Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi kuweza kuchangia kwenye hotuba ya afya ya Mheshimiwa Waziri ambayo ipo mbele yetu. Narudia tena kwa mara nyingine nilisema kwenye bajeti ya Waziri Mkuu na baada ya kupongeza juhudi zilizofanyika kwenye hospitali ya Muhimbili kuweza kuweka vipimo vya kutosha na vifaa tiba nikaiomba Serikali ihakikishe imepeleka vifaa tiba vya kutosha na vya kisasa kwenye hospitali zote za kanda na hospitali zote za rufaa Mikoa Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tulipo sasa hivi, Hospitali yetu ya Kitete, ambayo ni Hospitali ya Rufaa na Hospitali ya Mkoa wa Tabora, ukienda pale haina sifa ya kuweza kuwa Hospitali ya Rufaa kwa sababu haiwezi kutoa huduma za Hospitali ya Rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wagonjwa wengi ambao wanakuwa referred kutoka kwenye Hospitali za Wilaya wanakwenda Bugando, Muhimbili na maeneo mengine. Sasa fikiria mtu atoke Tabora mpaka Bugando, atoke Tabora mpaka Muhimbili na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kuweza kufanya, naomba Serikali ihakikishe kwamba inaweza kuweka vifaa tiba vya kutosha katika Hospitali zote, Hospitali ya Itete na Hospitali nyingine za Tanzania nzima kwa kweli, tutaweza kusogeza huduma karibu wale wananchi masikini ambao hawana uwezo wa kupata hata nauli ya kutoka Tabora, kuweza kwenda mpaka Muhimbili au kuweza kwenda Bugando waweze kupata huduma kwa maeneo ambayo wapo na maeneo ambayo ni ya karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora hata ile Hospitali ya Nkinga tu yenyewe inatoa huduma bora zaidi kuliko hata Hospitali ya Kitete. Kwa hiyo, naomba jicho la pekee kabisa kwenye Hospitali ya Kitete ya Mkoa wa Tabora ili wananchi wa Mkoa wa Tabora wanaopata rufaa kwenye Wilaya yetu waweze kupata huduma pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la huduma za afya kwa Wilaya ya Kaliua. Nashukuru kwamba tumetengewa fedha mwaka huu shilingi bilioni 1.5 ya kuweza kumalizia Hospitali yetu ambayo tumeijenga kwa fedha za ndani, tumekamilisha almost karibu nusu. Jengo la OPD tayari, jengo la akina mama na watoto tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoiomba Serikali, najua kwamba miundombinu iko kwenye Wizara ya TAMISEMI, lakini kwa msukumo wa Mheshimiwa Waziri kwa kuwa alifika kule akaona kazi inayofanyika, naomba aweze kusukuma fedha hii itoke ili Hospitali ile ifunguliwe, kwa sababu mwenyewe alituahidi kwamba tukimaliza jengo la akina mama tunaweza tukapata kibali cha muda ifunguliwe tuendelee na majengo mengine. Naomba msukumo wa Wizara ili tuweze kufungua Hospitali ile wananchi wa Kaliua ambao kiukweli wengi wao wanapata huduma mbali na Wilaya waweze kupata huduma pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni dawa. Tumekuwa tunapata dawa na dawa zimeboreshwa kwenye Vituo vya Afya na kwenye Zahanati zetu, lakini kuna Zahanati ambazo zina idadi ya watu wengi sana ambapo ule mgao wa huduma ya Zahanati hauwatoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Zahanati ya Usinge nimeshaleta maombi kwa Mheshimiwa Waziri na kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Zahanati ya Usinge ina tibu watu 35,000 kwa mwezi, inahudumia Kata mbili na pale hamna Kituo cha Afya. Tukawaomba Zahanati kama ile ya Usinge watu 35,000 kwa mwezi, Zahanati ya Igagala watu 28,000 kwa mwezi wapewe mgao wa Kituo cha Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wananchi wanaona kabisa kwamba hawapati dawa kwa sababu zikiletwa ndani ya wiki mbili zimeisha. Kwa hiyo, wakienda wanaambiwa dawa hamna kwa sababu idadi ya watu wanaopata huduma pale ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ahadi yake ya kuweza kutupatia Zahanati hasa hizi mbili; Zahanati ya Usinge na Igagala waweze kupata mgao wa dawa unaofaa kwa Kituo cha Afya ili wananchi walioko maeneo yale waendelee kupata huduma kwa quarter nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni huduma za wazee. Mheshimiwa Waziri ametuambia tuna Makazi ya Wazee 17 ya Serikali, lakini pia tuna makazi ya Wazee 14 ya Taasisi za Umma, Watu binafsi pamoja na Taasisi za Mashirika ya Dini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Makazi ya Wazee ya Serikali yana hali mbaya sana. Wazee wengi walioko kule wanateseka hawana huduma. Hakuna chakula na hakuna mavazi. Mfano mmoja mdogo, Wabunge wengi wanapita njia hii ya kwenda Tabora pamoja na Singida, ukipita pale Sukamahela, ule mlima pale, kuna wazee kibao wamekaa pale wanaomba barabarani. Wamechoka kukaa kule Kituo cha Sukamahela, wanakuja kukaa barabarani kuja kuomba. Ukiangalia mavazi waliyovaa, wako pale wanadonoa chawa kwenye nguo zao, kwa maana kwamba hata hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naomba kama mmeamua kuwaweka kwenye vituo, wapate huduma ili ukipita pale ukiwa na mkate uwape, ukiwa na maji uwape. Wale ni wazee ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, kile Kituo cha Sukamahela kwa kweli kinatia huruma. Mimi mpaka siku nilienda kukitembelea japokuwa siyo Jimbo langu, nikasema hebu nikaone hao wazee wanakaa maeneo gani? Wanatia huruma, wategemee mkate wa barabarani kweli! Magari yapite na bahati mbaya pale ni mlimani, likiharibika gari pale ndiyo wapate chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee hawa wamefanya kazi kubwa. Leo tuko hapa kwa sababu walikuwepo hawa wazee huku nyuma. Naomba vituo vyote vya Serikali vihudumiwe vizuri. Ukienda angalau kwenye Taasisi za dini zina unafuu, kwa sababu wanapeleka misaada mbalimbali, watu wanaenda kutoa sadaka kule, lakini hivi vya Serikali havitembelewi mara kwa mara na watu ambao ni wasamaria wema. Kwa hiyo, naomba sana wazee hawa waweze kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni huduma za wazee za Bima ya Afya. Serikali kwa muda wa miaka minne imekuwa ikisisitiza wazee wapatiwe vitambulisho vya kutibiwa bure, lakini bado speed za Halmashauri kutoa vitambulisho hivi ni ndogo sana. Mpaka leo wazee wengi hawana vitambulisho vya kutibiwa bure. Mojawapo ni Wilaya yangu ya Kaliua, tunasisitiza kila vikao wazee wapewe vile vitambulisho, lakini mpaka leo, zaidi ya robo tatu hawajapata vile vitambulisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba msukumo wa Serikali, wazee hawa, wapate vitambulisho wawe na dirisha lao waweze kupata haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni migogoro ndani ya ndoa. Mheshimiwa Waziri ameeleza kwa umakini mkubwa sana kwenye hotuba yake, migogoro imekuwa mingi sana ndani ya ndoa na wanaopata matatizo ni wanawake. Leo migogoro ni kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imezuka tabia nyingine hapa Tanzania, mimi naishangaa sana. Wanawake wanaojifungua mapacha zaidi ya watoto watatu mpaka wanne waume zao wanawakimbia. Yaani baraka inakuja nyumbani, halafu wanawake ambao wamepata mapacha wanakimbiwa. Nimekuwa nafuatilia mpaka nashangaa. Wengi wanasaidiwa sana na watu kwenye mitandao, waanze kuchangiwa shilingi 100/=, shilingi 200/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ituambie, wana mpango gani kwa watoto hawa wanazaliwa wanne mpaka watano kwa familia ambazo ni masikini halafu wanawake wanakimbiwa na waume zao. Wanaume wengine sijui ni mashetani! Unapata baraka, halafu unakimbia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano binti mmoja ambaye aliomba mimba kwa muda wa miaka minne hajapata mimba. Kapata mimba mwaka 2018 kajifungua mwaka huu watoto watatu, mwanaume kamwachia wale watoto kakimbia. Yaani mpaka unashangaa. Hivi huyu ni binadamu au mtu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naiomba Serikali, watoto ni baraka ya Taifa, watoto ndiyo raslimali, nguvu kazi ya Taifa. Watoto hawa wanaozaliwa kwa familia masikini, mapacha watatu, wanne, watano, Serikali inawasaidiaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nakua nilikuwa nasikia kuna kitu ambapo ukijifungua watoto zaidi ya watatu Serikali inakusaidia kuela wale watoto mpaka inawasomesha. Siku hizi nadhani hicho kitu sijui hakipo! Kwa hiyo, naomba Serikali itusaidie sana katika kuhakikisha kwamba watoto hawa waliozaliwa kwenye familia masikini ambao ni mapacha waweze kupata huduma nzuri, waweze kuwa ni Taifa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la Sheria ya Ndoa, migogoro imezidi, akina mama wana mizigo mikubwa ya kuweza kulea watoto wenyewe. Tunaomba Sheria ya Ndoa ije Bungeni, iliyopo imepitwa na wakati. Tumeongea sana muda mrefu kwenye Bunge hili. Kwa nini Sheria ya Ndoa haiji Bungeni tuifanyie marekebisho ili watoto wapate stahiki zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani akina baba wanawakimbia watoto. Ile Sheria ya Ndoa ukiangalia viwango vilivyoko kule ni vidogo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie Sheria ije Bungeni tuipitishe ili watoto wanaoachwa mzigo kwa akina mama wapatiwe huduma stahiki za kusoma za kula vizuri na huduma nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante. (Makofi)