Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kunijalia uhai na kuanza Mfungo wa Ramadhani vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali hasa Wizara ya Afya kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya ya kuhakikisha kwamba afya za Watanzania zinakuwa katika mikono salama. Uwekezaji mkubwa mnaufanya kwa maana ya kutenga fedha, kuzipeleka na kuzisimamia lakini kuhakikisha kwamba vifaa tiba vinapatikana na wauguzi wanakuwepo. Hili ni jambo kubwa, muendelee kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nisiache kumshukuru Mheshimiwa Angellah Kairuki, Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji ambaye aliamua kwa makusudi katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani yeye akishirikiana na wanawake wanaofanya kazi na Benki ya UBA walijitolea kuleta mashuka katika Hospitali ya Temeke. Wananchi wa Temeke wanakushukuru sana na kwao hawakuoni tu kama kiongozi lakini wanakuona kama ndugu yao wa karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Waziri Mkuu ambaye alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Temeke. Ziara yake imekuwa na tija sana, amerekebisha mambo kadha wa kadha lakini pia alisisitiza baadhi ya mambo ambayo Wizara ilibidi muendelee kuyashughulikia. Moja, ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunapata mashine ya kufulia katika Hospitali ya Temeke. Ni kweli hakuna tatizo la kufua kwa sababu wanakwenda kufua Muhimbili lakini kwa upekee wa Hospitali ya Temeke ambayo pia ni kituo cha magonjwa ya mlipuko si vizuri sana wakawa wanaenda kufua katika eneo linguine. Ni vizuri kwa ubora ambao mmeboresha hospitali ile basi tungekuwa pia na mashine za kisasa za kufulia ili shughuli zote zifanyike pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hospitali ile haijakabidhiwa kwa Wizara wakati ilipokuwa chini ya Halmashauri tulianza kujenga jengo la emergency kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa lakini pia na Ubalozi wa China. Sasa wakati tunakabidhi ujenzi ule ulikuwa bado haujakamilika na mpaka leo umesimama. Si vizuri kwa wadau wa maendeleo ambao wametuchangia halafu waone lile zoezi haliendelei. Tunaomba katika hiyo shilingi bilioni 10 ambayo Mheshimiwa Waziri umesema unayo basi tuelekeze hiyo shilingi milioni 100 iende pale ikamalize lile jengo la emergency.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto ya generator upande huu wa utawala. Hii imekuwa ni tatizo sana kwamba umeme unapokatika madaktari wanakosa standby generator ya kuwasaidia kwa sababu ile generator kila siku imeharibika. TEMESA wanaambiwa kwamba ile generator imekufa watoe kibali ili hospitali ikanunue generator lakini hawataki kila siku wanataka wawe wanalitengeneza baada ya siku mbili limekufa. Naomba mtusaidie waambieni hao TEMESA watoe hicho kibali hospitali ikanunue generator nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwashukuru kwa hayo mazuri mnayoyafanya, nina kero moja nataka niifikishe na hii ni kero kubwa kwa wananchi siyo tu wa Temeke lakini yawezekana ni Watanzania nzima na hili ni tatizo la kuzuia maiti eti kisa kuna deni hospitali. Kumekuwa na utaratibu huo hasa katika Hospitali ya Muhimbili na Mloganzila kwamba marehemu anapofariki kama anadaiwa iwe Sh.20,000, Sh.100,000 au kiasi chochote maiti inazuiwa isitoke hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili si la kibinadamu, linaondoa utu ambapo kama Watanzania tulizoea kuheshimu maiti. Hata barabarani maiti ikiwa inapita, unasimama unaacha maiti ipite. Huu ujasiri wa mtu kuzuia maiti unatoka wapi? Kwa nini maiti izuiliwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye mazingira ya kawaida kabla hatujaenda kuzika huwa tunatangaza jamani anayemdai marehemu ajitokeze, tunamkabidhi kwa ndugu wa marehemu wataendelea na shughuli za kudaiana baadaye lakini sisi tunaenda kuzika. Wengine kuzika ni ibada na sisi Waislamu tunasisitizwa mtu akishafariki awahishwe akazikwe lakini leo tunashindwa hata kuitekeleza hii ibada yetu kwa sababu badala ya kuchukua maiti mkazike mnaanza kupita na daftari la kukusanya michango.

T A A R I F A

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nafikiri Mheshimiwa Mbunge anachanganya, nimesema hapo awali kwamba ni utaratibu kabla hatujaenda kuzika tunatangaza wanaomdai marehemu wajitokeze, wanaodaiwa na marehemu wajitokeze, kisha tunawakabidhi kwa familia waendelee na taratibu za kulipana lakini hatuzuii kwenda kuzika. Sasa sijui yeye anazungumzia Uisalamu katika kitabu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu hapa ni kwamba, kwanza wakati mwingine unakuta maiti inayozuiliwa kwenye hospitali hiyo kwa sababu anadaiwa Sh.120,000 tayari labda ameshaugua hapo miezi miwili na bili nyingine ameshalipa yaani unakuta mgonjwa ameshalipa zaidi ya shilingi milioni 2 siku anakufa kwa sababu tu kuna siku mbili za mwisho bili yake haikulipwa eti tunazuia maiti, hii siyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuweka fedha nyingi kwenye huduma za afya na kutatua kero za wananchi haiendani na jambo hili linalofanyika la kuzuia maiti hospitalini. Dhamira ya kuwekeza katika hospitali si kufanya biashara ni kuboresha huduma lakini hata ingekuwa biashara mabenki haya yanakopesha hayadai maiti, mtu akifa deni lile limekufa inakuwaje hapa hospitalini? Tulitegemea sasa hivi tuwe tunakwenda mbele zaidi kwamba mgonjwa ambaye ameugua miezi miwili, mitatu hospitali na alikuwa analipa bili akifa hospitali hata itoe incentives ya kusafirisha ile maiti kwa sababu alikuwa wa kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anaonekana anaguswa na maisha ya wananchi lakini anaguswa pia na misiba inayotokea, ndiyo maana hata kwenye hotuba ameanza kwa kuwapa pole watu ambao wamepoteza ndugu zao. Sasa kauli hii haiwezi kuleta tija endapo bado maiti za watu zinazuiliwa hospitalini. Siyo kila jambo tumwachie mpaka Mheshimiwa Rais ndiyo siku asimame atoe maamuzi, hili mbona liko ndani ya mikono yenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anachapa kazi sana, Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Ndungulile namfahamu ni mtu ambaye amenyooka sana, anapenda kuhakikisha kwamba kero za wananchi zinaondoka, kwa nini hili hatuliangalii na linabaki kuwa kero Mloganzila na Muhimbili peke yake? Kwa nini hatulalamikii Temeke, Ilala au Mwananyamala kwani huko watu hawafi, kote huko watu wanafariki kila siku lakini haya hayatokei, mtuondolee na hili katika hizo hospitali mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kuamini kwamba hizi maiti zinazozuiliwa eti zikiachiwa ndio Mloganzila na Muhimbili zitapata hasara sana zitashindwa kutoa huduma sio kweli. Lakini kama tatizo ni fedha leo tuna makapuni haya ya bima za afya yanapata fedha kutokea kwa wagonjwa wanaopelekwa hospitalini. Na ni mara chache utasikia haya makampuni ya bima za afya yanafanya hiyo cooperate social responsibilities maana yake hata ile asilimia moja ya faida ambayo wanatakiwa kutoa kwa jamii hawatoi. Kwa nini msiweke utaratibu basi wailekeze huko iwe ina fidia hawa watu ambao hawana watu… (Makofi)

T A A R I F A

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti taarifa hiyo naipokea lakini nizidi kutoa angalizo kwamba, Serikali yetu imejikita katika kuondoa kero kwa wananchi hasa wananchi maskini na wanaoshindwa kutoa maiti zao kwa kuzuiliwa huko hospitalini wala sio matajiri ni wananchi maskini twende tukawasaidie tuondoe hii kero nakushuru. (Makofi)