Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Sonia Jumaa Magogo

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maji. Pamoja na hotuba ya Mheshimiwa Waziri kugusia baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tanga kuwemo katika miradi ambayo inaendelea kutekelezwa lakini ningeiomba Wizara iiangale miradi hii kwa jicho la tofauti. Nasema hivi kwa sababu miradi mingi ya maji Mkoani Tanga imechukua muda mrefu sana kukamilika na imezua sintofahamu kwa wananchi, hawajui ni kwa nini miradi hii imekuwa ni ya muda mrefu lakini haikamiliki na kuendelea kuacha changamoto ya maji ikiwakabili Wananchi hawa wa Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano wa mradi wa maji wa HTM; huu mradi umechukua muda mrefu sana na umesababisha tatizo kubwa sana la maji kwa wananchi wa Wilaya ya Handeni. Wilaya ya Handeni tatizo la maji limekuwa kama ni historia sasa na kila siku wanapewa ahadi juu ya huu mradi kwamba kuna mradi wa maji, kuna mradi wa maji lakini huu mradi umekuwa haukamiliki na wananchi wanaendelea kuteseka sana na maji. Hivyo, niiombe Serikali iangalie kwa jicho la tofauti ni nini kinazuia huu mradi usikamilike na wananchi wale waweze kupata maji kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga tuna vyanzo vingi vya maji na sioni ni kwa nini tunakuwa na tatizo kubwa sana la maji kiasi hiki. Hivyo Serikali iangalie vile vyanzo ambavyo tunavyo kuweza kuwasaidia wananchi hawa wa Mkoa wa Tanga kuondokana na hili tatizo la maji. Sisi sote tunafahamu umuhimu wa maji katika maisha ya mwanadamu na Mkoa wetu wa Tanga shughuli zetu nyingi sana zimetawaliwa na viwanda na kilimo, lakini tunapokuwa na uhaba wa maji tayari kwetu hili linakuwa ni tatizo kubwa sana. Huwezi kuendesha viwanda kwa ufanisi kama huna maji ya kutosha, huwezi kuendesha shughuli za kilimo kwa ufanisi kama huna maji ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna Sera ya Elimu bure ambayo inatolewa na Serikali. Hii sera ya elimu bure itakuwa haimfikii hasa mtoto wa kike vile ipasavyo kwa maana watoto hawa muda mwingi ndiyo wanatumika kwenda kusaka maji. Ule muda ambao wangeweza kuutumia kwenye masomo unakuta wanautumia kwenda kutafuta maji na katika harakati hizo za kutafuta maji ndiyo unakuta watoto wengi wanapata mimba za utotoni na maradhi mengine ambayo hayatibiki. Wakati huo huo kuna kipindi ambacho mtoto wa kike anakuwa kwenye hedhi na shule nyingi hazina maji. Unakuta mtoto ile hali inampelekea asiende shule kwa kuogopa kwamba nikienda shule nitajisitiri vipi nitakapokuwa katika hali hii. Hivyo Serikali iwasaidie watoto hawa kama tumeamua kuwapa elimu bure basi ikamilike pia, tuangalie na vichocheo ambavyo nivapelekea hii elimu iweze kuwafikia kwa ufanisi ikiwemo suala la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwenye miundombinu ya maji; miundombinu yetu ya maji haijakaa vizuri na hii inapelekea wananchi wengi kulalamikia suala la bili ambazo haziko realistic kutokana na kile ambacho wanakitumia. Mabomba mengi yanavuja na unaweza ukamwita fundi labda ukapiga simu ili upate msaada, lakini hupati ule msaada kwa wakati, hivyo kupelekea kupata bili ambayo pengine ilikuwa siyo tatizo lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hii system ambayo inanipa utata ya kwamba maji yanapovuja mbele ya mita inakuwa ni juu ya ofisi lakini inapovuja nyuma ya mita inakuwa ni juu ya mteja. Hili ni tatizo kwa sababu kama miundombinu yenu haiko sahihi ni lazima maji yatavuja. Pia tungeweza kuzuia pale mwanzo wakati yule mteja anaweka ile system yake ya maji kukawa na watu ambao wanakuaja kukagua kabla hamjamwekea maji ili kuona kama ameweka vitu vyake kwa usahihi ambapo itapelekea mwananchi huyu asipate bili zinazosababishwa na uvujaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine naomba pia Serikali iangalie umuhimu wa kutoa elimu juu ya matumizi ya vyanzo vya maji kwa wananchi. Wananchi wengi hawana uelewa juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na kupelekea vyanzo vingi kukauka na uharibifu wa vyanzo hivi vya maji. Hivyo, niiombe Serikali kuliko kuangalia zaidi kwenye kuwapa adhabu hawa wananchi waangalie zaidi kuwaelimisha kuwasababisha wawe mabalozi wazuri kwa utunzaji wa vile vyanzo vya maji ambavyo vinawazunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nizungumzie mfumo wa prepaid. Mfumo huu kama ungeweza kusisitizwa nchi nzima na ukatolewa elimu kila mtu akaufahamu vizuri ungeweza kusaidia kupunguza haya malalamiko ya bili za wateja. Hivyo, niiombe pia Serikali iangalie umuhimu wa kuhakikisha hii huduma ya prepaid inaenea nchi nzima na kila mwananchi anaelewa matumizi yake ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)