Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kwanza nimshukuru mwenyezi mungu, kwa kuendelea kutupa afya njema na kutufikisha katika siku ya leo. Nitumie nafasi hii pia kuishukuru sana Wizara ya Maji kwa jinsi ambavyo wameshughulika na matatizo ya Watanzania. Mnyonge mnyongeni lakini ukweli Wizara ya Maji chini ya uongozi wa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wao wanajitahidi sana kuhangaika na miradi ya maji pamoja na changamoto nyingi ambazo wamekutana nayo katika miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Bunge hili likakumbuka kwamba matatizo mengi yaliyoko Wizara ya Maji, hawa waliopo sasa wameyarithi, matatizo haya yalikuwepo huko nyuma, lakini Wizara kwa kweli wanajitahidi kuhakikisha kwamba tatizo la ubadhirifu wa miradi ya maji linaondoka. Tunawapongeza, kwa kweli si rahisi sana kukubali kwa sababu kule Jimboni kwangu kuna tatizo lakini kazi wanafanya tunawatia moyo waendelee kufanya kazi vizuri. Tunampongeza sana Profesa kwa jinsi ambavyo anawasaidia kutimiza majukumu yao na uzuri ni kwamba hawakai ofisini kila siku tunawaona huko na huko wakikimbia kuangalia matatizo ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu kama Bunge ni kuwasaidia Wizara kutafuta fedha na kuzipata kwa ajili ya kutekeleza miradi yetu. Kama Bunge hili hatutashauri namna ya kupata fedha, tutakuwa tunalalamika habari ya maji lakini hatutatatua tatizo, ndiyo maana naungana na walioomba kwamba tunawasaidia Wizara wafanye kila namna katika chanzo chochote wapate shilingi hamsini kwa ajili ya kuboresha Mfuko wa Maji. Hii ni faida kwao na lawama hizi za Wabunge za matatizo ya maji wataepukana nazo, kama watakubali ushauri wetu kwamba tukubali kutafuta chanzo chochote, sio lazima kwenye mafuta, mahali popote watakapoona inafaa tupate fedha kwa ajili ya kuboresha Mfuko wa Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kila Mbunge akisimama hapa anapongeza Wizara ya Nishati lakini ni kwa sababu wao wamepata chanzo cha uhakika cha fedha, ndiyo maana tunaona REA inapeleka umeme vijijini na watu wote wanapongeza. Kwa nini Wizara hii nao wasipate wivu wa kutafuta namna ya kupata hiyo shilingi hamsini ili tuweze kupata fedha kwa ajili ya miradi hii ya maji. Kwa hiyo, naomba ile shilingi hamsini waone kwamba ni nia njema ambayo inaweza ikatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili niwashukuru kwa kutoa kibali cha miradi miwili Monduli. Mradi wa Meserani na Mradi ule wa Nanja. Nampongeza Naibu Waziri alikuja Monduli alituahidi na sasa nimepata taarifa kwamba wamepata approval kwa hiyo miradi hiyo miwili inaweza kuanza wakati wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, ukiangalia katika Wizara ya TAMISEMI wamefanikiwa sana katika miradi yao ya ujenzi wa vituo vya afya na wamefanikiwa kwasababu wametumia Force Account na kipindi hiki tunao wasomi wengi, ma-engineer wa maji walioko vijijini ambao hawana ajira. Kwa nini tusiwe na mradi wa kutumia Force Account katika miradi mingi ya maji ili kule kijijini tuokoe fedha tunazopeleka kwa Wakandarasi, fedha kidogo tunazopata tununue vifaa wataalam wetu wazalendo walioko vijijini watasimamia miradi hiyo. Kwanza utakuwa umewapa ajira, lakini vilevile umeokoa fedha nyingi ambazo zingeenda kuwa faida ya Wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule chini wananchi wanaweza wakachimba mitaro, wananchi wanaweza wakafanya kazi ndogongogo, halafu tukapata miradi mizuri kwa bei nafuu, kwa nini tusitumie mfumo huu wanaotumia TAMISEMI kujenga vituo vya afya, kutekeleza miradi ya maji kuliko kupeleka fedha bilions of money kwa Wakandarasi ambao wame-prove failure na kila siku tunasumbuana nao kwa kuchelewesha miradi. Ni kwa nini Wizara wapokee lawama hiyo, tupeleke miradi hiyo kwa wananchi, kwanza itafanya ownership, wananchi watamiliki miradi yao na tutaokoa fedha nyingi kwa sababu wananchi watafanya kazi nyingi na hawa vijana wetu wanaomaliza Vyuo Vikuu, watatoa taaluma technical katika miradi hiyo na tutaokoa fedha nyingi. Kwa hiyo naomba, Waziri walione hilo, tutafute miradi ya pilot tuanze ili tufanye namna ya kuokoa fedha zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, naomba nishauri pia katika eneo hili la maji, miradi mingi ya maji hakuna mradi ambao uko chini ya milioni 800, 700 lakini ukiangalia watu wengi wanalalamika unamaliza mradi leo, ukija kesho mradi huo hautoi maji. Mradi unakamilika leo kisima kesho hakitoi maji na kama kinatoa maji kinatoa kwa kiwango cha chini. Hivi ni taaluma gani inayofanya tathmini ya kujua hapa maji yapo na ni chanzo cha uhakika ambapo baada ya miezi miwili, mitatu mradi kukamilika, miradi haitoi maji. Kwa hiyo ni muhimu tukafanya tathmini ya miradi yote nchi nzima kufahamu ni miradi mingapi inatoa maji na mingapi haitoi, kwa sababu takwimu za wataalam kwamba asilimia 80 mjini wanapata maji si kweli, miradi mingi imekamilika lakini haitoi maji, maana yake wananchi wa maeneo hayo hawapati maji. Tufanye review ya miradi ili tuwe na takwimu sahihi ya kiwango gani cha Watanzania wanaopata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya hasa katika majimbo ya vijijini na naomba Serikali itambue kila siku naona miradi mikubwa ya wafadhili inafanyika mijini, sisi watu wa vijijini ambao uwezo wa kupata maji hata iwe mita 400 wametuweka wapi. Hii si sawa, wafadhili wanatoa fedha mijini kwa sababu wana interest, sisi ambao tuko vijijini nani mwenye interest na sisi ambao hata sisi hiyo mita 400 wanayozungumza kuchota maji, sasa tunafuata maji kilomita tano na wakati mwingine hatupati maji hayo. Kwa hiyo tutazame kwa jicho la huruma majimbo ya vijijini, hali ya wananchi wetu ni mbaya sana na ndiyo walipakodi na ndiyo watu wetu waaminifu wakati wa uchaguzi, lakini tumewaacha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukatambua kama wafadhili wanatusaidia mijini, Serikali ijielekeze kusaidia majimbo ya vijijini angalau sisi tukipata maji ndani ya kilomita moja bado ni faida, achana na hao wa mjini wanaosema mita 400, mita 400 ni ndani ya kiwanja chako sisi tunafuata kilomita 10 na bado maji yenyewe hatuyapati. Kwa hiyo, Wizara itusaidie ni kwa namna gani ambavyo tunaweza kutatua changamoto hii, kwa kweli hali ya maji katika maeneo yetu ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niombe jambo moja, nimekuwa nikisikia visima vya DDC kila siku, mimi sijawahi kupata hata kimoja, walau leo ikimpendeza Mheshimiwa Waziri wanipe hata vine, hii si sawa. Mwaka juzi niliona, mwaka jana nimeona, mwaka huu naona lakini kwangu sijaona hata kimoja na sisi tuna maeneo machache yenye maji, wanipe vijiji vizima vinne kule Mswakini kule Makuyuni, nitaondolewa kwenye tatizo la maji, lakini kila siku wanagawa DDC mimi wameniweka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alikuja Monduli akasema hatanipita nami nimesema nikisimama mahali popote, akiniambaia niombe jambo moja, wanisaidie kutatua tatizo la kero ya maji katika Jimbo la Monduli. Wakinisaidia hayo, hayo mengine naweza nikasubiri, lakini nimewaomba hili moja tu la maji, kuhakikisha tunatatua tatizo la maji katika Jimbo letu. Juzi nilikuwa na Katibu Mkuu, akasema Majimbo mawili ambayo yana kero kubwa ya maji Arusha ni Ngorongoro na Monduli, basi watuangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kitabu hiki naona tu Majimbo mengine Longido, wapi, watutaje basi na sisi ili na sisi tujisikie kuwa ni sehemu ya mafanikio ya mradi na ya Wizara yetu. Naomba kwa unyenyekevu watuangalie kwa jicho la huruma, hali ya maji kwenye Jimbo la Monduli ni mbaya sana na mabwawa mengine mengi yamepasuka, tulikuwa na mabwawa 51, leo yanayofanya kazi hayafiki kumi, tutapata wapi sisi maji? Naiomba Wizara itusaidie, kwa kweli ninaomba nione huruma yao wakati wa kuhitimisha bajeti, wanatuongezea shilingi ngapi na wanatusaidia nini visima vingapi ili kuondokana na kero ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nimekuwa nikienda sana pale Wizarani, pale Wizarani inaonekana watumishi wengi wanakaimu, kwa nini tusiwape nafasi hiyo kama wanatosha ili waweze kufanya kazi? Tusipende tu kuwalaumu, lakini pale ambapo ni stahiki zao wawape idara, wawape nafasi wanazokaimu ili waweze kufanya kazi vizuri, wanakaimu kule wilayani, wanakaimu Makao Makuu, wawathibitishe kama wanatosha ili tuweze kupima katika utumishi wao, hatuwezi kuwapima kama hatujawapa majukumu kamili ili waweze kufanya kazi zao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kabisa naomba wakati wa mwaka wa fedha unaokuja, tunatamani Wizara ituambie tatizo la maji katika maeneo mbalimbali ambayo hatuna vyanzo vya uhakika vya maji kwa nini Serikali isitengeneze utaratibu hata wa uvunaji wa maji ya mvua kwenye maeneo yale ili wananchi wetu waweze kupata maji na waondokane na tatizo la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)