunapata watumishi 6, tunapata watumishi 10, lakini tuna upungufu wa watumishi zaidi ya 450 kwa hiyo, tulikuwa tunaomba watumishi waongezewe katika Hospitali hii ya Wilaya ya Mpwapwa.