Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza, niwapongeze Maprofesa wawili, Profesa Katibu, Waziri na Naibu wake Mheshimiwa Aweso.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui nianze wapi kwa sababu kuna vitu vingine niliwaza wakati hawa watu wameteuliwa, nikamwona Profesa Kitila, Mheshimiwa Profesa Mbarawa na Mheshimiwa Aweso wote wajanja. Kwa lugha ya kilaini kabisa na ya kitaalam na ya watu wale waliosoma wanasema, is software siyo hardware. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuja kutazama mambo yanavyokwenda, hivi kweli kwenye Wizara ya Maji ambako kuna wataalam leo wanapotuambia kwamba kufika Aprili katika nchi yetu kuna watu asilimia 64.08 wamepata maji vijijini, kweli? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Uongo mtupu.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lugha nyingine maana yake ni kwamba katika vijiji 1,000, at least vijiji 650 vina maji safi na salama na vijiji 350 ndiyo havina maji safi na salama. Kwa hao watu ambao tuko nao hapo ofisini kwa nini tunakariri vitu ambavyo havipo? Hivi Wabunge walioko hapa sasa wakisimama leo kila mtu aseme kijijini kwake kuna nini, kuna haja hiyo kweli jamani? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Hakuna maji.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunapewa takwimu ambazo hazipo? Kwa hiyo, wakati fulani vitu vingine vinachanganya kidogo. Kwa nini watu ambao tunawaamini wanaotumia kompyuta siyo maneno ya zamani, kompyuta halafu tunapewa takwimu siyo sahihi? Leo REA wanaweza kukuambia Bunda kuna vijiji 15 havina umeme na vijiji 20 vina umeme. Leo maji wanaweza kutuambia kila mkoa, wilaya, halmashauri, Jimbo la Mbunge lina vijiji vingapi vina maji, takwimu ikaja hapa. Jamani nyie bado vijana tupeni maji hakuna lugha nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema wazi hapa, katika kitabu hiki kuna changamoto zimetolewa. Changamoto ya kwanza nzito sana iliyotolewa ni ukosefu wa fedha za kutekeleza miradi ya maji, ndiyo iko humu jamani. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli amepita kila mkoa anawaambia viongozi sisi sometimes hatusaidii matatizo ya wananchi. Sasa leo Wabunge tunasema tunataka kusaidia mambo ya maji yaende, shida iko wapi sasa? Tunataka maji sasa yaende, tunataka aidha fedha shilingi 50 inatoka wapi lakini Kamati ya bajeti ikae ituletee, kwamba jamani eeh ili twende huko fedha ni hii hapa, nchi yetu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nani aliyechagua watu wachafu wakae vijijini halafu watu wasafi wakae mjini? Watu wanasema watu wamesongamana sana mjini, nani anayekaa kwenye uchafu huko vijijini, sisi wasafi tuko huku ndani. Mimi kijijini kwangu dampo ambalo ng’ombe na mbuzi wanakunywa maji ndiyo binadamu naye anakunywa yaani kila kitu kinakunywa mle ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki ni kipindi cha kuamua tu kwamba tunataka kusaidia nchi yetu iende, tupeni maji, tutafutie fedha. Mmetuletea wenyewe hapa, mmesema kikwazo ni fedha na sisi Wabunge tunasema fedha iko hapa, sasa shida iko wapi?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi mnafanya kazi nzuri lakini ndiyo hivyo sasa mmesema matatizo ni haya na sisi tunataka kuyasema. Mheshimiwa Waziri alipokuja Mheshimiwa Rais tarehe 09/9/2018, alipofika pale Nyamswa alikusimamisha Mheshimiwa Prof. Mbarawa kukuambia matatizo ya Jimbo la Bunda na mimi nilimwambia Mheshimiwa Rais matatizo yaliyopo na bahati nzuri nishukuru Wizara yako imetuma wataalam, wametembelea vijiji 30, wameleta mchanganuo lakini toka asubuhi nikasema labda miwani sina, nimenunua miwani nimetazama humu ndani sikuona hata kitu kimoja. Mheshimiwa Rais kasema, Waziri maliza matatizo, Waziri katuma wataalam wakaenda kufanya tathmini, wataalam wamekuja sioni Jimbo la Bunda hapa, sioni Bunda DC kuna nini kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwamba wakati fulani labda mtakuwa mmesahau lakini najua mtalikumbuka mtaniwekea hivyo vijiji ambavyo vina Kata za Unyali, Bungeta, Mihingo, Kitare, Salama, Nyamswa na ya Nyamang’uta. Wataalam walitembelea kote huko, nadhani mtaniambia kuna kitu gani kimetembea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza vizuri na naendelea kuzungumza vizuri kwamba nyie ni software, haiwezekana tukakariri gharama kubwa za kuendesha maji, gharama ni kubwa kuliko kawaida, kubwa sana. Leo mradi mmoja shilingi bilioni 20, shilingi bilioni 3, shilingi bilioni 4, tumefanya majaribio ya kujenga Hospitali za Wilaya na vituo vya afya kwa kutumia Force Account, gharama ni ndogo sana. Ninyi kwa nini msikae mkasema tufanye kama Malawi, tutandaze bomba kutoka Ziwa Victoria lipite barabarani tu, kila kituo, kila kijiji mnaweka toleo, barabarani tu. Vijiji vingine vilivyoko huko porini vitakuja kuchota maji pale kwa sababu vitakuwa na uhakika wa maji. Bomba lipite liende, inakuwa maajabu leo Bunda kilometa 15 kwenda kilometa 15 nyingine kutoka Ziwani hakuna maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnafanya wananchi wanakuwa watu wa ajabu. Hivi kama tunasema tunahurumia wananchi hawa, wanaendaje kupiga kura wakati wote hawana maji? Saa 12 akina mama ndiyo wanapiga kura, hawaendi kupiga kura maji hayapo, tupeni maji tuache

maneno jamani, tupeni maji. Tumechoka tupeni maji, haiwezekani. Mheshimiwa Aweso bado kijana mdogo unaweza ukatoa maji, tupeni maji. Kwa hiyo, nisema gharama za uendeshaji wa maji ni kubwa mno, tutumie akili tutengeneze namna ya kuwa na gharama ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimewaambia pale Bunda, kama mnaweza kunipa shilingi bilioni 10, nipeni mimi nipeleke maji nakotaka. Wataalam wa MUWASA wako pale, tutengeneze gharama. Tumeshatengeneza bomba, kiasi gani, wachimbaji ni wanakijiji wenyewe, ufundi unakuwepo tunaweka maji, kila mahali patakuwa na maji. Kama hiyo RUWASA hatuwezi kuiwekea mazingira mazuri itakuwa na hela kutokea wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo liko hapa, haiwezekani tukasema tunatafuta fedha, haiwezekani Mawaziri mkahangaika, haiwezekani Mheshimiwa Rais akahangaika mpaka anaomba misaada ya fedha kutoka nje, halafu watu wanaitwa sijui watumiaji maji, MUWASA, DUWASA, wanakula fedha. Tumeona kwenye ripoti ya CAG maeneo yote haya ya maji hasa ya majiji wamekula fedha. Tusisubiri ripoti kwamba PAC na LAAC wafanye kazi, hapana. Tukiona kuna chokochoko mahali, watu wanakula fedha za maji wakamateni waondoeni kwenye nafasi, mnasubiri Kamati za nini? Hatuwezi kukusanya fedha halafu watu wengine wanakula. Kwa hiyo, naomba tuangalie tunakwendaje kwenye suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili sasa nitaongea kwa upole, polepole tu msikie. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ni karne sijui ya ngapi, sijui ni 21 au 22 sielewi.

MBUNGE FULANI: Hiyo ndiyo polepole?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Hiyo ndiyo polepole.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekanaje leo eti mtu anakuja pale hodi, hodi, nani? Mimi mpima mita, jamani! Anakuja kuangalia bili apelike ofisini. Kwa nini tusiwekewe mita mtu alipie maji kadri anavyotumia, kuna shida gani? Hili nalo mpaka Mheshimiwa Rais aje aseme ndiyo mfanye? Kwa nini watu wanatumia bill kwa ajili ya kula fedha? Kwa nini wanaletea watu bili kwa maji ambayo hawajatumia? Kwa nini tusitumie mita kila mtu anakunywa analipa, shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie hili tena polepole ili muelewe vizuri. Mheshimiwa Waziri, Naibu Mheshimiwa Aweso, Katibu Mkuu katika jambo ambalo hatuwezi kufanya mchezo wa kuigiza au wa kupiga siasa ni suala la maji, watu wana hali mbaya sana. Wakati fulani naenda kijijini nasema huu Ubunge wa nini sasa, si bora nitoke tu. (Makofi)

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri ni vizuri mkafanya kazi ya kutusaidia kupata maji.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Muda wake umeisha, Mheshimiwa Getere muda wako umemalizika.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)