Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kama Bunge, nafikiri hatuwi wakali vya kutosha. Nadhani mnakumbuka miaka mitatu mfululizo Wizara hii imekuwa ikitengewa pesa kidogo sana, asilimia 18, 19. Bajeti iliyopita tumetenga shilingi bilioni 700 wamepata shilingi bilioni 300, hivi hizi zilizobaki zinafidiwa lini? Leo anakuja tena kuomba shilingi bilioni 600. Lazima Bunge tutimize wajibu wetu wa kuibana Serikali, unless otherwise tutakuwa tunamshambulia Mheshimiwa Prof. Mbarawa wakati Serikali haitimizi wajibu wake wa kupeleka pesa za kutosha katika Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji hayana mbadala, umeme ukikatika leo, unaweza ukawasha kibatari, lakini ukikosa maji huwezi ukatumia maziwa kuoga, huo ndiyo ukweli. Huwezi ukatumia maziwa kunywa, kiu ya maji na kiu ya maziwa ni vitu viwili tofauti. Operesheni hospitalini zinakwama kwa sababu maji hakuna na ukiuliza sababu ni nini, Serikali haipeleki fedha za kutosha katika Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutakuja tutawasulubu hawa Mawaziri lakini pesa haziendi, Bunge sasa tutimize wajibu wetu, tuwe wakali, tuhakikishe pesa zinaenda na hiyo dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani iwe kweli. Sisi tunaotoka majimbo ya mikoani, tunajua akina mama wana- suffer kiasi gani kwa kukosa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ninapozungumzia Jimbo la Bunda Mjini, shame. Kuna mradi wa maji pale una miaka kumi na moja haujakamilika yaani mradi wa maji na mwanangu Brighton wamepishana miaka mitatu. Mradi una miaka kumi na moja haujakamilika, Brighton yuko form one ana miaka kumi na nne, ni aibu. Kila siku unakuja kuzungumza kitu hicho hicho, ukiuliza tanki, chujio, chujio gani miaka kumi na moja inashindwa kukamilika watu wapate maji safi na salama? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni aibu, tunatesa wanawake, tunatesa akina mama vijijini huko. Wanatembea umbali mrefu wanakosa maji safi na salama. Mheshimiwa Waziri umeenda, naomba sasa usifike mwaka wa kumi na mbili, wananchi wa Bunda wamechoka kupata maji machafu. Hatuna mbadala, hatuwezi kunywa maziwa wakati tuna kiu ya maji, hatuwezi kuoga maziwa wakati tunataka kuoga maji, please. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mradi mwingine kwenye Kijiji cha Chakung’ombe, Mamlaka ya Mji wa Bunda ni Grade C haipati ruzuku Serikalini, kuna mradi wa shilingi milioni 800 umekamilika. Hata hivyo, kwa sababu Serikali haiwapi pesa mradi umeshindwa kujiendesha, umefungwa na gharama za maji zimepanda, kila siku wananchi wanalalamika. Haya mmeshindwa kukamilisha miradi iwezesheni basi Mamlaka hii iweze kutimiza majukumu yake. Gari haina, hamuipelekei ruzuku, mnategemea nini? Tunawapa stress tu watumishi, stress ya kuongezewa mishahara wanayo sasa wana-stress ya kupelekewa vitendea kazi ili watimize majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawaombeni sana Serikali hebu tutimize wajibu wetu na sisi Wabunge tutatimiza wajibu wetu kuisimamia hiyo miradi iwe na tija kwa sababu tunahitaji kumtua mwanamke ndoo kichwani. Tunamtuaje ndoo mwanamke kichwani kama hatupeleki pesa za kutosha? Nawaomba sana Halmashauri yangu ya Mji, Mamlaka ile ya Maji ipewe ruzuku iweze kutimiza majukumu yake, watu wana morali lakini Serikali haipeleki hela, please.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)