Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuweza kusimama na kutoa mchango wangu katika bajeti hii muhimu ambayo ni bajeti ya maji, bajeti ambayo kwa kweli ndiyo uhai wa Taifa letu. Kwa kweli maji ni uhai na bila maji hakuna chochote ambacho kinaweza kufanyika ikiwemo hata masuala ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuleta salam za wananchi ninaowawakilisha ambao ni wanawake wa Tanzania walionipitisha kwa kura zao zote za kishindo tena kura zote za ndiyo. Wamenileta nilete salamu; wale wananchi wanaotoka katika maeneo yaliyopata maji kwa asilimia 64 wanaishukuru Serikali kwa kazi njema waliyoifanya ya kujenga miundombinu. Hao ni wale wa vijijini wamenituma nije niishukuru Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naleta salamu za wananchi wanaoishi maeneo ya mjini na hasa katika Makao Makuu ya Mikoa kwa kiwango cha maji kwao sasa ni asilimia 80. Wanawake hawa wamenituma nije kusema ahsante sana maana Serikali imewatendea haki. Vile vile wapo wanawake walionituma wanaoishi katika miji midogo midogo, kwa kiwango cha asilimia 64 wamepatiwa maji safi na salama na wenyewe wanasema ahsante. Hata maandiko ya dini yanasema, mtu anayeshukuru huwa anaomba tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilete salamu za wanawake wa Tanzania, kama alivyosema Mheshimiwa Kitandula, bado kuna Watanzania zaidi ya 20,000 hawapati maji. Wanawake ambao nawawakilisha ambao wamekuwa wakitembea kwa umbali mrefu, ambao wamekuwa hata hawafanyi kazi wanashinda barabarani, ambao wamekuwa hata hawapati nafasi ya kukaa na familia, kulea familia zao, kila wakati wako barabarani na wenyewe wamesema nilete kilio chao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wanaomba Serikali yao Tukufu, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Magufuli, ambapo kwa kweli ni wanawake wa Tanzania, wanawake wa nchi hii, ambao ndio walioiweka madarakani, wanaomba Serikali ithubutu, itafute fedha na hata kama ni za kukopa na kama ni kuongeza vyanzo vya mapato kwenye kodi ya mafuta, kwenye mitandao ya simu na namna yoyote ile wanavyoona inafaa, fedha zitafutwe kwa ajili ya kupeleka maji vijijini, wanawake wa Tanzania waweze kuhudumiwa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamenituma niseme wanawake wamevumilia kwa muda mrefu sana, wanapata adha kubwa sana. Kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tumewaahidi kuwatua ndoo ya maji kichwani. Hebu Serikali yetu na tunajua inaweza ikathubutu, itafute hizi fedha kwa namna inavyojua na kwa vyovyote vile miradi itekelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilete salamu za wananchi wa Mkoa wa Mara. Tunashukuru sana kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa leo, tumeona kuna miradi mingi inakwenda kutekelezwa katika Mji wa Mugumu. Katika ile Miji 29 na Mugumu ni wadau. Tunaomba tulete shukurani zetu, ahsante Serikali kwa kisikiliza kilio cha Wana-Mara, Mji wa Mugumu sasa upate maji safi na salama. Ni kwa muda mrefu wananchi wa Mji wa Mugumu wamekuwa wakitumia maji kama tope. Tunaishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunaishukuru sana Serikali inakwenda kujenga mradi wa maji Tarime ambapo kwa muda mrefu sana tumekuwa tukileta kilio. Naomba kwa niaba ya wananchi wa Tarime, Majimbo yote mawili; Tarime Mjini na Tarime Vijijini nilete shukurani zao kwa mradi unaokwenda kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naleta shukurani kwa wananchi wa Rorya na hasa wananchi wa Mji wa Shirati, Mji ambao ni mkongwe, Mji ambao umekuwepo miaka mingi. Wananchi wanazungukwa na ziwa lakini kwa muda mrefu wamekuwa hawapati maji. Kwa awamu hii sasa naona Serikali inakwenda kuwatendea haki. Kwa kweli kipekee nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wako, tumeona ambavyo mmekuwa mkifuatilia katika Mkoa wetu kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Mara wanapata maji kwa sababu ni haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara unazungukwa na Ziwa Victoria, Mto Mara, Mto Suguti na Mto Simiyu, lakini kiwango cha upatikanaji wa maji Mkoa wa Mara kwa vijijini ni kwa kiwango cha asilimia 50.8 na kwa upande wa mjini ni asilimia 60. Kwa hiyo, bado naona kwa kweli hali ni mbaya. Ni imani yangu na ni imani ya Wabunge wa Mkoa wa Mara na wananchi wa Mkoa wa Mara na hasa wanawake, miradi hii ikienda kutekelezwa tena kwa wakati itaongeza kiwango kikubwa cha maji na wanawake wa Mkoa huu wataachana na adha hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie mradi wa Mgango-Kyabakali - Butiama mradi ambao nimeusikiliza kwa muda mrefu sana, tangu Mbunge akiwa Marehemu Dkt. Magoti, Mwenyezi Mungu amjaalie. Akaondoka, akaja Balozi Ndobo, ameupigia kelele katika Bunge ameondoka; amekuja Mheshimiwa Mkono, vipindi vyote viwili ameupigia kelele, hakuna kilichofanyika; amekuja Profesa Muhongo; nami tangu nimeingia Bunge hili, Awamu ya Kwanza nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Maji, tumeupigia kelele, kila jibu tunalopewa, mradi utajengwa kupitia BADEA, mradi utajengwa kupitia Saudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013, Serikali ya Tanzania ilisaini mkataba na BADEA, ilisaini mkataba na Saudia na tukakubaliana kwamba ifikapo 2015 mradi utakamilika. Nimefurahishwa kwenye kitabu hiki nimeona mradi unaendelea na mipango nimeiona ni mizuri na ninaona mambo ni mazuri. Naomba Mheshimiwa Mbarawa ambaye umekuwa ukiniambia hata huko nje na Mheshimiwa Muhongo hata juzi mlikaa naye, hebu wewe tuambie wananchi wa Mgango na Butiama wanapata maji au hawapati? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi unaanza lini? Kwa sababu kusema kweli nimepitia vitabu vya hotuba nyingi, kila wakati inazungumzwa BADEA lakini mradi hauanzi. Mheshimiwa Waziri alipokuja na Mheshimiwa Rais alituambia mradi tunakwenda kutangaza tenda na siyo muda mrefu mradi utaanza. Leo tunakwenda kumaliza mwaka, napenda leo tusikilize kauli yake, atakapokuja kuhitimisha hii hoja, wananchi wa Mgango wanamsubiri, wananchi wa Butiama nyumbani kwa Baba wa Taifa wanamsubiri, akina Mzee Msuguri waliotumikia nchi kwa uaminifu na weledi mkubwa wakapumzika, wanahaingaika na maji. Jamani hamwoni aibu ndugu zangu tupige kelele kila siku? Hebu Mheshimiwa Waziri tuambieni mkakati ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoshituka hapa, naona huu mradi kwa kiwango kikubwa unategemea fedha za nje, BADEA na Saudia, nafikiri ndiyo maana hautekelezeki. Leo Mheshimiwa Mbarawa nakupongeza kwa sababu umeweka fedha nyingi zaidi ya shilingi bilioni nane kwa fedha za ndani. Nitoe ushauri kwako, nami najua ni Waziri msikivu ambaye umekuwa ukitusikiliza Wabunge na umesikiliza Watanzania wote; hebu hizi shilingi bilioni nane, ni fedha nyingi, mradi basi uanze hata wananchi wawe na matumaini ili Saudia na hao BADEA watakapokuja, watukute tuko barabarani. Kusema kweli tumeshaongea kule maneno yote yamekwisha. Kila wakati, wananchi wanapoteza imani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mheshimiwa Waziri mwenyewe alipokuja Butiama siku ile na Mheshimiwa Rais alipoelezea huu mradi kama alikuwa anafuatilia, wananchi walinyamaza kimya kwa sababu viongozi wengi walishawaambia hivyo. Alianza Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa aliwaambia hivyo, hakuna kitu; akaja yule Mheshimiwa Profesa Mwandosya, hakuna kitu; akaja Mheshimiwa Profesa Maghembe, tena yeye alikwenda kabisa mpaka kwenye chanzo na tuliongozana naye, hakuna kitu; amekuja juzi Mheshimiwa Engineer Lwenge hakuna kitu. Kwa hiyo, hata yeye alipokuwa akiwaambia siku ile mbele ya Mheshimiwa Rais, walikuwa wanaona hakuna kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu leo Mheshimiwa Waziri toa neno la matumaini kwa wananchi wa Wilaya ya Butiama, nyumbani kwa Baba wa Taifa, kuliko na kaburi, tusiendelee kuomba maji hapa hata kwa ajili ya kumiminia lile kaburi lake kumwagilia maua Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie upatikanaji wa fedha. Mwaka 2018 Serikali ilitenga fedha nyingi sana, lakini kwa mujibu wa Bajeti hii fedha hazikutoka zote. Nami naungana na wenzangu kwamba fedha sasa zitole. Lipo tatizo kubwa ambalo naliona, hawa Wakandarasi ambao wanawazungumza wenzangu, kwa kweli baadhi ya maeneo Wakandarasi ni wa ovyo sana. Hawana uwezo, wengine sio waaminifu, wengine wamefikia hatua wanakimbia miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fanyeni tathmini, hivi tunao Mainjinia wa miradi ya maji? Kwa sababu Tanzania naona tunazalisha Mainjinia nchini na wengi hawana kazi wako majumbani, hivi kweli…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri; na Waziri amekusikia.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)