Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha vizuri, lakini vilevile nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kazi kubwa nzuri inayoonekana ndani ya Sekta ya Afya. Wote ni mashuhuda tumeona bajeti ya afya ilivyopanda juu, wote tumeona hospitali nyingi kwa wakati mmoja zikijengwa za ngazi ya wilaya, lakini wote tumeona vituo vya afya zaidi ya 300 vinajengwa kwa wakati mmoja ndani ya Tanzania, wote tumeona tunavyonufaika na upatikanaji wa dawa ambayo sasa hivi huko zaidi ya asilimia 94, lakini wote tumeona huduma za matibabu ya kibingwa zinavyopatikana pale Muhimbili, Moi, Jakaya Kikwete, Benjamini Mkapa na Ocean Road. Tunasema hongera sana, Wizara wanafanya vizuri sana, sekta ya afya inafanya vizuri sana, kwa hiyo tunampongeza Jemedari wetu Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ya kuboresha afya ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiangalia Mkoani Kagera tulikuwa na hospitali kumi na nne, hospitali kumi na nne kati ya hizo kumi na mbili zilikuwa za mashirika ya dini, moja ya binafsi tulikuwa na hospitali mbili tu za Serikali, lakini katika muda mfupi kwenye bajeti iliyopita wametupatia bilioni nne na nusu tunajenga hospitali za wilaya tatu na kwenye bajeti hii naona wanatuongezea mbili, tunasema ahsante sana. Vile vile, tulikuwa na vituo vya afya 34 na kati ya hivyo ni vituo vitano tu vilivyokuwa na theatre ambazo zingeweza kuwasaidia akinamama wanaopata uzazi kinzani, wameshatupatia bilioni 5.9, tumekarabati vituo vya afya 14 ambavyo vitaongeza utoaji wa huduma nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za matibabu ni kubwa mno, hakuna mtu anayeweza kuzimudu kirahisi, ndiyo maana tunasema bima ya afya ndiyo mkombozi, hata ukienda kwenye nchi za wenzetu walioendelea kitu cha kwanza wanahakikisha kwamba binadamu yeyote anakuwa na bima ya afya. Ukija kwa Tanzania kwa bahati mbaya mpaka sasa hivi watu walio kwenye mfumo wa afya wa bima ya afya ni asilimia 33 tu. Kwa hiyo, ina maana kwamba zaidi ya asilimia 60 hawapo kwenye mfumo wowote wa bima ya afya. Ni asilimia moja wanatumia bima za afya za binafsi, asilimia saba wanatumia Bima ya Afya ya Taifa na asilimia 25 ndiyo wako kwenye Bima ya Afya ya Jamii hii CHF, lakini CHF ingeweza kuwa mkombozi kwa mfano kule Mkoani Kagera kwa mtu kulipa 30 tu, anatibiwa yeye, mke na watoto wane, kwa hiyo watu sita wanatibiwa kwa elfu 30 kwa mwaka mzima na katika kituo chochote kile katika mkoa. Kwa hiyo hii naona kwamba ndiyo imekuwa mkombozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoiomba Wizara ingeweka mkakati wa makusudi wa kuhakikisha kwamba sasa wanaenda kuhamasisha kwenye vijiji vyote kuhakikisha kwamba Watanzania sasa wanaingia kwenye hii CHF iliyoboreshwa ili waweze kupata huduma ya afya na kama tunaweza kuipandisha sasa, watu walioko kwenye CHF wakatoka kwenye asilimia 25 ya sasa, tukaenda mpaka asilimia 60, hata wanapokuja kuzungumzia Bima ya Afya kwa kila mtu itakuwa ni rahisi, watakuwa wameshazoea, wameshajua utamu wa Bima ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera inaitwa Bukoba Referral Governemnt Hospital, lakini hospitali hii ina changamoto kubwa sana. Wote mnajua Mkoa wa Kagera upo pembezoni jamani, unakwenda weee unavuka Ziwa Victoria upande ule karibu na Uganda, Rwanda na Burundi ndiyo Mkoa wa Kagera ulipo. Kwa hiyo hospitali tunayoitegemea ni hiyo Hospitali ya Rufaa ya Bukoba, lakini bado ina changamoto kibao, kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi, kati ya watumishi 6,265 wanaohitajika, wako watumishi elfu mbili mia tatu sabini na kitu ambayo ni asilimia 37.9 tu, tunaomba tupatiwe watumishi, Madaktari, Wauguzi na Madaktari Bingwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kule Mkoani Kagera hatuko kwenye grid ya Taifa kwa maana ya umeme. Kwa hiyo tunatumia umeme wa Uganda na umeme unakatikakatika, pale hospitali kuna generator ndogo sana ambayo haiwezi ku-supply umeme kwenye majengo yote. Tunaomba generator kubwa ya kutosha kuweza ku-supply umeme kwenye majengo yote ya Hospitali ya Rufaa ya Bukoba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilizungumza kwa uchungu nikiomba ambulance kwamba hospitali ile ya rufaa inayotegemewa na watu watakaoshindikana Kyerwa, Karagwe, Ngara, Biharamulo, Muleba, Misenyi na Bukoba yenyewe haina ambulance. Mtu akipata rufaa anaenda kwenye hospitali ya kanda ipo Mwanza, ni mwendo wa masaa nane mpaka kumi kwa basi. Sasa unakuta kwamba wakishakosa ambulance wanamweka mgonjwa kwenye basi pamoja nurse anamsindikiza kwa masaa hayo mpaka Bungando, ni hatari, anaweza kupoteza hata maisha. Niliomba mwaka jana Mheshimiwa Waziri aliniahidi, lakini sijapata hata Waziri Mkuu nilimwendea na mwenyewe akaahidi bado hatujapata. Tunaomba tupatiwe ambulance ili tuwasafirishe watu wanaokuwa wamezidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niishukuru Serikali kwa sababu kwa sababu hospitali ile wanatupanulia kwenye wodi ya wazazi wanaongeza theatre ili akinamama wanaopata uzazi pingamizi waweze kufanyiwa upasuaji. Hapo awali ilikuwa kama mama anapaswa kwenda kufanya operesheni anapelekwa kwenye general theatre, akikuta kuna mtu mwingine anafanyiwa operation ya magonjwa mengine, inabidi asubiri, akinamama mnaojifungua una uzazi, mtoto anataka kutoka, unasubirije? Kwa hiyo nawashukuru sana kwa kutujengea hiyo theatre, lakini basi watuletee na fedha tununue vifaa kusudi theatre hiyo iweze ku-operate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendelea kuboresha hiyo Hospitali yetu ya Rufaa ya Bukoba, tunaomba wodi ya watoto ipanuliwe, ijengwe ICU ya watoto, lakini vile vile sasa hivi kuna tatizo kubwa watu wanazaa watoto njiti, tuwekewe na vyumba vya kulea njiti. Hospitali ya Bukoba inawachanganya wagonjwa wenye matatizo ya akili ambao tunawaita vichaa pamoja na wagonjwa wa kawaida. Sasa yule ziki-charge anaweza akawaumiza na wenzake. Tunaomba tujengewe hospitali ya watu ambao wana matatizo ya kiakili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinga ni bora kuliko tiba, tunayo kada ya wahudumu wa afya ambayo wanaitwa Community Health Workers, karibu elfu kumi na tatu katika Tanzania ambao waliopata mafunzo, lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa hivi hawajaajiriwa. Hawa wakiweza kuajiriwa kwa sababu wanakaa karibu na wananchi wanaweza kwenda kule kwa sababu wanayaelewa matatizo yaliyoko kule kwenye jamii wataamasisha ujenzi wa vyoo bora, kunywa maji safi na salama, lakini umuhimu wa kutumia vyandarua, watawafuatilia wajawazito kuhakikisha wewe mama ni mjamzito mbona hujaenda kliniki? Watawafuatilia akinamama kuwakumbusha kwenda kujifungulia kwenye vituo vinavyotoa huduma mapema, lakini vile vile wataangalia lishe na namna tunavyokula hiyo milo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwaajiri hawa tutapunguza magonjwa yanayotokana na uchafu kwa mfano kuhara, kuhara damu, kipindupindu, lakini watu watatumia vyandarua, kwa hiyo tutapunguza malaria na vilevile tutapunguza vifo vya mama na mtoto ambavyo vinatokana kwa sababu wengine hawaendi kwenye vituo vya afya. Rwanda wenzetu wamefanikiwa kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa sababu wanatumia Community Health Workers ambao kila wakati wanao akinamama kule kwenye vijiji wanawahamasisha na kuwafundisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kwa kutumia hawa watu tutakuwa tumepunguza gharama kubwa kwa sababu tutazuia magonjwa mengi, tutakuwa tumepunguza gharama ambayo sasa ingetumika kutibu hayo magonjwa na wote tunatambua kwamba kinga ni bora kuliko tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naunga mkono hoja. (Makofi)