Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweke mawazo yangu katika Wizara hii ya Maji lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kutupa nafasi hii maana ni kwa neema yake tu tutimize wajibu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu na Katibu Mkuu na timu yake kwa jinsi ambavyo wanachapa kazi hongera sana. Nafahamu wanapambana sana, Wizara hii kila mmoja anatamani atendewe haki kwenye eneo lake na kila siku wako site. Pia niwashukuru wanatutembelea huko majimboni, Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Babati, akafika Imbilili kwenye mradi ambao umekuwa ukisumbua muda mrefu sana, lakini naona sasa kuna mwanga na mambo yanaendelea. Niwapongeze mno kwa kuwa wanapambana usiku na mchana ili wananchi wa Tanzania wapate maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Mradi huu wa Maji katika Mji wa Mtwara na Babati, ukurasa wa 90 kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri. Naomba tu watusaidie wawe wakweli, watuambie wapi wamekwama kwa sababu wameandika Mtaalam Mshauri anaendelea na usanifu wa kina wa mradi na ujenzi wa mradi utaanza baada ya kukamilika kwa usanifu huo. Sasa naomba nifahamu usanifu unafanyikia wapi Dodoma, Dar es Salaam au Babati na Mtwara. Kama ni Babati na Mtwara nafikiri warudi kwa wataalam wao wawaambie tu ukweli, huyu mtu wanayemsema Mtaalam Mshauri amefika, hayuko site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachofahamu Mradi huu wa KfW kati ya Serikali yetu na wenzetu wa Ujerumani ni mradi wa mwaka wa kumi na moja sasa ambao ungetusaidia kilomita 45 coverage pale tukapata maji, lakini ukatusaidia kujenga vyoo katika maeneo ya stand, masoko na maeneo mengine katika shule zetu. Maeneo mengine wameshatekeleza, Mheshimiwa Makamu wa Rais alikuja Babati tukaomba pia na hili, tukaomba kwa Mheshimiwa Waziri aliyepita na aliyepo sasa na Naibu Waziri wakatuambia tatizo Wizara ya Fedha ndio hawajasaini huu mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tu nisikitike kuwa Mheshimiwa Waziri leo anatuambia Mtaalam Mshauri yupo site Babati huko akiendelea na usanifu, nafikiri hizi taarifa zao waziangalie upya kwa nia njema tu, kwa sababu ni mradi wa miaka kumi na moja sasa. Sasa ni vizuri wakatuambia kwa sababu utatusaidia sana pale Babati Mjini na sijapoteza imani na Mheshimiwa Waziri, lakini natamani tuwe wakweli, kama tumekwama mahali tuambizane, hilo tu. Kwa huu mradi wakate mzizi wa fitina, wasituambie mkataba haujasainiwa, Mtaalam Mshauri yuko site, wakati hayuko site, naomba kwa hili watuambie ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niwapongeze walifika katika Kaya ya Sigino upande wa Imbilili. Usiposhukuru kwa kidogo pia maana yake utakosa kikubwa, wametulipia certificate za maji za Mradi wa Malangi na Mradi wa Haraa na unaendelea vizuri. Pia nimewapatia certificate ya Imbilili ambako wamefika, kwa kweli niwaombe wanafahamu ni viongozi wangapi wamefika pale, sitaki kuwataja, nawaomba watulipe hizo fedha za certificate ya Imbilili milioni mia mbili kama na arobaini ili ule mradi uende kwa sababu mradi ule ume-expire mara tatu, 2017 yule mkandarasi aliyeko site mkataba wake uli-expire. Mwaka 2018 tukaongezea tena ule mkataba uka-expire na mwaka 2019 ume-expire tena, lakini sasa anaendelea site kwa sababu fedha hazitoki na maeneo mengine pia anafanya miradi mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina tatizo na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, ninachoomba katika zile bilioni 40 walizosema zimesalia basi watulipe na ule mradi kwa sababu zifuatazo:-

Kwanza, ndio kijiji pekee kati ya vijiji vinne kwenye kata nzima ambako mradi ndio umeanza kidogo. Kwenye Kata ya Sigino Mheshimiwa Waziri wa Maji alifika baba yangu ambaye sasa yuko kwenye Wizara ya Ujenzi, akafika pale, akaongea na wale wananchi, akawaambia Kata ya Sigino tunawapatia maji umekuwa ni wimbo wa miaka yote. Naibu Waziri amefika ameona kata nzima ule mradi haujafika, naombeni Kata ya Sigino ndio mradi wetu wa kwanza Halmashauri ya Mji wa Babati hatuna mradi mwingine ni wa Kata ya Sigino, Kijiji cha Singu, Kijiji cha Sigino, Dagailoi na hicho cha Imbilili milioni 230 wakitulipa sisi hatuna ugomvi na wao, watupatie hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasahau naomba nishukuru sana pia kwa kitendo walichotufanyia watu wa Babati na Watanzania kwa kipindi hiki, wamefuta service charge kwenye bili zetu za maji, bili za mwezi wa Nne zimekuja, wananchi wa Babati walikuwa wanalia kuhusu Sh.2,500 kwa kila bili, kwa kweli nawapongeza na hii kauli ni ya wananchi wa Babati, wameondoa hiyo service charge, hongera sana. Sasa wanapopiga hatua mbele Mheshimiwa Waziri ni vizuri wakatuletea sasa prepaid meters, hizo wakitupatia kwanza zitatusaidia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji hayatapotea pia zile bili za maji ambazo zilikuwa hazikusanywi zitakusanyika sasa kirahisi, nawaomba wa-roll out mapema Waheshimiwa Mawaziri wetu, wameshafuta hilo wananchi wa Babati wamefurahi sana kwa sababu ilikuwa kila mkutano nikienda wanasema mama tunakuomba service charge iondolewe, wameiondoa hatuna cha kuwalipa tunawashukuru, lakini sasa watuletee prepaid meters itasaidia sana maji yasipotee na watu walipe bili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine katika Mji wetu wa Babati bili za maji imependekezwa na EWURA na mchakato kutoka chini kwamba ipandishwe kutoka unit moja kwa Sh.1,190 hadi Sh.2,000. Hivi imagine ongezeko la Sh.1000 niwaombe sana watu wa EWURA wasije wakathubutu kupokea hayo maombi ya kupandisha bili za maji katika Mji wa Babati kwa sababu hata hizo za sasa tu wanaona watumiaji wa maji sio wengi ni kwa sababu pia hizi bili ni kubwa kwa units tano mpaka 10 haitoshi kwa matumizi ya nyumbani, lakini units 10 na kuendelea wakaongeza kutoka Sh.1,100 mpaka Sh.2,000 Mtanzania wa Babati hawezi kumudu hiyo bili. Kwa hiyo chondechonde watu wa EWURA wasije na watu wa maji wakapandisha hizo bili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ni suala la usimamizi wa maji. Mheshimiwa Waziri amesema ana upungufu wa watumishi 3000, hao watumishi 3000 katika Wizara yake ambapo alitakiwa awe na watumishi 10,000, sasa una 6,000 lakini hiyo inashuka mpaka kwenye halmashauri zetu. Mimi nishauri kama hawa watumishi ni pungufu fedha za maji wanazotutengea waache mamlaka zisimamie kwa sababu hao ma-engineer wa maji wameshindwa kusimamia miradi ya maji katika halmashauri zetu. Utakuta usanifu mbovu, maeneo ambako mabomba ya chuma yanatakiwa yawepo kwenye makorongo wanaweka ya plastiki, tatizo ni kubwa kwenye mji wetu sisi miradi mingi ya halmashauri tumekuwa tukikabidhi BAWASA kwa sababu mradi unatekelezwa na halmashauri ukipelekwa kwa wananchi wau-test haufai hata kidogo. Mradi wa Managhat jana tumetoka kulipa, juzi kwenye kikao cha Kamati ya Fedha imebidi tutoe milioni 10 kwa ajili ya ku-repair ule Mradi wa Managa kukabidhi kwa BAWASA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mradi wa Nakwa milioni 800, umechakachuliwa ilibidi tulipe zaidi ya milioni 26 ndio BAWASA waupokee, kwa nini tupoteze fedha. Nashauri hivi, ni vizuri fedha wakatuletea halmashauri lakini wataalamu Experties wakasimamia watu wa BAWASA maana halmashauri zetu wameshindwa kusimamia hii miradi, inasababisha miradi inakuwa mibovu, kunakuwa na uchakachuzi mwingi, mwisho wa siku wananchi wanakosa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo niwatakie kila la heri, wanipatie fedha za Kata ya Sigino, certificate zetu watulipe, nawashukuru kwa kufuta service charge, tupo pamoja. Naunga mkono hoja. (Makofi)