Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Alfredina Apolinary Kahigi

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Nianze na Wizara ya Elimu, Wizara ya Elimu mimi nitaanza na Walimu. Walimu ni kioo cha jamii lakini Walimu kuanzia mavazi, kuja maadili, kuja na mahusiano na jamii Walimu wana upungufu. Kwa mfano mavazi, Walimu hapo zamani tulikuwa tunawaona ndiyo watu ambao wanafundisha watoto, kujipenda, kuvaa vizuri, kuwa wasafi lakini Walimu wa sasa hivi wanasikitisha mavazi wanayovaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Walimu wa kike, baadhi siyo wote wanavaa nguo ambazo hazina heshima yoyote, nguo ambazo ni fupi kiasi kwamba wanafunzi hawajifunzi kitu chochote kwa mavazi wanayovaa. Niombe Wizara ya Elimu katika suala hilo la mavazi iliangalie sana iwape mwongozo kusudi wawe wanavaa nguo ambazo wanafunzi wataona kwamba na sisi tujifunze kutoka kwa Walimu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwa watoto wa kiume wanavaa ma-jeans tisheti, jeans hilo akilivaa wala kulinyoosha halinyooshwi utadhani ng’ombe amelitafuna amelitema ndiyo anakuja amelivaa mwanafunzi akiona namna hiyo kwa kweli haileti ustaarabu wa aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka katika mambo ya mavazi, nije katika maadili. Sisi ambao tumetoka vijijini Walimu wa vijijini wanasikitisha, baadhi lakini siyo wote. Wanalewa, wanakunywa pombe yaani Mwalimu anakuta wanacheza ngoma na yeye anafunga kanga anacheza ngoma na wanafunzi wanamwona, kwa kweli haileti heshima yoyote. Mwalimu ni kioo kama nilivyosema, hapaswi kunywa pombe akalewa mpaka na wanafunzi wale ambao anawafundisha wakamwona kesho yake akija darasani watajifunza kitu gani, ni aibu tupu. Niombe Wizara ya Elimu, wajaribu kuwakanya, wajaribu kujieshimu ili watoto wetu waweze kuchukua maadili mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye mahusiano ya Walimu na jamii. Kuna baadhi ya Walimu wanajifanya Miungu watu. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Profesa Ndalichako na uongozi mzima kwa kitendo ambacho walitufanyia watu wa Kagera kwa mtoto yule aliyepigwa mpaka akauwawa lakini walisuuza nyoyo za Wanakagera au na wazazi wote Tanzania nzima kwa yule Mwalimu aliyempiga na ameadhibiwa kutokana na makosa yake, lakini bado baadhi ya Walimu wana tabia ambayo si nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi niliangalia kwenye WhatsApp, kuna Mwalimu sehemu za Mbeya amepiga mtoto wa miaka nane, alimfunga miguu juu, kichwa chini mtoto wa miaka nane, eti ameshindwa kufanya hesabu, akampiga mpaka akamvunja uti wa mgongo. Mheshimiwa Waziri nitapenda hilo alifuatilie sana, tujue matokeo ya huyo mtoto. Sisemi vitu vya longolongo nasema vitu ambavyo nimeviona, amenisikitisha mno hata angelikuwa ni mtoto wako ungelia, mimi nilisikitika sana sana. Amempiga, wazazi wake wamemshughulikia yule mtoto mpaka hela zimewaishia, sasa hivi wamelipeleka mpaka kwa Mkuu wa Wilaya. Naomba Mheshimiwa Profesa Ndalichako alifuatilie hilo suala awasaidie wale wazazi wana masikitiko makubwa na mtoto wao. Bado kuna Walimu ambao ni wakorofi, wanajifanya ni Miungu watu, huyo Mwalimu nasikia wamemtoa kwenye hiyo Kata ameenda kwenye Kata nyingine aendeleze na ubabe wake huo, naomba afuatiliwe mpaka apatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za msingi ambazo hazina uzio. Mheshimiwa Waziri, niombe Serikali washughulikie kuwajengea walau shule ambazo ziko mijini, uzio siyo wa matofali hata ukiwa wa senyenge kusudi kile kipindi cha break ambacho wanatoka madarasani kwenda nje, wasizurure hovyo hovyo yaani ndiyo kipindi ambacho wanatoroka, wengine wanaenda kuvuta bangi, wengine wanaenda kufanya mambo ambayo ndivyo sivyo. Niombe walau zile shule ambazo ziko mjini, wajaribu kuwawekea uzio wawe wanakaa shuleni hapo wana-discuss na wenzao muda ukifika wa kurudi nyumbani waende nyumbani, siyo kuzurura zurura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoke huko nije kwenye suala la Mitaala, suala la Mitaala kuna shule Serikali na shule za binafsi. Shule za Serikali wanafunzi kuanzia awali wanajifunza Kiswahili tu, Kiingereza ni kidogo mno mpaka darasa la saba, lakini shule za watu binafsi wanajifunza Kiingereza kuanzia shule za awali mpaka juu. Kwa hiyo tumekuwa na matabaka ya hawa watoto, watoto wa shule za binafsi wanajiona ni bora zaidi kuliko hawa wenzao na hawa watoto wanapenda nao kujifunza Kiingereza lakini wazazi wao hawana fedha za kuwapeleka kwenye shule za Kiingereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiingereza ni muhimu, sisemi Kiswahili siyo muhimu, Kiswahili ni lugha yetu ya Taifa, ni lugha nzuri sana na mimi naipenda lakini na Kiingereza ni lazima na watoto nao wajifunze. Kama ni kusoma lugha zote mbili, Kiingereza na Kiswahili watoto wote wasome lugha hizo kusudi waweze wote kuwa uniform. Naomba Wizara hilo na lenyewe waliangalie na wengine wameshaliongelea zaidi na mimi nimeliongelea hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye motisha; Walimu nawapenda sana, japokuwa wanafanya mambo ya ndivyo sivyo hao ambao nawasema lakini wengi wanajituma wanafanya kazi nzuri. Naomba Serikali iwaangalie, mishahara yao ni midogo sana, kuanzia shule za chekechea mpaka kwenye vyuo. Sijui maprofesa labda wao wanakula mishahara mizuri sana sijui, lakini hawa Walimu wengine wanakula mshahara mdogo sana. Serikali iwaangalie Walimu iwaongezee mshahara, japokuwa wafanyakazi wote wanalia lakini Walimu wanafanya kazi ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani walikuwa wana- teaching allowance sijui zilienda wapi. Naomba Serikali wafanye mpango zirudi kusudi waweze kukimu mahitaji yao angalau madogo madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mengi ya kusema mengine nitayaandika, lakini yangu ni haya. Nashukuru sana. (Makofi)