Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana jioni hii. Kwanza kabisa naomba nimtangulize sana Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya kwa kuboresha Wizara ya Afya. Kwa kweli mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Mheshimiwa Rais toka amechaguliwa ameweza kufanya kazi kubwa sana na hii kazi inaonekana hata huko vijijini kote anakokwenda pongezi nyingi amekuwa akizipata. Kwa hiyo kwa kweli tumpongeze na tupongeze Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuwachagua hawa Mawaziri, hajafanya kosa, dada yetu Mheshimiwa Ummy anafanya kazi nzuri sana. Hii Wizara nakumbuka kuna siku moja mtu mmoja alisema kwamba huyu dada anafanya kazi kama mwanaume, nikasema hapana, wanawake tunapiga kazi sio kwamba lazima awe mwanaume. Kwa hiyo dada Ummy anatutendea haki sisi wanawake wote. Vile vile Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, Naibu Waziri pia kwa kweli anajituma, wakati wowote yuko tayari tukimwita anaitika na amekuwa anatusaidia kazi nyingi sana ambazo anatufanyia. Niwapongeze sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze Makatibu Wakuu, tena yuko mwanamke kwenye Wizara hii, hiyo ndio inahakikisha kwamba wanawake wanaweza, wachape mzigo, waoneshe kwamba sisi wanawake tukipewa kazi tunafanya kweli kweli, niwapongeze na watendaji wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali kwanza kabisa kwa kutenga pesa kwa ajili ya hospitali za wilaya 67, hospitali za mikoa nane, vituo vya afya 332 nchini na sisi katika mkoa wetu tuliweza kupata bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ambazo kwa kweli tunashukuru Hospitali ya Kilolo, wakati wowote Mheshimiwa Rais atakuja kuizindua tunashukuru sana. Vilevile tumepewa pesa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Mufindi na Hospitali ya Iringa DC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, hili ni ombi maalum tunayo Hospitali ya Frelimo ambayo yenyewe siyo inajengwa tayari ishajengwa kuanzia 2008 imeanza kufanya kazi. Sasa niombe kwa kweli Serikali ifanye utaratibu, hospitali ambazo tayari zinafanya kazi zina upungufu kwa mfano ile ya Frelimo ni kujengewa tu wodi za akinamama, akinababa na watoto ili kupunguza msongamano mkubwa kabisa uliopo katika hospitali ya mkoa. Kwa hiyo wangekuwa wanatoa kipaumbele kwa hospitali ambazo tayari zinafanya kazi na zinaweza kupunguza msongamano kwenye hospitali zetu za mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia Serikali iboreshe sasa vituo vya afya ambavyo vimeshajengwa ili kupunguza vifo vya akinamama na watoto kwa sababu kujenga ni kitu kingine, lakini tusipoboresha bado tatizo la vifo litabaki kuwa pale pale. Sasa niombe vifaa tiba vipelekwe, manesi wapelekwe ili kuhakikisha kwamba vituo vyote vinapatiwa pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa hospitali yetu ya mkoa. Hospitali yetu ya Mkoa ina changamoto nyingi sana; ya kwanza, Madaktari Bingwa wa Upasuaji wote hawapo, wameondolewa, wananchi wanapata shida mno, mno. Sasa hivi mgonjwa akitaka kufanya upasuaji, aidha apelekwe Muhimbili au aletwe Dodoma kwenye hospitali yetu ya Benjamini Mkapa. Bado kuna tatizo kubwa sana la magari, ambulance tuliyonayo imepewa jina la Ummy Mwalimu ambulance, ambayo kwa kweli kwanza ni ya petroli lakini imekuwa ndio hiyo hiyo moja nyingine zote ni mbovu, aidha wale Madaktari waweze kuchukua katika vituo vya afya na vituo vya afya bado vinakosa ambulance. Kwa hiyo nimwomba Mheshimiwa dada Ummy kwa heshima na taadhima kwanza kabisa aje pale Iringa atembelee hospitali yetu au Naibu azungumze na wafanyakazi walioko pale na Madaktari ili kwa kweli awape hata moyo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna upungufu wa watumishi, kuna upungufu wa Manesi, kuna upungufu pia wa nyumba na sio upungufu hakujawahi kujengwa nyumba za Madaktari kutokana na ufinyu wa eneo. Sasa niombe kabisa tufanye utaratibu wa kuhakikisha kwamba Madaktari wetu wanapatiwa nyumba kwa sababu hata call allowances zile zimekuwa ni shida mno kupatiwa pamoja na kuwa hawana nyumba, wanapokwenda kutibu wagonjwa usiku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona changamoto kubwa zilizopo katika hospitali zetu kwanza kabisa kukosekana kwa hizi mashine wagonjwa wanakufa mno kwa sababu ugonjwa wanaotibiwa wanakuwa hawaujui. Madaktari sasa wana- guess aidha huyu mtu anaweza akawa anaumwa homa au akiwa na homa pengine ana mafua au malaria. Sasa ni vizuri pengine kutokana na changamoto hii ya vifaa tungefanya hata miradi ile ya PPP ili waweze kufunga katika hospitali zetu, ni bora tulipie hiyo huduma kuliko kwenda kuitafuta hiyo huduma Muhimbili au kuja Dodoma. Kwa sababu ukienda Muhimbili bado utatumia gharama kubwa, lakini tukipata wawekezaji wakawekeza katika hospitali zetu itatusaidia, wagonjwa watatibiwa magonjwa ambayo kwa kweli yatasaidia kwamba watakuwa wanajua anachotibiwa mgonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipongeze Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali ya Benjamini Mkapa, kwa kweli hizi hospitali hata katika hotuba yake ametueleza kwamba zimefanya kazi kubwa kweli kweli, badala ya wagonjwa kupeleka nje ya nchi sasa hivi wanatibiwa hapa nchini. Hii ni kazi kubwa ya Chama hiki cha Mapinduzi na Rais wetu na Serikali hii kuhakikisha kwamba wananchi wanatibiwa hapa nchini. Hata hivyo, kuna changamoto, naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri, wanapokwenda kutibiwa kwenye hizo hospitali, wanavyosubiri sasa tiba hizo labda kufanyiwa mionzi ya kansa au figo hawana pa kukaa, wamekuwa wakipata shida mno. Niombe sasa kama kuna uwezekano ufanywe utaratibu, watengenezewe maeneo maalum ya kuhakikisha kwamba wakati wanasubiria basi wanakaa pale, kwa sababu tumekuwa tukifanya michango kwa wagonjwa ambao wamekuwa wakitoka nje kwenda kusubiri hayo matibabu, kwa kweli hili naliomba liangaliwe kwa hali ya juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze pia MSD, wanafanya kazi nzuri mno ya kusambaza dawa, nakumbuka kipindi kilichopita kila aliyekuwa anachangia alikuwa anasema upungufu wa madawa, lakini MSD sasa hivi inafanya kazi nzuri mno hata katika Mkoa wetu wa Iringa wamekuwa wakisambaza dawa, nimefanya ziara nimekuta wanafanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo niwaombe waendelee kufanya kazi hiyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu Bima ya Afya; nipongeze Bima ya Afya kwa Wote, kwa kweli huu mpango najua utachukua muda mrefu, lakini uwepo mchakato na wenzangu wamelizungumzia sana, uwepo mchakato wa haraka kuhakikisha wale ambao hawana Bima ya Afya sasa hivi wanakufa, kuna wengine ambao hawatibiwi, tufanye mchakato kwa sababu najua walio wengi na ndio wanyonge na Serikali hii inawajali wanyonge, sasa tuhakikishe hawa wanyonge wetu ambao hawana bima za afya tuwawekee utaratibu mzuri wa kuwatibu ili waweze kutibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie huduma ya afya kwa watu wenye ulemavu; Mheshimiwa Ummy alishakuja kujionea kwenye kongamano la watu wenye ulemavu kwa Ikupa Trust Fund. Nami pia ni Mjumbe katika Kamati ya Watu Wenye Ulemavu, hawa watu wanapata shida sana kutokuwa na mkalimali wa kuwasaidia wakati wanaenda kwa Daktari. Sasa je, Serikali inawasaidiaje? Kuna mmoja alisema kwamba alipoteza mpaka mtoto wake, yeye ni kipofu lakini ameenda kujifungua mtoto kabadilishiwa mtoto, sasa wawekewe utaratibu mzuri kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu nao wanatendewa haki katika matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie dawa za uti wa mgongo, ni ghali mno, watu wengi sana wanakufa mimi niliona, waweke utaratibu dawa hizi zipunguzwe bei ili watu waweze kutibiwa, zinaua watu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Bima ya Wazee na Watu Wenye Ulemavu; hii bima pamoja na kuwa vitambulisho sisi kwetu wamepata wengi sana, lakini bado dirisha lile lina dawa kiasi kidogo sana, wengi hawapatiwi, ukizungumza na wazee unaona wanalalamika kwamba dawa zile hawapatiwi zote na kuna baadhi ya vipimo hawapimwi na wazee kila wakati ni kuumwa, ni migongo, ni nini, lakini dawa hawapatiwi. Niombe kwa kweli Serikali iangalie wazee wetu wapatiwe dawa ambazo zinahitajika katika kile kitambulisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tutakuwa hatuwatendei haki wadau ambao wamekuwa wakichangia huduma za afya katika mkoa wetu. Tumpongeze sana Mheshimiwa Asas m-NEC wetu wa Mkoa, kwanza kabisa ametujengea jengo la damu salama katika mkoa wetu, lakini ametujengea jengo la watoto njiti, vilevile ICU, jamani Mwenyezi Mungu ampe nini huyu baba, tunamshukuru sana. Pia kajenga jengo la wazee, zuri, Mheshimiwa Waziri aje atutembelee aone wazee wanaishi kwa raha mustarehe. Hii yote ni kazi ya m-NEC wetu wa mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama cha Mapinduzi Wilaya, pia kimeleta mashine za kufulia mashuka. Kwa hiyo hata Chama chetu cha Mapinduzi kinafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo kwa kweli na mimi nitoe pole kwa Mheshimiwa Mengi, pole nyingi sana kwa sababu ni baba ambaye ametufundisha mambo mengi sana na Mwenyezi Mungu amrehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Peter Msigwa ajiandae Mheshimiwa Janeth Masaburi

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)