Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote na mimi napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kusimama hapa na kuendelea kuchangia kupitia Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote katika hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasema yale ambayo nakusudia kusema kupitia Wizara hii, naomba nieleze kwamba mimi ni Mjumbe katika Kamati hii. Nachofahamu mimi ni kwamba tumekuwa tukifanya kazi kupitia Kamati mbalimbali, naamini tunakuwa na Mwenyekiti wa Kamati ambaye anamwakilisha Mheshimiwa Spika lakini kunakuwa na Wajumbe kwenye Kamati zile mbalimbali ambapo tunakuwa tunawawakilisha Waheshimiwa Wabunge wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kupitia maneno ya utangulizi ambayo nimeyasema, naomba nieleze masikitiko yangu. Sisi kupitia Kamati yetu tumekuwa tukijadili mambo mengi mbalimbali na kuweka maazimio tukiwa tunaamini kwamba tunapoleta kwenye kikao hiki cha Bunge basi yanapata baraka, pengine kunatolewa ushauri kwenye maazimio hayo ili Serikali ifanye utekelezaji. Kinachoshangaza tumekuwa tukijadili mambo mengi, tunafanya maazimio lakini utekelezaji unakuwa wa kusuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye ule ukurasa wa 18 tumetoa maoni mbalimbali ya Kamati. Naomba niseme machache kadri Mwenyezi Mungu atakavyonijalia. Jambo la kwanza ninalolisema ni kuhusiana na suala la kutenga pesa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Tumelisema sana na tumekuwa tukitolea maazimio na kuleta mbele ya Bunge lakini jambo hili limeonekana ni sugu na halitekelezeki. Pesa hazipelekwi kwa wakati na pengine zinapelekwa kwa asilimia ndogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza suala la maji, sote tunafahamu kwamba maji ndiyo uhai na maji ndiyo kila kitu. Sisi kama Kamati tunaleta mbele ya Bunge lako Tukufu ili Waheshimiwa Wabunge wenzetu watoe maoni yao na bahati nzuri Bunge limekuwa likipitisha maazimio lakini tatizo ni kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatutapeleka pesa za miradi ya maendeleo kwa wakati hatuwezi kuwasaidia wananchi wetu. Haya yote tunayoyafanya itakuwa sawasawa na hakuna kitu chochote kile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, sisi kupitia Kamati yetu tuliazimia na tulileta kwenye Bunge Tukufu, lakini kabla ya Bunge lilipelekwa kwenye Kamati ya Uongozi, nafikiri huo ndiyo utaratibu, kuhusiana na suala la kuongeza shilingi 50 katika Mfuko wa Maji. Wabunge wengi wamesema na mimi naomba niseme kwa masikitiko makubwa sana. Sielewi tatizo linakuwa wapi kwa sababu sisi tunasema kulingana na matatizo tuliyokuwa nayo kwenye maeneo yetu na tulishawishika kusema hivi tukifikiri kwamba inawezekana lakini tukija hapa inakuwa shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Waziri atakapokuja leo atuambie kwa sababu jambo hili sisi tulianza kuzungumza kwenye Kamati kwa nguvu sana, Wabunge tulisema sana. Bahati nzuri hili sio Bunge la kwanza kujadili jambo hili, kama sijasahau kuna Mabunge kama matatu tumekuja tunapitisha maazimio lakini wanapokuja kwenye Serikali wanapokwenda kwenye Kamati ya Bajeti majibu yanakuja sivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukuombe kwamba hili jambo sasa wakati umefika wa kutekelezwa. Hiki kiasi ambacho sisi kama Kamati tulipendekeza lakini kupitia Bunge pia wenzetu waliunga mkono na tulifanya maazimio, tatizo ni nini? Tunaomba tutekeleze, tutenge hizi pesa kwa ajili ya kutunisha kwenye ule Mfuko wa Maji ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu. Kama sivyo tuombe safari hii tuambiwe na Serikali njia nyingine, kama tunaona shilingi 50 haitoshi basi watuambie mbadala wake ili sisi tupitishe maazimio kwa sababu wetu wana shida ya maji. Kama mnaona hiki sio chanzo stahiki basi tuleteeni chanzo kingine ili sisi tupitishe maazimio wananchi wetu wapate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niyaseme haya na nimetanguliza kusema kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati, toka tumeingia kwenye Kamati ile katika mambo ambayo tunayazungumza ni kuona ni namna gani tunapata maji. Waheshimiwa Wabunge wenzetu sisi tunaomba hili mtuunge mkono kwa sababu tukiwa kwenye Kamati tunafanya kazi kwa niaba yenu ninyi na tunapoleta hapa tunaomba tufanye maazimio ili utekelezaji ufanyike. Sasa Waziri utakapokuja utatuambia tatizo liko wapi na kama siyo shilingi 50 basi tuambie ni nini kitakuwa chanzo ili wananchi wetu wapate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza kuyasema hayo maazimio ya Kamati ambayo tumekuwa tukiyasema na tunayaleta kwenye vikao na bahati nzuri Kamati hii mara nyingi inaleta kwenye Bunge lako mambo ambayo na wenzetu wanayakubali. Niombe tu Waziri aseme hili jambo tunalitekeleza kwa utaratibu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ya maji ni kubwa sana na mimi ni sehemu ya akina mama na nafahamu jinsi gani akina mama wenzangu wanapata shida katika suala la maji. Tunayo maeneo mengi katika nchi yetu yana tatizo la maji, maji ni ya shida sana. Sisi tuliopo humu ndani bila maji hata hizi suti zisingekuwepo, tusingependeza; hata mitandio tunayoivaa isingeng’aa bila maji lakini hata kuoga nako kunahitaji maji, kama hakuna maji ni mtihani mkubwa sana, hili ni jambo kubwa sana. Tuombe Waziri atakapokuja aseme neno kupitia Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)