Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya Waziri. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna anavyosimamia suala la elimu na idadi ya wanafunzi wameongezeka kutokana na uamuzi wake wa msingi kabisa kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanasoma bure hasa elimu ya msingi kuanzia awali mpaka kidato cha nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana Profesa Ndalichako, Waziri wa Elimu, Naibu Waziri wake, Naibu Waziri wake Mheshimiwa Ole Nasha, Katibu Mkuu wa Wizara hii ya Elimu na Manaibu Katibu Wakuu wote na watendaji wote kwa namna wanavyofanya kazi kwa weledi lakini pia kwa kujituma kuhakikisha kwamba kiwango cha elimu kinaongezeka nchini, niwapongeze sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kidogo kuhusu suala la kwanza juu ya mikopo ya wanafunzi hasa mikopo ya elimu ya juu, kuna tatizo kubwa sana sasa hivi pamoja na kwamba wigo wa mikopo umeongezeka wanafunzi wengi wanapata mikopo lakini bado kuna idadi kubwa ya wanafunzi wengi wanakosa mikopo na hatimaye wengine kuacha kabisa kuendelea na masomo ya Chuo Kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wengi wanaotoka vijijini maeneo ya vijijini wanakuwa wamedahiliwa, lakini wakifika Chuoni, kutokana na masharti yaliyopo au vigezo vilivyopo basi wanakosa na mwisho wa siku wanarudi tu vijijini na kuendelea na maisha pengine kufanya shughuli nyingine kuacha kabisa kuendelea na masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Wizara lakini pia nishauri Serikali, nafikiri sasa tuanzishe utaratibu, kwa kuwa wanapewa mkopo na wanapewa na unaitwa mkopo siyo kwamba wanapewa bure tu, ni hela ambazo wanatakiwa warejeshe baada ya kumaliza masomo yao. Hivi ni kwa nini sasa tusiwe na utaratibu kwamba kama mwanafunzi amedahiliwa kwenda kuanza Chuo Kikuu apewe tu mkopo kama tunavyosema mkopo, akimaliza basi abanwe alipe na kwa kuwa sasa tunaona hata makusanyo ya mkopo yanaongezeka kutokana na jitihada zao, basi tuombe sasa tuwape mikopo wote wanafunzi ambao wanakuwa wamedahiliwa kwenda Chuo Kikuu, kuliko ilivyo sasa hivi, utakuta kwamba watoto wengi wa maskini, sisi tunaotokea maeneo ya vijiji Wabunge tunajua, tunajua namna gani watoto wanavyohangaika huko, kila siku watoto wamejaa milangoni, wanaomba tuwasaidie namna ya kusoma Chuo Kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe sana Serikali yangu, tuamue tu kwamba sasa mikopo itakuwa kwa wanafunzi wote wanaoenda Chuo Kikuu mradi tu wamechaguliwa. Kama haiwezekani kuwasomesha watoto wote kwa kuwa wanafunzi ni wengi wanaosoma Chuo Kikuu, basi tuanzishe utaratibu kwamba kama tumeamua division one, division two ndiyo watakaopata mikopo, basi iwe hivyo ili mwanafunzi ajue mapema kwamba mimi nimepata division three au nimepata points ambazo haziruhusu kupata mkopo, basi aanze utaratibu pengine wa kujiunga na vyuo vingine kuliko kuruhusu mtoto anadahiliwa anaenda Chuo Kikuu, anakosa mkopo mwisho wa siku wengine wanajiingiza kwenye tabia ambazo au mienendo ambayo haifai katika nchi yetu. Kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Profesa Ndalichako wakae huko ndani Serikalini washauriane namna gani ya kuwasaidia Watanzania hawa wanaotaka kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

Mheshimiwa mwenyekiti, jambo la pili ni juu ya lugha ya kufundishia, tumekuwa in dilemma siku zote, ukiangalia hata sera yenyewe ya elimu unakuta kule ndani kuna contradiction, sehemu moja inafuatana sikumbuki sehemu gani kama siyo 3.2 to nine inasema kwamba elimu ya kufundishia sasa itakuwa Kiswahili, lakini ukienda chini yake pale inasema kwamba elimu tutaendelea na kufundishia maana elimu ya sekondari kwa lugha ya Kiingereza sasa ni vizuri tukaamua, kwa sababu hawa watoto tunawachanganya wanapokuwa shule ya msingi wanasoma Kiswahili, wanapofika form one wanaanza Kiingereza kwa hiyo kwao inakuwa ni lugha ya pili sasa na kitaalam ni kwamba ili mwanafunzi asome vizuri ni vizuri atumie lugha yake ya kwanza. Hiyo Walimu wote tunajua na sisi wote Walimu tunajua kwamba lugha ya kwanza ndiyo inamwezesha mtoto ku-acquire maarifa kivizuri zaidi na aki- acquire vizuri kwa sababu uelewa wake ni mzuri ataendelea vizuri na mwisho wa siku atakuwa na ufaulu mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukiangalia matokeo, ukiangalia matokeo ya shule ya msingi, shule ya msingi wanafaulu sana watoto wakifika sekondari wanaanza kufeli. Kwa hiyo ukiangalia wanaoshindwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano sekondari ni wengi zaidi ukilinganisha na walioanza pale form one. Ukichunguza ndani lugha ya Kiingereza ni shida Tanzania. Kwahiyo tuamue vizuri, tuamue kwamba tunaamua kufundishia Kiingereza, toka darasa la kwanza ama toka awali mpaka Chuo Kikuu au tunafundisha Kiswahili toka awali mpaka Chuo Kikuu. Kwa hiyo niombe tusibaki na dilemma hii itatusumbua kwa hiyo ni vizuri tukae tuamue kwamba ni lugha gani sasa tunaenda kufundishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya udhibiti wa ubora. Niipongeze Serikali nipongeze hatua zilizochukua kuhakikisha kwamba zinaanza kujengwa ofisi, lakini pia tunaanza kuwanunulia magari. Tatizo la magari imekuwa ni changamoto kubwa sana ukienda kwenye halmashauri nyingi magari wanayotumia Wadhibiti Ubora yamechoka na siyo magari tu hata mafuta ya kwenda kufanyia ukaguzi hawana utakuta mara nyingi wanaenda kukagua shule binafsi zisizo za Serikali kwa sababu wale wanalipa ada wanatumia zile fedha kwa ajili ya kuwajazia mafuta na posho, lakini shule za Serikali imekuwa tatizo kwa sababu wakati mwingine hawapati posho wanategemea halmashauri yenyewe iweze kuwachangia mafuta ili waweze kukagua na hili ndiyo jicho la Serikali kwenye upande wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara ya Elimu iwawezeshe Wakaguzi, Kitengo cha Ukaguzi ili muda wowote wanapoona kuna dalili za mwenendo kwenye shule fulani hauendi vizuri au taaluma haiendi vizuri waweze kwenda kukagua muda wowote ambapo anaweza akafanya hiyo kazi, kuliko wanavyokuwa na bajeti ndogo ya mafuta na magari yenyewe hawana ya kutosha, kwa hiyo inakuwa shida kwenda kukagua mpaka wasubiri wawezeshwe. Kwa hiyo hii sasa inazorotesha ubora wa elimu kwenye shule zetu. Hivyo, nimwombe sana ndugu yangu Profesa Ndalichako, yeye ni mtaalam wa elimu, lakini wote pia ni wataalam awawezeshe hawa Kitengo cha Udhibiti Ubora ili waweze kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kuendelea kufanya kazi zao vizuri ili tuweze kuboresha ubora wa elimu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia juu ya elimu ya ufundi, nilishauri mara kadhaa hapa, ni vizuri turudishe ule utaratibu wa zamani kwamba tuwe na shule za misingi za ufundi, kila kata kuwe kuna shule mojawapo ambayo itakuwa na mchepuo wa ufundi, lakini pia kwenye tarafa au kwenye halmashauri tuwe na Sekondari moja ya ufundi ili tuanze kuwazalisha mafundi michundo wengi. Ilivyo sasa hivi, mpaka mtu amalize form four, amefeli ndiyo anaanza kutafuta fursa ya kuajiriwa anakwenda kusoma Chuo cha VETA. Kwa hiyo tukianza huko chini kwanza tutakuwa na mafundi wa kutosha kuanzia shule za misingi, hata kama amemaliza la saba amefeli, hajaendelea na masomo ya sekondari ana uwezo wa kujitegemea kwa sababu ana skills ambazo zitamfanya aweze kujiajiri yeye mwenyewe. Hivyo hivyo anayemaliza form four badala ya kusubiri ajira nyingine anaweza akaanzisha shughuli na mwisho wa hizo shughuli hizo ndogo ndogo zitafanya watu wengi waweze kuajiriwa kwa mfano kwenye useremala, kwenye umakenika mdogo kwenye ufundi uashi na ufundi mwingine, mwingine mwingi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali yangu tuanze kuanzisha huo, pamoja na kwamba tunaanzisha vyuo na tunaziboresha hizi Focal Development Colleges, hizi tuziwezeshe ni kweli, lakini pia tuangalie shule za msingi ambazo tunaweza tukaanzisha kwenye kila kata, lakini pia kwenye kila tarafa au halmashauri kuwe na shule ya ufundi na mwisho wa siku tutakuta kwamba tumepata wataalam wa kutosha kuliko ilivyo hivi sasa hivi. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Mheshimiwa Ole Nasha na wataalam wengine wa Wizara, hebu wajifungie ndani waweze kuangalia namna gani tunaweza tukafanya haya mambo yote yaweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana kwa nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)