Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Awali ya yote naomba nitumie nafasi hii kuwashuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Madaba kwa kuitikia wito wa Mheshimiwa Rais wa Hapa Kazi Tu kwa vitendo. Wameshiriki kikamilifu katika ujenzi wa miundombinu ya elimu yakiwemo madarasa, mabweni na mabwalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee niwapongeze wananchi wa vijiji vya Wino, Lilondo na Maweso ambao katika umoja wao wamechangia zaidi shilingi milioni 104 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba makazi yao yanapata maji lakini shule zote za sekondari na za msingi wanapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti niwapongeze wazazi wa shule zote za msingi za Madaba. Kwa namna ya pekee, wazazi wa Shule ya Msingi Njegea, Igawisenga, Turiani, Kifaguro, Mahahanje, Likalangilo na shule nyingine ambazo katika umoja wao katika kila mwaka wanachangishana zaidi ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya kupata walimu wa ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali na kwa namna ya pekee Wizara hii ya Elimu na TAMISEMI ambao wameunga mkono jitihada za wananchi wa Madaba kwa kuhakikisha kwamba ile miundombinu ambayo wazazi wameendela kuijenga, Serikali inaikamisha. Tumepata fedha nyingi kwa ajili kukamilisha, lakini kutokana wingi wa mahitaji yetu, bado hizo fedha hizo hazitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sikupata nafasi kuchangia kwenye Wizara ya TAMISEMI, nitumie nafasi hii hii pia kuiomba Wizara ya TAMISEMI watuongee bajeti na kuhakikisha kwamba madarasa, mabweni na mabwalo ya shule zetu za msingi na sekondari yanakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekti baada ya hizo shukrani kwa wananchi wa Madaba na kwa Wizara, nitumie nafasi hii kutoa wito kwa Wanamadaba kuhakikisha kwamba tunaendelea kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja kwa sababu tuna jukumu la pamoja kuhakikisha kwamba watoto wetu wanapata elimu bora na wanapata katika mazingira mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nitoe ushauri kwa Serikali. Tunayo changamoto kubwa sana ya walimu katika shule zetu. Hili siyo kwa Shule za Madaba pekee, ni shule za sekondari karibu taifa zima. Tatizo hili la walimu pengine tunaweza tukalichukua kama dogo, lakini madhara yake yanaonekana dhahiri katika maeneo tunayotoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna vijana waliohitimu kidato cha nne katika shule zetu mbalimbali. Kijana huyu tangu anaanza Form One mpaka anamaliza kidato cha nne, kwa sababu ya kukosa Walimu darasani, wametumia madarasa yetu kama vijiwe vya kujadili masuala ya siasa na kuijadili Serikali katika mambo wasiyoyataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawa wanapotoka mashuleni wanahamishia mijadala kwenye vijiwe na kwenye mitaa yetu. Kwa kadri tunavyoendelea, Taifa hili sasa linaelekea kupata wanung’unikaji na siyo watenda kazi katika Taifa hili. Jambo hili leo tunaweza kulichukulia mzaha mzaha, lakini kwa kadri siku zinavyokwenda, tunazalisha vijana wa kijiweni ambao hawana ajenda nyingine zaidi ya kulalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imeelezwa kuhusu sera yetu ya elimu. Nimeona Wizara imeweka mkakati wa ku- review hii sera sayansi, teknojia na ubunifu. Hili lisichukue muda. Mwaka 2018 tumeona huo mchakato ukiangalia kwenye hii taarifa ya Wizara ambayo ni nzuri sana, lakini unaona katika ukurasa wa tisa wanasema Wizara imeanda Rasimu ya Mapitio ya Sera ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu. Mwaka umeisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa bajeti Wizara inaendelea na mchakato na inasema itakamilisha Mapitio ya Sera ya Sayansi na Teknolojia ya Mwaka 1996 ili kuwa na Sera ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu inayoendana na mahitaji ya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa miaka miwili inakatika; hili haliakisi kabisa kasi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Naiomba Wizara Watanzania wanatambua umuhimu na wanaona jithada zinazofanyika na hawana tatizo, lakini tuongeze speed ya kufanya kazi. Tufanye review ya hii sera kwa wakati ili Watanzania waliopo mashuleni, waliopo kwenye vyuo vyetu za ufundi waweze kunufaika na hii sera. Tutaisubiri hadi lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini sera hii inayoenda kufanyiwa review itazingatia ukweli kwamba kila Halmashauri ya Wilaya tunahitaji kuwa na Vyuo vya Ufundi na siyo kimoja. Kwa sababu watoto wanaohitimu kidato cha nne ni wengi, wanaopata fursa ya kujiendeleza sekondari kwa maana ya kidato cha tano na cha sita na wanaokwenda Vyuo Vikuu ni wachache. Hawa wanaobaki tunawaachia ujuzi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hatutaki ku- capture? Kwa nini hatuataki ku-tap hii rasilimali muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu? Namna nzuri ya kutumia hii rasilimali watu ambayo ina ari ya kazi ni kuiongezea ujuzi kupitia vyuo vyetu vya elimu. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri tuwajengee uwezo vijana wetu wawe na uwezo wa kiufundi na kiujasiliamali ili tuondoe tabia yao ya kulalamika, tuwajenge uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, walimu wetu katika maeneo mbalimbali wana hali ngumu sana. Wengi hawajapandishwa madaraja kwa muda mrefu. Kwa hili sisi Wabunge tumetekeleza wajibu wetu wa kuja mpaka kwenye Wizara zinazohusika kuyaeleza, lakini hayafanyiwi kazi. Wengine madaraja yamekwama kwa miaka minne, mitano; wengine posho zao za miaka mingi tunakwenda kujenga Taifa la walimu wanaolalamika ambao watawazaa wanafunzi na vijana wanaolalamika na mwisho tutapata Taifa la walalamikaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)