Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nakushukuru sana kupata nafasi ya kuchangia hoja hii ambayo ni muhimu sana na ni tatizo kubwa sana mpaka sasa hivi hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya. Pia nawapongeza Mkurugenzi wa Tanga-UWASA pamoja na ma- engineer wa Muheza, Eng. Bakari na Eng. Elikana ambao wanafanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba maji kwenye Jimbo la Muheza yanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, sisi Muheza tuna mradi, ukiacha mradi mkubwa lakini uko mradi ambao unatoa maji kutoka Tanga (Pongwe) na kuyaleta Mjini Muheza ili kuondoa tatizo la maji Muheza. Mradi huu ulitegemewa umalizike tangu Mei 2018 lakini mpaka sasa hivi mradi huo bado unaendelea kujengwa na uko kwenye asilimia 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa inafanyika lakini mradi huu ambao tunautegemea ulikuwa kwenye Quick- Wins ili kupunguza tatizo pale Mjini Muheza. Sasa hivi kama nilivyosema imebaki kitu kidogo sana ni asilimia 30 ili maji haya yaweze kutiririka pale Muheza ingawa haitakidhi sehemu kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ambalo limebaki ni kufumua mabomba yaliyochakaa pale Mjini Muheza na kuweka mapya. Suala hili limesitishwa kidogo ili tusubiri mradi mkubwa wa maji wa kutoka India wa Dola milioni 500. Nimeongea na Waziri na nasisitiza sana kwamba waruhusu sasa hivi ili mabomba yale yaanze kufumuliwa kwa sababu tenki ambalo lilikuwa linachelewesha limekwishatengenezwa na limekaribia kumalizika. Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu mmefika kule na mmeona kazi kubwa ambayo imefanyika ya kutoa tenki kubwa Pongwe na mabomba yameshalazwa. Nashukuru sana hivi karibuni mmetoa fedha kwa wakandarasi na sasa hivi mabomba ya chuma yanalazwa kupelekwa kwenye chanzo kikubwa cha maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi maji hayawezi kwenda kwa sababu bado hiyo sehemu ndogo ambayo imebaki ifumuliwe. Nimeona kwenye bajeti mmepanga karibu shilingi milioni 700, Mheshimiwa Waziri naomba uruhusu, wakati tunasubiri mradi mkubwa, mabomba ya Muheza Mjini yaanze kufumuliwa ili mkandarasi aanze kazi hiyo na maji yaanze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nashukuru sana kwamba tumepewa fedha kwa ajili ya maji vijijini, karibu shilingi bilioni moja na zaidi. Ipo miradi mingi sana pale ambayo imebuniwa, kwa kweli nawashukuru sana ma-engineer wa maji pale Muheza ambapo tumebuni na mmekwisharuhusu tutangaze zabuni kwa ajili ya kutafuta wakandarasi, kuangalia uwezekano wa kuanza kujenga Miradi ya Kwemdimu, Zaneti na Tongwe. Hii miradi ni maji ambayo yanachirizika kutoka milimani yaweze kusafishwa na kusambazwa kwa wananchi kule vijijini.

Kwa hiyo, nashukuru sana isipokuwa nashauri tupunguze urasimu wa kutoa vibali uliopo pale Wizarani. Baada ya kutangaza basi mruhusu moja kwa moja ili wapatikane wakandarasi na watie saini badala ya tena irudi Wizarani kuomba kibali kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ambalo nataka kuongelea ni mradi huu wa India wa Dola milioni 500. Najua Mheshimiwa Waziri unatupa taarifa, maendeleo yanavyokwenda kila mara lakini mradi huu ni muhimu sana na una-cover miji karibu 29 hapa nchini. Mradi huu ukikamilika utapunguza sana tatizo la maji hapa nchini. Pamoja na kwamba suala hili lipo kwenye mchakato lakini unachukua muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Waziri aangalie uwezekano wa kuona huu mchakato utafupishwa namna gani, umekuwa ni mrefu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba uweke jitihada sana kwenye suala hili kwa sababu watu wengi tumeliongelea kwenye majukwa ya kisiasa kwmaba mradi unakuja mpaka sasa hivi tunashindwa kueleza kwamba mradi unakuja namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne, ni kama walivyosema Kamati kuhusu tozo ya maji ya shilingi 50. Suala hili limepigiwa kelele sana, miaka mitatu sasa na Kamati imependekeza hapa kwamba tozo ya shilingi 50 inatakiwa iongezwe ili ifikie shilingi 100. Hii ni kutokana na fedha ambazo zinapatikana kwa sababu fedha ambazo zinalipa wakandarasi sasa hivi inaonekana zote zimetoka kwenye Mfuko wa Maji wa Taifa. Mfuko huu umesaidia sana kuonekana kwamba Wizara haina fedha. Kutokana na Mfuko huu kuwa ring fenced, imesaidia sana kulipa malipo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini fedha hizi hazitoshi, wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri umetembelea miradi mbalimbali hapa nchini na umeona kabisa wakandarasi wengine wamesimama kutokana na kutokulipwa fedha. Kwa hiyo, ni vizuri kilio cha Wabunge ambacho wengi tangu miaka hiyo tumekuwa tunasema tuongeze shilingi 50 ili tozo hii ya mafuta iweze kuwa shilingi 100 ili iweze kusaidia kidogo kupunguza tatizo kubwa la maji. Naamini kabisa kwamba tutakapoongeza fedha hizo basi inaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa kuweza kufikia lengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni Uanzishwaji wa Mamlaka ya Maji Vijijini. Wazo hili ni zuri sana na tunategemea linaweza likasaidia sana kupunguza tatizo la maji kwenye vijiji vyetu. Hata hivyo, ni vizuri tuangalie tumeipangia kiasi gani na tutapata wapi fedha za kuanzisha Mamlaka hii kwa ajili ya kutatua matatizo ya maji vijijini? Tumeanzisha TARURA lakini fedha ambazo zinakwenda TARURA ni ndogo sana. Kwa hiyo, ni vizuri sana kuangalia uwezekano wa kupeleka fedha ili Mamlaka hii itakapoanza basi ianze kwa bidii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)