Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu na nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kwanza niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Afya kwa sababu bila afya njema hakuna Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani hivi nilizungumza tukiwa katika Vikao vyetu vya Briefing nikamweleza Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu, kwamba kuna tatizo kubwa la Ugonjwa wa Malaria Tanzania na hasa ukiangalia maeneo yetu ya Pwani, kwa mfano, Jimbo la Mtwara Mjini, pale Mikindani na ukanda mzima wa Pwani kwa sababu kuna mazalia mengi ya mbu kutokana na chaneli za bahari ambazo zinaingia nchi kavi zinazalisha mbu wengi sana na Malaria umekuwa ni ugonjwa ambao unaua sana Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti nilimweleza Mheshimiwa Waziri wa Afya kwamba, wakati nasoma kidato cha kwanza mwaka 2000, niliweza kusikia taarifa za nchi mbalimbali duniani wamedhibiti ugonjwa huu wa malaria kwa kutoa chanjo ya malaria, nilipewa majibu ambayo sikuridhika nayo sana, lakini baada ya juzi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea nchi ya Malawi tukasikia kule Malawi kwamba wameingiza mpango wa kutoa chanjo ya malaria ikiwa ni nchi ya kwanza barani Afrika. Niwapongeze sana, hawa watu wa Malawi na jambo hili nimwombe Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kama kweli tuna nia ya dhati ya kudhibiti tatizo la malaria Tanzania, basi tutoe chanjo ya malaria kwa wananchi wa ukanda huu wa pwani ambapo kuna mazalia mengi ya mbu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linawezekana, Mheshimiwa Waziri atuletee mpango wa kuleta chanjo ya malaria hapa Tanzania kwa sababu ni ugonjwa ambao unaua sana sana na wazungu wanasema failure to plan is plan to fail kama Wizara haina mkakati wa kuweka utaratibu wa kuwa na chanjo ya malaria maana yake malaria haiwezi kuondoka Tanzania. Tunaomba Watanzania wapewe chanjo ya ugonjwa huu malaria na hii inawezekana, kama wenzetu wa Malawi wameweza kanchi kadogo tu haka inakuwaje sisi Watanzania wenye resources nyingi kwenye bahari hii kubwa sana ambayo imeleta channel nyingi za kusababisha mazalia ya mbu kuwa mengi hapa nchini Tanzania. Tunaomba Watanzania wapewe chanjo ya malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine pale Kibaha kuna Kiwanda cha Viuadudu, kiwanda ambacho kwa muda mrefu hivi sasa, Serikali ama Wizara haijaweka mpango mzuri wa kuhakikisha kwamba zile dawa zinazotengenezwa hapa Tanzania zinapelekwa kwenye halmashauri zote nchini ili ziweze kupulizia kwenye mazalia ya mbu. Kiwanda kinazalisha dawa nyingi sana, tulitembelea pale kama Kamati, cha ajabu, wale wataalam wanasema zile dawa soko lao kubwa liko nje ya nchi wakati Tanzania hapa watu wanaugua malaria, watu wanakufa kwa malaria kuliko ugonjwa hata wa UKIMWI, malaria inaua kuliko hata UKIMWI, Kiwanda cha dawa za kuondoa mazalia ya mbu kipo Kibaha Tanzania, lakini soko lake lipo nje, wakati huku watu wanakufa kwa malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ije na mkakati na mpango maalum kwamba zile dawa za kuondoa mazalia ya mbu hasa kwenye miji ya pwani kwa mfano Mji wa Mikindani, Tarafa ya Mikindani pale Mtwara Mjini, watu wanakufa sana kwa malaria, kwa sababu kuna channel nyingi za mbu. Tunaomba hii Wizara iweke mikakati wa kuleta dawa katika halmashauri zote na kuanzia Mtwara Mjini ili wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini wasife kwa malaria kwa sababu dawa zinapatikana hapa nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zikipulizwa kwenye channels zote, kwenye vile vyanzo vya maji tukapuliza hii dawa ambayo inazalishwa pale Kibaha, ugonjwa wa malaria utaondoka Tanzania, tudhibiti kwanza kwa sababu watu wanasema vaccination is better than cure, kwamba kinga ni bora kuliko kutibu sasa tusisubiri, tusisubiri watu wanaugua malaria then sisi tuweze kuomba misaada kwa hisani ya wananchi wa nchi za Ulaya ama nchi ya Marekani, tunaomba Serikali iweke kwenye bajeti Wizara hii, ije na mpango maalum wa kuhakikisha kwamba dawa zinazozalishwa pale Kibaha zinaenda kuondoa mazalia ya mbu Tanzania nzima na hii inawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuzungumzia ni hospitali za wilaya; Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa kwamba tuna mpango wa kujenga hospitali za wilaya Tanzania, lakini ukiangalia kwenye mpango huu, Mtwara Mjini sisi hatuna hospitali ya Wilaya na kila mwaka nimekuwa nazungumza kwa nini wasiweke kwenye bajeti kwamba kama yale maeneo yote ambayo tunahitaji kujenga hospitali za wilaya, basi yapewe kipaumbele yale ambayo hayana hospitali za Wilaya. Kwa hiyo naomba sana Mtwara Mjini, Manispaa ya Mtwara hatuna hospitali ya wilaya, tunaomba Mheshimiwa Ummy Mwalimu atuletee hospitali ya wilaya, wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini wanataka watibiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuzungumza hapa ni kwamba, tumezungumza kwa muda mrefu kuhusu Hospitali ya Mkoa wa Mtwara na hii hospitali Mheshimiwa Ummy Mwalimu amekuwa akiizungumza kwa muda mrefu kwamba imepandishwa hadhi na kuwa hospitali ya rufaa. Jambo la ajabu, hii hospitali hata specialist hakuna, nimekuwa nazungumza miaka yote hapa ndani ya Bunge hili, kwamba tunahitaji specialist hakuna. Nimetembelea pale, kila siku nakuwepo pale, naongea na Madaktari wananiambia Mheshimiwa Mbunge katufikishie kilio chetu hiki, hatuna specialist hapa na hii hospitali inasaidia mkoa mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu, hii hospitali nimezungumza sana na wanasema kwamba wameipandisha hadhi kuwa ni hospitali ya rufaa, haina vifaa tiba pia, hata x-ray ni mbovu. Mwaka jana nimezungumza hapa x-ray ya hosptali ya Ligula ya Mkoa ambayo inahudumia mkoa mzima ni mbovu, kwa maana hiyo hatuna x- ray, hatuna vifaa tiba, ukienda pale dawa zenyewe hakuna dawa, yaani unatibiwa lakini hakuna dawa, unaambiwa uende ukanunue. Kila siku tunazungumza maneno haya, naomba Wizara iiangalie hii hospitali ya mkoa ambayo inahudumia wananchi wote wa Mkoa wa Mtwara na wananchi wengine kutoka nchi za jirani kama Mozambique.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye hospitali hii, nimekuwa nazungumza sana, niliongea wakati nachangia Wizara ya TAMISEMI hapa kwamba, sasa hivi hospitali zote zimewekwa utaratibu wa kulindwa na watu wa Suma JKT, lakini hawa Suma JKT hawapewi utaratibu mzuri za kuweza kuwapokea wagonjwa kama walinzi pale magetini, wakati mwingine wanawapiga wagonjwa, wanawadhalilisha wagonjwa, eti kwa sababu wamepita milango ambayo siyo sahihi. Mfano mzuri ni hii Hospitali ya Ligula, kuna walinzi wa Suma JKT, wananchi wameniletea malalamiko haya mengi sana, wameniambia kwenye mikutano ya hadhara, wameniambia nyumbani kwangu, Ofisini kwangu, wameniletea kwamba wanapigwa wanapoenda kutibiwa pale Hospitali ya Ligula na walinzi waliowekwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu tatizo hili siyo la Mtwara tu, siyo Ligula tu ni katika maeneo mengi, hawa walinzi awaangalie kwa sababu mtu anakwenda hospitali akiwa anaumwa, halafu anaenda kusumbuliwa, anapigwa ni jambo la ajabu sana, tunaomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumezungumza hapa kwamba Serikali imeweka mkakati ya kuwa na hospitali za kanda Tanzania na kila mwaka tunazungumza Kanda ya Kusini hatuna hospitali ya kanda ya rufaa. Katika maeneo mengi ya Tanzania kuna hospitali za kanda, maeneo haya yote na Serikali inapeleka fedha nyingi na mwaka jana hapa Mheshimiwa Waziri alituambia kwenye bajeti kwamba ametenga bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa OPD pale Mtwara. Hiyo bilioni moja haijaletwa Mtwara, bilioni moja hiyo haijaletwa kwa ajili ya kujenga hospitali ya kanda ambayo inatakiwa ijengwe pale Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni jambo la ajabu sana, tumekuwa tukizungumza kwa muda mrefu, kila mwaka Mheshimiwa anatenga bajeti, anatuambia tunapeleka bilioni moja na bilioni moja hata kama ingepelekwa bado haiwezi kukidhi haja. Tunaomba kama kweli tuna nia ya dhati ya kuboresha hospitali hizi za kanda au kujenga hospitali ya kanda, basi kule Mtwara ambako ndiko kunatakiwa kuwe na hospitali ya kanda kusini walete fedha ya kutosha kama wanavyopeleka maeneo mengine ili na sisi wananchi wa Mikoa ya Kusini tuwe na hospitali ya kanda ambayo tutaweza kuitumia kwa ajili ya kujitibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana safari hii, Mheshimiwa Ummy Mwalimu namweleza kabisa, kama hatatenga na kuleta fedha hii nang’ang’ania shilingi yake atatoka bila mshahara kwenye Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hayo kwa niaba ya wananchi wa Mtwara kwa sababu wamenituma nije kuwaeleza wana tatizo la afya na Wanamtwara mnanisikia nazungumza ndani ya Bunge tukufu, Mheshimiwa Waziri ananisikia ninavyozungumza kwamba yale maneno mliyoniambia nije kumwambia Mheshimiwa Waziri aboreshe afya Mtwara, leo hii nazungumza na Mwenyezi Mungu ananisikia, ni siku ya kwanza ya Ramadhani nimefikisha kilio chenu wananchi wa Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri Ummy arekebishe mambo ya afya, amebaki yeye tu, mambo mengine yote Mtwara yako safi isipokuwa kwenye afya. Mheshimiwa Ummy Mwalimu namwaminia sana dada yangu, aje atuboreshee afya Mtwara. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)