Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Elimu. Sekta ya Elimu kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu, Kitaifa inatakiwa kuwa na mifumo mitatu, yaani formal, non-formal and informal education.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera zetu za elimu, zinadhihirisha hilo kwani watoto wetu huondolewa mikononi mwa wazazi yaani hasa mama zao na kupelekwa shuleni chini ya walezi wengine yaani walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu ndiyo walezi wa Taifa, hoja kwa kielelezo humu ndani Bungeni hata Serikalini zaidi ya theluthi moja ni Walimu, nitatoa mfano, Serikalini na humu Bungeni, Mwalimu John Joseph Pombe Magufuli, Mama Janet Magufuli, Mwalimu Jenista Mhagama, Mwalimu Kilagi, Mwalimu Kabudi, Mwalimu Mwakyembe, Mwalimu Joyce Ndalichako, Mwalimu Susan Lyimo, Mwalimu Salma Kikwete, Mwalimu Profesa Mbarawa, Mwalimu Philipo Mpango, Mwalimu Grace Tendega, Mwalimu Shamsi Vuai Nahodha. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mwalimu Haonga.

MHE. JAMES F. MBATIA: Ndiyo na Mwalimu Haonga. Nikitaja kwa uchache, hapa ni Mwalimu, Mwalimu, Mwalimu. Nenda kwa Makatibu Wakuu, Katibu Mkuu Akwilapo Mwalimu, dada yangu Semakafu Mwalimu, wote ni Walimu, Walimu. Mama aliye na mtoto mchanga asipopata mahitaji msingi hawezi kumnyonyesha ipasavyo mwanaye, rai yangu, tumuenzi Baba wa Taifa hili, kwa kuwapatia Walimu wetu upendeleo wa makusudi katika mishahara yao na stahiki zao. Msemo wa hakuna mwingine kama mama, kwa heshima tuseme Tanzania hakuna mwingine kama Mwalimu, kwani sisi sote humu ndani ni zao la Walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu, Mwalimu John Joseph Pombe Magufuli, rai yangu kwake, awe mstari wa mbele kesho Mei Mosi, awe wa kwanza kuongeza mishahara ya Walimu na stahili zao kwa upendeleo wa makusudi, kwa kuwa Walimu ndiyo sekta kuu ya uzalishaji katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulinde uhuru na heshima ya Taifa letu, yaani Tanzania kwa kuwapatia walezi wetu, Walimu mishahara na stahiki zao zenye kukuza na kuhifadhi utu wao ili waweze kuwa na furaha ya ndani, wawe na uwezo na utu na rai ya kufundisha. Tutoke kule kwenye asilimia 60 ya Walimu sasa hivi ambao hawataki kufundisha warudi kwenye ari yao, warudi kwenye taaluma yao waweze kufundisha na kulilea Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza na hilo kwa sababu naiangalia elimu ya Tanzania kwa miaka 25 ijayo, miaka 30 ijayo. Ukisoma hotuba ya Kambi ya Upinzani, nimeisoma yote kwa makini ifikapo mwaka 2036 tutakuwa na Watanzania zaidi ya milioni 90. Mwaka 2045 tutakuwa na Watanzania zaidi ya milioni 120, je critical mass ya Watanzania, critical thinkers ya Watanzania watakuwa kwenye hali gani kama hatuondoi itikadi zetu, hatuondoi tofauti zetu tukajikita kwenye kuiangalia Tanzania miaka 30, miaka 50 ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bora, sawa na shirikishi kwa wote, mfumo wetu rasmi wa elimu wa sasa, kwa mfano Sera ya Elimu ya mwaka 2014 elimu msingi, ukiangalia na mitaala yake. Mitaala ya darasa la saba tayari imeshafundishwa darasa la nne, la tano na la sita. Ukiangalia Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, kwa nini hatukubali kuwa na mfumo ambao ni shirikishi, ni sawa, na ni elekezi kwa wote, badala ya kila Waziri anayekuja anakuja na mfumo wake na matamko yake ambayo tunaharibu elimu ya Taifa la Tanzania, lazima tuiangalie Tanzania kwa miaka zaidi ya 50 ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kwenda Finland, Finland, kwa nini hata mwaka jana, wameweza kuwa ni watu wa kwanza duniani kwa watu wao kuwa na raha? Waliandaa mifumo yao ya elimu yenye kujenga utu wa binadamu kwa zaidi miaka 40 iliyopita. Wakasema Taifa letu, tunataka liwe na uelewa wa namna gani, Taifa letu watu wake wajitambue namna gani, Taifa letu tushirikishane namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bahati mbaya sana hapa tunazungumzia formal education, lakini non formal and informal education tunaiweka kwenye hali ya namna gani. Uandaaji wa sera hizi, Daktari ndiyo ukienda hospitalini anakwambia wewe umeugua kitu gani na unatakiwa utibiwe namna gani? Leo hii, ukija kwenye Sera zetu za Elimu mitaala yetu inatengenezwa na watu wengine, ambao sio wale walezi, Walimu ambao wangekuwa ni shirikishi wa kutosha kwa sababu wanajua athari za watoto. Ukija hata kwenye lishe yetu, siku 1,000 za kwanza, yaani miaka miwili na miezi tisa, watoto wetu wanapokosa lishe ya kuweza kujenga vizuri uwezo wao, kwa mfano jana niliona mtu mmoja, mvua imenyesha, lakini kwa sababu yeye ameshazoea kwamba lazima kila siku aamke na amwagilie bustani, mvua huku inanyesha na huku anamwagilia bustani. Unakuta tayari ana udumavu wa akili kwa sababu alikuwa amezoea tu na unajua kwamba ni mtu mwenye akili nzuri tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, so we must think big, and think global namna gani tunawaacha, tunawakuza watoto wetu, namna gani tunawapa Walimu wetu ambao ndiyo walezi wakuu wa Taifa letu, waweze kuliangalia Taifa, waweze kuwa na utulivu, waweze kulea watoto wetu. Kwa sababu kama mama wewe, unamtoa mtoto wako unamkabidhi Mwalimu, ni kwamba umemwamini zaidi huyu Mwalimu kuliko hata wewe mzazi, kuliko hata mfanyakazi wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako alikuwa Taasisi ya Elimu, alikuwa Baraza la Mitahani, ametoka huko amepewa dhamana hiyo, anaacha legacy ya namna gani kwa Taifa la Tanzania kwamba umeanzisha mfumo huu, tunaiona Tanzania ya miaka 50, tunaiona Tanzania ya miaka 30 yenye uelewa wa hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Naibu Waziri, Mheshimiwa Ole chonde chonde, tuache tofauti zote, tuwe na utulivu wa ndani, tukubali bila shaka, ukitaka kuliangamiza Taifa lolote lile anza kuua mifumo yake ya elimu inayolinda utu wa binadamu. Sasa hapa kila siku tunapiga kelele, hili, limetokea hivi, hili limetokea, tunakuwa negative, negative, let us think positive, think globally, think big and tuione Tanzania ya miaka 50 ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vitabu, leo hii Taasisi ya Elimu, inachofanya na vitabu, kwa mfano tangu mwaka 2014 vitabu vya darasa la sita, vitabu vya darasa la saba, viko, havionekani, viko wapi? Tunasema vinaandaliwa, vinaandaliwa, niombe chonde chonde wawachukue akina Mzee Walter Bugoya, tuachane na tofauti zetu. Tuseme yaliyopita, yamepita si ndwele tugange yajayo, wawachukue akina Mzee Mture Elibariki, wanavyo vitabu vingi tu. Wazungumze nao, wawe na partnership, washirikiane nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule binafsi naupongeze Mkoa wa Kilimanjaro, ambao unaongoza na nimekuja kufanya utafiti kwa nini unaongoza?. Utaona shule nyingi ni za binafsi ndizo zinazoongoza, sasa Serikali badala ya kupambana na hizi shule binafsi ionekane ni washindani, wawe na ubia nao wawe ni washirika wenzao, hata kuwapatia ruzuku kwa sababu wanaelimisha Taifa kwa niaba ya Watanzania wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo niombe Walimu tulioko humu ndani, na asilimia 35 ya shule za Sekondari za Mkoa wa Kilimanjaro ni Shule binafsi na niwapongeze sana na Shule za Walimu wa Vunjo. Nikiangalia Ikama ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi tunazungumzia Walimu, Ikama ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, shule za Sekondari za Serikali zina upungufu wa Walimu 685. Shule za Msingi zina upungufu wa Walimu 376, sasa licha ya kazi kubwa wanayofanya Walimu hawa na wa Vunjo kule Halmashauri ya Moshi na sehemu nyingine Tanzania nzima, ni namna gani tunawapa uwezo, shule unakuta ina Walimu wawili au watatu, sio Wabunge tuje hapa tuongee basi tumeondoka. Wakati wa kupitisha bajeti, Wabunge tuoneshe nafasi yetu kwa mujibu wa Katiba tuiambie Serikali hapana, ukiwekeza kwenye akili ya mwanadamu ndiyo miundombinu mikubwa yenye rasilimali kuu, kuliko raslimali nyingine yoyote ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuipe Wizara hii bajeti ya kutosha, tufikiri vizuri, tuisimamie Serikali, la sivyo, watoto wetu miaka 20 ijayo, miaka 30 ijayo watakuja kuona kizazi hiki ni kizazi cha ajabu kweli, kwa mfano Joseph Roman Selasini hapa, Mbunge wa Rombo, baba yake alikuwa ni Mwalimu na aliwanasihi vizuri familia yao na unaweza kuona wamefika wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi baba yangu alikuwa Mwalimu na unaweza kuona nimekuwa ni zao la namna gani, sasa hebu jamani tuache tofauti zetu, tulikumbuke Taifa letu, tumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wote humu ndani tukisema Tanzania, tunasema hakuna mwingine kama Mwalimu, tukisema Tanzania tunarudia hakuna mwingine kama Mwalimu, tukisema Tanzania tunasema hakuna mwingine kama Mwalimu. Tukisema mlezi wa Taifa la Tanzania, tunasema ni Mwalimu, mlezi wa Taifa la Tanzania tunasema ni Mwalimu, mlezi wa Taifa la Tanzania, tunasema ni Mwalimu. Sekta inayozalisha kuliko zote ni Wizara ya Elimu, sekta inayozalisha kulko zote ni Wizara ya Elimu tuache tofauti nyingine zote tukubali sote kwa pamoja, Taifa hili ni letu sote tulinyonyeshe Taifa hili, tumnyonyeshe mama Tanzania kwa kuipa upendo Sekta ya Elimu, ili Sekta ya Elimu iweze kuwa na utulivu wa ndani, iweze kuwa na furaha, inyonyeshe watoto wa Tanzania ili Mwalimu wetu aweze kuwa nambari moja katika Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. (Makofi)