Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ufafanuzi wa hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge kutokana na hotuba yangu ya taarifa ya utekelezaji wa mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/2019 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2019/2020 niliyoiwasilisha hapa Bungeni tarehe 24 Aprili, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yangu imechangiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo imetoa maoni na ushauri kwa Wizara na Serikali kwa ujumla katika maeneo mbalimbali. Kwa dhati kabisa naishukuru Kamati hii kwani imekuwa ikitoa maoni ya msingi kwa Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 92 wamechangia hotuba hiyo, kati ya hao Wabunge 45 wamechangia kwa kuongea na Waheshimiwa Wabunge 47 wamechangia kwa maandishi. Pamoja na maelezo ya ufafanuzi nitakayoyatoa, hoja zote za Waheshimiwa Wabunge zitawasilishwa rasmi kwa maandishi katika Ofisi ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima nianze kutoa majibu kutokana na ushauri mbalimbali ambao umetolewa na Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, lakini kwa sababu ya muda nitagusia maeneo machache na ushauri mwingine ambao umetolewa na Kamati naomba uingie kwenye Hansard kwa sababu Wizara ushauri wote uliotolewa tumeuzingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametoa ushauri kwamba Serikali itenge shilingi bilioni nane ili kuendeleza Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto pale Mchicha, Dar es Salaam. Tumezingatia ushauri wa Kamati kwamba kwa kuwa tumehamia Dodoma na sasa tumeanza kujenga Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mjini Dodoma, lile jengo tumeunda Kamati Ndogo ya Wataalam ili waweze kutushauri kwa ajili ya kubadilisha matumizi na kwa sababu tuna chuo, tunaweza tukafanya kuwa Tawi la Chuo chetu cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Kamati yako ilishauri kwamba mchakato wa kukamilisha Sheria ya Usalama barabarani umechukua muda mrefu. Nikuhakikishie pamoja na Bunge lako tukufu kwamba katika Mwaka huu wa fedha, sheria hii iko katika hatua nzuri tutakuwa tumeiwasilisha kwenye Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwewnyekiti, pia ushauri mwingine ambao tumeuzingatia ni kuendelea kutumia utaratibu wa Bodi ya Parole ya kupata adhabu mbadala kwa ajili ya kupunguza msongamano kwenye Magereza wa wafungwa pamoja na mahabusu. Si hilo tu, ni pamoja na kuendelea kutumia msamaha wa Mheshimiwa Rais ikiwa ni pamoja na kujenga magereza hapa nchini kama ambavyo tunaelekea kumaliza Gereza la Ruangwa pamoja na Chato pamoja na ukarabati na kupanua mabweni kwenye magereza mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ambao ni vyema nikaugusia ni kwamba Kamati ilishauri Serikali itoe fedha za maendeleo bilioni 5.79 zilizoidhinishwa kwa ajili ye ujenzi wa Ofisi za Uhamiaji za Mikoa, Wilaya na vituo, hata hivyo fedha hizo kwamba hazikutolewa. Ni kwamba Wizara imeendelea kuwasiliana na Hazina na mpaka sasa tunaendelea na mawasiliano kuhakikisha kwamba hizo fedha kabla ya mwaka wa fedha haujakwisha zinatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ushauri walioutoa ambao ni vyema nikaugusia ni huu wa wahamiaji haramu kwamba wahamiaji haramu wapatao 3,260 wako kwenye magereza yetu hapa nchini na wametoa ushauri, tumezingatia na hasa ikizingatiwa kwamba Tanzania, Ethiopia pamoja na Kenya tumefanya mkutano wa pamoja, yako mambo ambayo tumekubalina kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo la wahamiaji haramu. Kwa hiyo ushauri wote ambao Kamati imetupatia sisi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tumeuzingatia na tutaufanyia kazi na hatutakuwa na mzaha. Naamini ninavyozungumza hapa, Naibu Waziri anajua, Naibu Katibu Mkuu na Katibu Mkuu wote wamesikia na Wakuu wote wa vyombo wamesikia, tutafanya kazi kama mchwa usiku na mchana kuhakikisha kwamba yote haya tunayatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kugusia hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge zingine ambazo zimetolewa kwa maandishi, zingine kwa kusema na zinahusu vyombo vya ulinzi na usalama mbalimbali ambavyo viko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kabla sijafikia hatua hiyo, nataka niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge na nataka niuthibitishie umma wa Watanzania kwamba mkiona vyaelea vimeundwa. Amani na usalama na utulivu wanaouona katika nchi hii ni kwa sababu ya kazi nzuri, kazi ambayo imefanywa na vyombo vya ulinzi na usalama na hususan Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa nchi yenye heshima duniani na kuheshimika kwa kuwa na amani na usalama wa hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, nataka niwafahamishe Wabunge; kazi namba moja kabisa ya Jeshi la Polisi ni kumlinda Mheshimiwa Rais pamoja na Taasisi yake na ndiyo maana alipo Mheshimiwa Rais, Jeshi la Polisi tupo. Hainiingii akilini baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kusimama na kubeza kazi nzuri zinazofanywa na Jeshi la Polisi na kulibatiza majina mengine ya kejeli, kitu gani ambacho unakifanya wewe mpaka uone kwamba Jeshi la Polis linahitaji kubatizwa majina ya namna hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi, siku mia tatu sitini na tano na robo hawana cha Jumamosi, hawana cha Jumapili, hawana cha Sikukuu, hawana cha mvua, hawana cha jua. Askari hawa wanafanya kazi kubwa halafu humu ndani anaibuka Mbunge anasema hata Askari kung’atwa na mbu hiyo ni kazi yao, ni majukumu yao na maneno hayo yanazungumza na mtu ambaye anaheshimika, Mheshimiwa ambaye ni Mchungaji na sisi waumini hatumwiti tu Mchungaji, tunamuita Baba Mchungaji, lakini anasema maneno ya namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu hapa wanasema Jeshi la Polisi wanatumia lugha ambazo ni za kuudhi, za kejeli, hazina staha. Nataka nikuhakikishie; wakati ule CAG aliposema Bunge hili ni dhaifu wapo baadhi ya Wabunge hapa walitetea kauli hizo ambazo ndizo za kejeli, kauli ambazo zinadhalilisha Bunge lakini leo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Kamanda ambaye amefundishika, Kamanda ambaye anajua kutumia lugha za Kibunge anasema “ole wao watakaoandamana kesho, watapigwa na watachakaa” hiyo ni lugha ya kufundishwa Askari ambaye amefundishika, hiyo ndio lugha ya kipolisi”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie sisi Jeshi la Polisi tunazo lugha nyingi ambazo tukiongea hapa wengine hamtatuelewa. Kwa mfano, wewe unaitwa Mheshimiwa Zungu sisi Polisi tunakuita Zulu uniform Novemba uniform ndivyo tunavyokuita sisi, hawa hawatatuelewa. Tunaposema kwamba tunatumia lugha hizi, lugha hizi zinatokana na preemption model. Preemption model kwenye Jeshi maana yake nini, nifungue darasa kwa wale walioikosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linapoona kwamba kuna mambo ambayo yanataka kufanyika, mikusanyiko isiyoruhusiwa, Jeshi la Polisi tunajiandaa kwenye vifaa ndiyo maana mtaona askari wanamwaga mahali wanatembea kikakamavu, wanafanya hivi kuona kesho uandamane uone cha mtema kuni. Wakati mwingine tunatumia lugha hizi kwamba ole wake na wale tunaowaambia lugha hizi ni wale watakaokuwa wahalifu, hii ni lugha ya kushughulikia wahalifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa Mheshimiwa Msigwa mara kwa mara namuona ananyanyua Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Niende kwenye hiyo hoja ya mikutano ili tumalizane na akina Mheshimiwa Msigwa na Mheshimiwa Ruth Mollel na wote wale ambao mmekuwa mkiuliza ni sheria gani inawanyima haki ya mikutano ya ndani, inawanyima haki ya mikutano ya hadhara na mnisikilize vizuri ili leo tumalizane hapa. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipo apa kwenye Uwanja wa Taifa aliapa kuilinda, kuhifadhi na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais anapokuwa analinda na kuitetea ni kuhakikisha yale yote yaliyoandikwa humu yanatekelezwa na hayavunjiwa na mtu yeyote na yeye kama Mkuu wa Nchi anasimamia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 20(1) unayoinua inasema hivi: “Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 20(3) inasema hivi: “Bunge laweza kutunga sheria inayoweka masharti yatakayohakikisha kuwa vyama vya siasa vinazingatia mipaka na vigezo vilivyowekwa na masharti ya ibara ndogo ya (2) kuhusu uhuru na haki ya watu kushirikiana na kujumuika.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 30 ya Katiba inaweka masharti ya mipaka na inasema hivi: “Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika sehemu hii ya Katiba hii, yanayofafanua misingi ya haki, uhuru na wajibu wa binadamu, hayaharamishi, naomba nirudie, hayaramishi sheria yoyote iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote halali kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo kwa ajili ya-

(a) Kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya na uhuru na haki za watu binafsi. (Makofi/ Vigelegele)

(b) Kuhakikisha ulinzi, usalama wa jamii, amani katika jamii, maadili ya jamii, afya ya jamii, mipango ya maendeleo mijini na vijijini haviathiriwi”. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati umefika sasa, Mheshimiwa Rais alipopiga marufuku mikutano hii ni kwa mujibu wa Katiba hii kwenye vifungu nilivyovieleza kwa maana kwamba mikutano hii…

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Order, order.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Sikiliza basi Mheshimiwa Msigwa.

MWENYEKITI: Order, order.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana kwamba mikutano hii isije ikavuruga mipango ya maendele, nimesoma Ibara hii.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Msigwa Mbunge ukitaka kuongea unafuata utaratibu.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri hebu ngoja kwanza. Waheshimiwa Wabunge, kama Serikali inajibu watu wote tukae kimya.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Hapana, ndiyo muda wake wa kujibu.

MBUNGE FULANI: Anadanganya.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, anajibu ndiyo muda wake, sasa mnapoanza ku-provoke, mnakifanya Kiti kianze kuwa…

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa, kifungu cha 11(1) kinasema hivi: “Kila chama chenye usajili wa muda na usajili wa kudumu kitakuwa na hadhi ya-

(a) Kufanya mikutano katika sehemu yoyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kutoa taarifa kwa Afisa Msimamizi wa Polisi wa eneo husika kwa ajili ya kujitangaza kwa umma na kutafuta wanachama. (Makofi)

(b) Kupata ulinzi kwa ajili ya usalama wa mikutano ingawa vyama vyenye usajili wa muda havitaruhusiwa kuweka mgombea au kufanya kampeni katika uchaguzi wowote wa Ubunge, Uwakilishi au Urais au Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha (2) kinasema: “Bila kuathiri sheria nyingine, vifungu 43, 44, 45 na 46 vya Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi, Sura ya 322 vitatumika katika mikutano yote itakayofanyika ndani ya Jamhuri ya Muungano na chama chochote hata kama kina usajili wa kudumu au usajili wa muda”.

MBUNGE FULANI: Vifungu hivyo vinahusu ulinzi.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha (3) kinasema: “Kila chama chenye usajili wa kudumu kitakuwa na hadhi ya kuweka mgombea na pia kufanya kampeni kwa ajili ya mgombea yeyote katika uchaguzi wa Wabunge, wawakilishi wa Urais au uchaguzi wa Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha (4), Mheshimiwa Ruth Mollel sasa unisikilize vizuri ili uone ni sheria gani tunatumia ya kuzuia mikutano yako ya ndani. Kifungu cha (4) kinasema: “Pale ambapo chama cha siasa kinapokuwa na nia ya kufanya mikutano au maandamano katika eneo lolote la wazi, hiyo ndiyo ya hadhara, au sehemu yoyote, maana yake sehemu ya ndani au wapi, kinatakiwa kutoa taarifa si chini ya saa 48 kabla mkutano husika kufanyika. Taarifa hiyo ni lazima iwe kwa maandishi itakayowalishwa kwa Afisa wa Polisi Msimamizi wa eneo husika ambapo mkutano husika unatarajiwa kufanyika. Ikitokea chama cha siasa kimewasilisha taarifa kulingana na kifungu kidogo cha (4) chama hicho kinaweza kuendelea na mkutano kama ulivyopangwa isipokuwa kitakapopokea amri kutoka kwa Afisa wa Polisi Msimamizi wa eneo husika kutoendelea na mkutano husika, mkutano huo hautafanyika”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zuio hili ambalo linahusisha Sheria ya Vyama vya Siasa limeenda kutafsiriwa kwenye Sheria ya Jeshi la Polisi. Sheria ya Jeshi la Polisi, kifungu cha 42 kinasema hivi: “Mtu yeyote atakayekaidi amri au kudharau au kutekeleza amri iliyotolewa katika kifungu kidogo cha (1) hapo juu atakuwa ametenda kosa na atakamatwa bila hati ya ukamataji na endapo atatiwa hatiani anaweza kuuhukumiwa kulipa faini au vifungo au vyote”. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kinaendelea kusema: “Pale ambapo mtu atawalisha taarifa ya maandishi kama ilivyoelezwa kwenye kifungu kidogo cha (1) anaweza kuendelea kuandaa au kukusanya watu au kuandamana kama ilivyopangwa isipokuwa tu pale anapopokea amri kutoka kwa Afisa wa Polisi Msimamizi wa eneo husika juu ya kusanyiko hilo au maandamano kutofanyika kama ilivyoelekezwa.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilichotaka kuwaambia hawa Wapinzani ni nini? Tatizo la wenzetu hawa hawataki kutekeleza na kufuata Katiba. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la wenzetu hawa hawataki kufuata sheria za Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi. Sasa mimi niwaambie, najua haya yote yanawasumbua kwa sababu mmekosa hewa ya oxygen upande mliopo. Ushauri wangu wa bure kwenye chama kingine cha siasa bado kuna oxygen ya kumwaga na kutosha, kama mnaona kufanya siasa huko hakuwezekani nendeni kwenye vyama vyenye oxygen. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe maelekezo kwa Jeshi la Polisi na naamini IGP unanisikia kwamba vyama vyote vya siasa na najua uchaguzi unakuja Novemba, najua kuna watu wanaokaidi na kutotaka kuzingatia sheria na najua sikio la kufa halisikii dawa, endeleeni kuhakikisha kwamba mikutano isiyoruhusiwa ni kweli hairuhusiwi na wale watakaokaidi waendelee kukamatwa. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila utaratibu)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hoja za Mheshimiwa Msigwa, mimi nakuheshimu sana. Mambo mengi sana yamesemwa humu kuhusiana na watu kupotea, kuuwawa, kutekwa lakini Mheshimiwa Msigwa alienda mbali zaidi akawa ananitaka mimi Waziri kwa niaba ya Serikali nitoe majibu kuhusiana na upigwaji risasi wa Mheshimiwa Tundu Lissu, kutoonekana kwa kina Ben Saanane na wengine aliowataja. Maneno yote haya yanaletwa kwa sababu moja tu na sababu yenyewe ni kutaka Serikali na wananchi kuchonganishwa. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Aaaa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali pale ambapo tunaona Mheshimiwa Mbunge anatoa maneno ambayo kila kukicha tunapotoa maelezo lakini hataki kusikia, anabaki na kazi moja tu. Kazi moja hiyo kwa sababu ni Mchungaji, ukisoma kwenye Kutoka 23:1 inasema: “Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ambaye ni mchonganishi ana shetani ndani yake. Biblia inasema mtu ambaye ni mchonganishi anakuwa ni mmiliki halali wa ibilisi shetani. Biblia inasema mtu ambaye ni mchonganishi anakuwa ni mtumwa wa shetani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba Bunge hili mnisikilize vizuri, nimekuwa nikieleza hapa nyakati mbalimbali kwamba taarifa zote za watu kupotea, kutekwa, kuuwawa, ambazo zimeripotiwa kwenye vituo vya Polisi zote hizi zina mafaili na upelelezi unaendelea. Katika mazingira ambayo upelelezi unaendelea, sisi tuna Jeshi la Polisi lenye weledi na teknolojia katika kufuatilia uhalifu ambao umetokea wa watu niliowataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulaumu Jeshi la Polisi na kutaka kuonesha kidole kwamba matukio hayo yanafanywa na Serikali, sisi kama Serikali hatutakubali. Ziko nchi nyingi ambazo wananchi wake tena wengine maarufu wamepotea, wameuwawa lakini mpaka leo waliofanya matukio hayo hawajapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, nchi ya Marekani ambayo ina FBI, Central Intelligence Agency pamoja na taasisi nyingine 24 za Serikali kwa ajili ya usalama kuanzia mwaka 1947, miaka zaidi ya 72 alikufa pale Elizabeth Short aliyekuwa anataka kujiunga na Hollywood kwa ajili ya movie, mpaka leo pamoja na vyombo vyote hivyo wanaendelea kuchunguza, hawajampata aliyehusika na tukio hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Marekani hapo hapo, kuna mwanamuziki Tupac Shakur, leo ni miaka 23 wanaendelea kuchunguza lakini hawajampata nani amefanya tukio hilo. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sisi Tanzania ambao tunaendelea na uchunguzi pale ambapo hatujapata mtuhumiwa aliyefanya tukio, kwa nini baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaonesha kidole kwa Serikali? Hii yote wanafanya kwa sababu ya kuchonganisha Serikali na wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme bayana matukio mengine kama nilivyowahi kusema upelelezi unachukua siku nyingi na sisi Jeshi la Polisi tunashindwa kuunganisha dot za upelelezi kwa sababu baadhi ya wahusika hawataki kutoa ushirikiano. Umezungumzia kesi ya Mheshimiwa Tundu Lissu, Mheshimiwa Msigwa nilikilize vizuri, unataka kusikia Serikali inasema nini kuhusu nani aliyempiga risasi Mheshimiwa Tundu Lissu, nataka nilihakikishie Bunge lako Tukufu baada ya tukio hili kutokea Polisi tulianza uchunguzi na hata kabla hatujaanza uchunguzi Madaktari wa Serikali kwa nia njema ya kunusuru uhai wa Mheshimiwa Tundu Lissu walikuwa mstari wa mbele kabisa na baada ya hapo kupitia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma alimtaka dereva aliyekuwa na Mheshimiwa Tundu Lissu aje kwenye kituo cha Polisi atoe maelezo. Polisi hawa sio Mungu, Polisi hawa wanahitaji binadamu ambaye alikuwa kwenye tukio aje atoe maelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu wakati huo dereva wa Mheshimiwa Tundu Lissu kwa jina Adam amekimbia na hataki kuonekana kuja kutoa maelezo kwenye kituo cha Polisi. Sasa sisi Jeshi la Polisi huwa tunaangalia na mazingira yanayozunguka tukio lililotokea. Kwa kuwa risasi zilizopigwa ni nyingi zaidi ya 38; na kwa kuwa risasi hizo zilimpiga Mheshimiwa Tundu Lissu kutokea alikokuwa amekaa kuelekea upande alikokuwa dereva lakini dereva alitoka akiwa hana kovu hata ukucha wake kupigwa risasi.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii inatia mashaka na ndiyo maana Jeshi la Polisi wanamtaka Adam aje atoe maelezo nini kilitokea. Pili kwenye gari mule walikuwa wawili tu dereva Adam na Mheshimiwa Tundu Lissu, yeye ni mtu muhimu sana wa kusaidia Jeshi la Polisi.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Sisi Jeshi la Polisi tunakosa usaidizi…

WABUNGE FULANI: Mwongozo, mwongozo.

MWENYEKITI: Waheshimiwa wote mnaofanya fujo nawaona na nawa-note.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Hapana, Serikali inajibu na kama mtu ana hoja baadaye atatoa siyo sababu ya kufanya fujo ndani ya Bunge.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Unapomkatisha Waziri unakifanya Kiti kichukue hatua za Kikanuni. Nimekuona hapo Mheshimiwa. Endelea Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Wewe Mheshimiwa Heche tulia, hizi ajali gani kuanzia Chacha Wangwe dereva anatoka mzima, anakuja Mheshimiwa Tundu Lissu anatoka mzima halafu tusiseme?

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

WABUNGE FULANI: Kakae huko.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, endelea.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Toa dozi, toa dozi Mheshimiwa Kangi.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo baadhi ya watu wamekuwa wakitaka Jeshi la Polisi litumie sheria inayoitwa Mutual Assistance on Criminal Matters kwamba tunaweza tukam-summon mtu yeyote ambaye yuko nje ya nchi akaja akatoa ushahidi. Hata hivyo, katika kesi hii matumizi ya sheria hii yangelenga kwa mtu ambaye anajificha asiweze kuja kwa hiari yake, kwa hiyo, tunatumia vyombo na nchi nyingine kumlazimisha huyo mtu aje lakini kwa dereva wa Mheshimiwa Tundu Lissu na Mheshimiwa Tundu Lissu wenyewe wanatakiwa waje kwa hiari yao na hivyo hatulazimiki kutumia sheria ya namna hiyo. Kwa hiyo, katika mazingira ambayo Mheshimiwa Tundu Lissu ametekeleza kesi yake, katika mazingira ambayo Adam hatakuja kutoa ushahidi, isitokee tena Jeshi la Polisi kulaumiwa katika mazingira ya namna hii.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo lingine, niende kwenye ufisadi ambao umeelekezwa kwenye Jeshi la Polisi. Wako Waheshimiwa Wabunge hapa wameelezea kuwepo kwa ufisadi ndani ya Jeshi la Polisi lakini taarifa za ufisadi huu wamezipata kwenye Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali na kama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tunahakikisha kabisa kwamba hakuna chombo chochote cha ulinzi na usalama ambacho kitakuwa na matumizi mabaya ya fedha, kitafanya ufisadi na ndiyo maana pale ambapo tunabaini kwamba ufisadi umefanyika tumekuwa tukichukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ambao wanahusika na ufisadi huu. Ufisadi mwingine ambao umetajwa kwenye taarifa ya CAG lazima niwe bayana CAG pamoja na mambo mengine amelihusisha Jeshi la Polisi na kashfa ya sare hewa na kwamba sare hewa hizi ni za shilingi bilioni 16.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima, kwa moyo mkunjufu, kwa mikono yangu myeupe nikiwa kama Waziri makini, nikiwa kama Waziri ambaye ninaitakia mema nchi hii, nikiwa kama Waziri ambaye ninatetea rasilimali za Watanzania na tumuogope Mungu, sijawahi kuona mtu muongo kama CAG katika nchi ya Tanzania. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani sare zinazodaiwa kuwa hewa mimi Waziri ambaye nimekwenda kwenye ma-container na ma-godown ya Jeshi la Polisi. Ambapo nimekuta sare nyingi ambazo zimeletwa halafu CAG anapeleka taarifa kwa Mheshimiwa Rais ya uwongo kwamba, hakuna sare za Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nanyanyua mikono juu, itakapofika jioni kama mimi nasema uwongo kwamba, hakuna sare hewa, kama nasema uwongo najivua nguo. Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama tukiwa tumeambatana na maafisa wa CAG twende main store akaangalie ma-container zaidi ya 15 yenye futi 40, ma- godown matano ambayo yamesheheni sare za vitambaa, viatu, kofia na mikanda, halafu CAG anapeleka taarifa mbele ya Rais kwamba, Jeshi la Polisi wamepokea sare hewa na kulipa shilingi bilioni 16.6 na ninaweka uwaziri wangu rehani kama nasema uwongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumuogope Mungu. Na kama tutaendelea kuwa na mtu anayefanya ukaguzi halafu anaenda anasema uwongo kwamba, kule kuna sare hewa, huyo mtu tumuogope kama ukoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilianza kuwa na wasiwasi inakuwaje Jeshi la Polisi liwe na Sare hewa? Sare ambazo nimeziona kwa macho yangu mimi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumuogope Mungu, sare hizo zipo, hakuna hewa…

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche kaa chini, mda wetu mdogo.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche kaa chini.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni na Katiba zinavunjwa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche utaratibu maamuzi yote ni ya Kiti. Kaa chini.

MBUNGE FULANI: Aaah!

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, liligusiwa pia, suala la Lugumi. Kwamba, suala la Lugumi lilianza nikalichukua, sasa limeishia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, baada ya kubaini kwamba, chombo kingine cha Serikali (TAKUKURU) kwamba, wameanzisha uchunguzi na wakati ule nilikuwa tayari nimeshamuita Lugumi kwa ajili ya kuchukua hatua, suala hilo nililiacha mikononi mwa TAKUKURU, ili waendeleenalo na pale ambapo watakuwa wamelimaliza, jambo hilo litawekwa hadharani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwathibitshie kwamba, wale wote waliokuwa wamekwapua fedha za NIDA. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tuliweza kuyaita makampuni tukanusuru fedha aslimia 84 ya fedha ambazo zilikuwa zimekwapuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko hoja mbalimbali pia za Wabunge ambazo ni vema nikazigusia, hasa Vitambulisho vya Taifa:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema jana wakati umeelekeza mwongozo wa Mheshimiwa Felister Bura kwamba, kutakuwa na usajili wa simu na watanzania wanayo hofu. Napenda niendelee kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba, usajili wa Vitambulisho vya Taifa tunaendelea vizuri na ni lengo letu itakapofika Disemba mwaka huu malengo yetu ya kufikia milioni 24 ya Watanzania tutakuwa tumefikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndio maana nikasema kwa kuwa mpaka sasa tumekwishafikia katika kusajili na kuweza kuandaa namba ya utambulisho wa Taifa, tumefika milioni 16 ambapo Watanzania milioni 16 wana uwezo wa kwenda kusajili simu zao kwa mujibu wa masharti ya TCRA. Wale ambao hawataangukia kwenye hiyo milioni 16 sisi kama Serikali tumesema kwamba, si makosa ya wanaomiliki simu, tutaweka utaratibu maalum wa kuhakikisha kwamba, hakuna Mtanzania ambaye simu yake itakapofika Disemba itazimwa kwa sababu hajawa na namba ya utambulisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo ni vema nikagusia, Naibu Waziri amezungumzia masuala ya ujenzi wa vituo vya Polisi, makazi ya askari kwenye Jeshi la Polisi:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza tayari tumekwishaanzisha The Police Force Cooperation Soul, yaani hili ni shirika ndani ya Jeshi la Polisi. Tayari mkurugenzi mkuu tumemteuwa na wale wakurugenzi wa idara tumewateuwa, tayari wajumbe wa bodi tumewateuwa. Ni imani ya Wizara kwamba, watakwenda kukusanya fedha nyingi sana ambazo ni imani yetu kwamba, watakwenda kumaliza tatizo la makazi na vituo vya Polisi ndani ya Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye Jeshi la Magereza. Kwenye Jeshi la Magereza pia nigusie kwamba, tunaendelea kuhakikisha kwamba, ule mfumo wa ujenzi wa nyumba bunifu wa kila gereza tunauendeleza vizuri, ili kila mwaka kila gereza tumeshalielekeza lazima liwe na nyumba zisizopungua tatu mahali ambapo kuna gereza ili kuhakikisha kwamba, askari wetu wanapata nyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri amezungumzia stahiki mbalimbali za askari, posho:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie askari wote kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, najua mnanisikiliza; la kwanza ambalo tumelifanya ni kuhakikisha kwamba, tunapitia sheria zote pamoja na kanuni zote, ili kubaini na kuorodhesha posho zote ambazo ni stahiki ya askari kwa sababu, kuna baadhi ya posho ambazo ziko kwenye kanuni au kwenye sheria, lakini askari hawajaanza kuzipata. Ni imani yangu kwamba, tutakapokuwa tumekamilisha zoezi hilo lazima tuhakikishe kwamba, askari wanapata hizi posho ambazo zipo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nijielekeze kwenye madeni ya wazabuni mbalimbali, Waheshimiwa Wabunge wengine kwa maandishi mmezungumza hapa:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli inaendelea kulipa madeni ya wazabuni na watoa huduma. Na ndio maana wapo wazabuni kwenye vyombo hivi vya ulinzi na usalama tumeanza kuwalipa fedha. Wale ambao madeni yao yamekwishahakikiwa naomba waendelee kuamini kwamba, madeni yao yatakwenda kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hoja ya Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Kagera, hususan kwenye suala la uhalifu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwenye Mkoa wa Kigoma, alipofanya ziara kwenye Mkoa wa Kigoma, pamoja na mambo mengine na taarifa ya Ulinzi na Usama aliyoipata ni kweli kabisa kwamba, mazingira ya Mkoa wa Kigoma na sehemu ya Mkoa wa Kagera hali ya uhalifu wa kushtukiza na hasa wenye silaha za moto kutoka nchi jirani ya Rwanda au Burundi wamekuwa wakiingia. Na ni kweli kabisa tukiweza kufunga milango ya mipakani ni kweli tutapunguza uhalifu wa silaha ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, tayari tumeanza kutekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu ambapo Jeshi la Polisi wanaendelea na mchakato wa kutathmini na kuangalia vigezo ambavyo vinasababisha maeneo gani ambayo yanaweza yakatengwa, halafu tukayatafutia mkoa maalum wa kipolisi au kanda maalum ya kipolisi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge mnaotoka maeneo yale naomba muwe na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie jambo lingine la wahamiaji haramu. Wahamiaji haramu Mheshimiwa Kitandula amegusia, Wataita pamoja na Wakamba maeneo ya Mkinga wana maingiliano na nchi ya Kenya na kwamba, kuna usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge. Na ndio maana hata juzi Waheshimiwa Wabunge kutoka Kigoma mliweza kutusifia Immigration kwamba, sasa ile kero ya kutumia pua au kuimba wimbo wa Taifa kwamba, huyu ni Mrundi au sio Mrundi imeanza kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie Wabunge kwamba, tutaendelea kudhibiti mipaka na tutaendelea kupambana na uhamiaji haramu mpaka tutakapoutokomeza. Na ndio maana wahamiaji haramu wengine ambao tayari tumekwisha wakamata tunafanya mpango wa kuwarudisha makwao. Na ndio maana katika kuwarudisha makwao tumeendelea pia kupata taarifa za madalali au watu wengine Watanzania wenzetu ambao wanashiriki katika kuwatafutia usafiri ama kuwahifadhi, ili tuweze kuvunja mitandao hii ya uhamiaji haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala kwa ujumla la usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kero ya bodaboda:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie na niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge, kama kuna eneo ambalo sasa tunafanya vizuri ni kwenye kikosi cha usalama barabarani ndani ya jeshi la Polisi. Sasa hivi kikosi cha usalama barabarani zile rushwa zile ambazo zilikuwa zinatuhumiwa sasa zinaenda kwisha. Na ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwa sababu, wengine pia mlikuwa mkiombwa, lakini siku hizi hamusemi kwa maana hali inaendelea kuwa nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, ajali zimepungua kwa asilimia 38.7. Na kielelezo kwamba, tunafanya vizuri ni kupungua kwa ajali na hasa ambazo zilikuwa zinachukua vifo vya watu wengi ikiwa ni pamoja na watu kupata vilema, pamoja na uharibifu wa mali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndio maana huko mbele tunakokwenda, hilo shirika la Polisi nililolisema litaenda mbele zaidi kuhakikisha kwamba, wanapata wawekezaji ambao wana fedha na sisi Serikali hatutoi hata senti tano kwa ajili ya kuanzisha vituo maalum vya ukaguzi wa magari katika nchi nzima. Tutakapokuwa tumemaliza hilo ni imani yangu kwamba, magari mabovu yote yatatoka barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bodaboda nimeshatoa maelekezo na hayo maelekezo ni vema nikayarudia. Ibara ya 4 ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi inazungumzia kwamba, Serikali zote mbili zitatumia nguvu zake zote kuhakikisha kwamba changamoto kubwa nne zinafanyiwa kazi. Changamoto ya kwanza ni kuondoa umasikini. Changamoto ya pili ni kutatua tatizo la ajira hasa kwa vijana na changamoto ya tatu ni vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali na ya nne ya mwisho ni kuendelea kudumisha amani, usalama, utulivu na kulinda maisha ya watu na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bodaboda ni eneo ambalo wamejitokeza kama kujiajiri na hawa ni vijana wanajiajiri. Nimetoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kwamba, bodaboda hawa kwanza lazima wafuate sheria za usalama barabarani kama chombo kingine chochote ambacho kiko barabarani. Hawaruhusiwi kubeba mshikaki, hawaruhusiwi kutokuwa na leseni, hawaruhusiwi kutovaa kofia lazima wavae, lazima waende speed inayotakiwa, sheria zote na watengeneze bodaboda zao. Lakini tumepiga marufuku namna walivyokuwa wanakamatwa na nikaelekeza kwamba, bodaboda za aina tatu tu ndizo zitakazokamatwa na kupelekwa kwenye kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kundi la kwanza la bodaboda ni bodaboda ambayo imehusika kwenye uhalifu. Bodaboda ya pili ni iliyohusika kwenye ajali na bodaboda ya tatu ni ile ambayo ni ya kuokota, haina mwenyewe. Bodaboda ambazo haziko kwenye makundi hayo zisikamatwe na kupelekwa kituoni, tunachofanya ni nini, na nimetoa maelekezo; pale ambapo Askari wa Usalama Barabarani hakumuonya, akaamua kumpiga fine, atampiga fine na yeye atakwenda atafute fine yake kwa muda wa siku saba sawa na wenye magari. Na atakaposhindwa ndani ya siku saba nimeelekeza namna ya kuwapata hawa bodaboda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewaambia kwa kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322 inawataka pia, halmashauri wawe na hawa Polisi auxiliary. Ma-DTO wote nchi nzima washirikiane na wakurugenzi wa halmashauri zote nchi nzima. Hizi halmashauri zina viongozi kuanzia vitongoji, vijiji na kwa mijini kwenye mitaa yote, kila bodaboda hapa nchini lazima aisajili kwa kiongozi wake mahali anapoishi. Atasajili namba ya bodaboda yake, jina la dereva au mmiliki wa bodaboda, baadaye orodha zile zitakusanywa ndani ya ile halmashauri, mkurugenzi ataingiza kwenye database halafu atazalisha database ile ataipeleka kwa DTO, yani Mkuu wa Traffic katika wilaya ile. Na asubuhi askari wa usalama barabarani watakapokuwa wanaenda kazini mojawapo ya kitendea kazi ni orodha ya bodaboda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bodaboda atakapokuwa ametenda kosa ataangalia namba, akiangalia kwenye orodha yake bodaboda haipo atajua huyu hajasajiliwa mahali kwa hiyo, hilo nalo tutadhibiti wizi wa bodaboda. Na bodaboda hiyo ambayo haijasajiliwa lazima atoe maelezo na ile ambayo ataikuta kwenye orodha ata-indicate kwamba wewe tarehe fulani unatakiwa uwe umelipa fine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtindo huo katika nchi yote ya Tanzania hakuna bodaboda atakayetuchenga na hatutahangaika na bodaboda kwa sababu tutakuwa tunajua mahali walipo na namna ambavyo tunaweza tukawasaidia kwa sababu, lengo sio kuwasumbua bodaboda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa wafanyabisahara ndogondogo, almaarufu mamantilie au mamalishe. Vijana wanachoma chips wanakaanga chips:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na sintofahamu wakati mwingine, Ilani hii inasema waondoe umasikini; sasa kama mamantilie anasumbuliwa biashara zake, babalishe anasumbuliwa biashara zake. Lazima Jeshi la Polisi mahali walipo watafute namna bora ya kuwalea hawa wafanyabiashara ndogondogo. Na pale ambapo wanajihusisha na makosa ya kipolisi ya kijinai, waweze kuwaelekeza namna bora ya kuendesha biashara yao na sio kila wakati kuwafunga mashati halafu wanashindwa kufanya biashara zao watu masikini hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la kusisitiza kesi za kubambikiza pamoja na dhamana. Wamesema Waheshimiwa Wabunge hapa kwamba, kweli kwenye magereza zetu hapa nchini kuna baadhi ya kesi ndogondogo ambazo watu wako mahabusu kule magereza au kesi ndogondogo mtu amefungwa yuko kule magereza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliarifu Bunge lako Tukufu tumeishakubaliana na Waziri wa Katiba na Sheria namna ambavyo tutakwenda kutumia hizi Mobile Courts, namna ambavyo ushauri uliotolewa na Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, ya kuhakikisha kwamba, tunatengeneza kamati za kutembelea magereza kila wakati kwenda kuwabaini wale ambao kwa kweli wako kule, lakini hakuna sababu za msingi kuendelea kulundikana kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimuombe Mheshimiwa Esther Matiko katika hili wewe ni shuhuda mzuri, kuna watu walikuwa wanasema msongamano magerezani wengine wanatoka na ukurutu, wengine wanatoka na vifua, lakini tumeshuhudia Mheshimiwa Esther Matiko na Mheshimiwa Mbowe wametoka kule wako vizuri tu kwa hiyo, magereza yetu wanakula vizuri na wanalala vizuri na wanatoka wakiwa na afya njema kama mnavyomuona Mheshimiwa Esther Matiko anavyong’ara. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala alilolisema Mheshimiwa Esther Matiko. Mheshimiwa Esther Matiko mpaka sasa bado mimi Waziri haijaniingia akilini kwamba, kwenye kituo cha Polisi na ukavitaja baadhi ya vituo vya Polisi kwamba, wako Polisi wetu ambao wanalawiti watuhumiwa kinyume na maumbile, watuhumiwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hilo kama kweli litakuwa na ushahidi kwa sababu, kuna mambo yanaweza kufanyika, lakini yakiwa na ushahidi. Nimuombe Mheshimiwa Esther Matiko aligusia wakati anachangia kwamba, kuna RCO alienda magerezani pale kwa hiyo, niombe unisaidie jina la huyo RCO, ili tupate mahali pakuanzia, pengine tunaweza tukaona kwamba, jambo hili lilitokea kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi mmehitaji vituo kwenye maeneo yenu, mmehitaji magari au pikipiki akiwemo na ndugu yangu Mheshimiwa Suzan Kiwanga, Mbunge wa Mlimba. Changamoto ya Mlimba pale naifahamu. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge na ndiyo maana nimekuwa nikiongea na Halmashauri zilizopo kule; Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji, kwamba sisi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tunapokuwa hapa Bungeni, tunagawana sungura mdogo huyu. Tunapomaliza kugawana, baadhi ya Wizara wanakwenda kule kwenye Halmashauri zao wanagawana sungura mwingine tena. Sisi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tunakosa fursa kama hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, ninyi ni Madiwani kwenye Halmashauri zetu. Nimezunguka, kuna baadhi ya Halmashauri kwa kweli wanatenga fedha. Kuna maeneo ambapo wananchi wameshaonyesha nguvu zao, yapo maboma; nawaomba kwenye hizo Halmashauri pia, vyombo hivi vya ulinzi na usalama na vyenyewe vinatoa huduma kama ambavyo darasa linatoa huduma. Kama ambavyo kwenye elimu mwalimu anahitaji nyumba; nasi Askari tunahitaji nyumba. Mahitaji ni yale yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba Waheshimiwa Wabunge kwenye Halmashauri zenu mjaribu kushawishi, nami nitaendelea kuwasiliana na Waziri mwenzangu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuone namna ambavyo tunaweza tukasaidia maeneo hayo. Mheshimiwa Suzan Kiwanga ahadi yangu ya kuja Mlimba bado iko pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mkuchika, masuala yanayohusu mishahara, maslahi pamoja na vyeo, ametoa kauli ya Serikali hapa leo. Pia niwahakikishie Askari wote kwenye vyombo vyote vya ulinzi na usalama na katika hotuba yangu nimeeleza, nimeeleza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa Waziri, muda wako umekwisha.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza kwamba Askari wapo ambao tumewapandisha vyeo hivi karibuni na wapo wale ambao mchakato wa kuwabaini na kuwapandisha vyeo unaendelea. Kwa hiyo, wafanye kazi bila kuchoka kwa sababu mchakato wa kuangalia maslahi ya vyeo unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, nataka niwahakikishie Watanzania na Bunge hili kwamba pamoja na kasoro ndogo ndogo ambazo zinajitokeza kwa baadhi ya askari, endeleeni kuliunga mkono Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama, wanafanya kazi kubwa. Hatuwezi kukata tamaa, na ndiyo maana wale wachache ambao wanataka kuharibu taswira ya Jeshi la Polisi, tumeonyesha kwenye hotuba yetu kwamba tumekuwa tukichukua hatua za kuwashusha vyeo na wengine kuwafukuza kwa aibu. Kwa hiyo, nasi hatuvumilii na kukaa na watu kama hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, kwa heshima na taadhima, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.