Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Anthony Calist Komu

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, naomba nami nichangie hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani kutokana na umuhimu wake katika suala zima la usalama wa raia na mali zetu.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema katika vipaumbele vya Wizara yake ni kuhakikisha amani na utulivu unaendelea katika nchi yetu na kuhakikisha kuwa wanajitosheleza kwa chakula kupitia miradi inayoendeshwa chini ya Jeshi la Magereza. Haya ni malengo mazuri sana na ya kuungwa mkono lakini ni lazima ukweli huu hapa chini uzingatiwe.

Mheshimiwa Spika, moja, amani na utulivu ni tunda la haki na uzingatiaji wa sheria kwa kila mtu yaani watawala na watawaliwa, raia na viongozi. Suala la kuzuia mikutano ya hadhara na sasa karibu shughuli zote za kisiasa za wanasiasa ni uamuzi usio sahihi, wa haki na wala siyo wa kisheria. Hii inaweza kuwa sababu ya uvunjifu wa amani siku za baadaye. Ni vyema Jeshi letu la Polisi likatumia weledi wake kuhakikisha shughuli za kisiasa zinafanyika kulingana na sheria na mtu mmoja mmoja anayetumia fursa hii vibaya achukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, hivi majuzi nimeona katika vyombo vya habari Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara akitoa maelekezo na vitisho kwa OCD wa Tarime eti awakamate Wabunge wa CHADEMA waliofanya mkutano wa hadhara huko Tarime Mjini na kama hatawakamata basi aondolewe mara moja katika nafasi yake. Hii inatia mashaka sana kauli kama hizi zinapoachwa bila ukemeaji wowote kutoka kwa Waziri mwenye dhamana. Naomba atakapokuja kuhitimisha na hili alitolee maelezo na kukemea tabia hii ili Jeshi letu liendelee kuaminiwa na kuheshimiwa na watu wote.

Mheshimiwa Spika, mbili, pawepo na ushirikiano wa karibu baina ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Katiba na Sheria na Idara ya Mahakama juu ya uwepo wa mahabusu wengi ambao kwa sababu mbalimbali wanakaa katika magereza yetu kwa muda mrefu bila mashauri yao kuamuliwa au hata kuanza kusikilizwa tu. Masuala kama haya yanatumia gharama nyingi sana za jeshi letu mfano chakula, magari, rasilimali watu na hata hali ya afya ya mahabusu wenyewe kutokana na msongamano wa mahabusu wa aina hiyo.

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeeleza katika ukurasa wa 11 na 12 jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kukabiliana na uhaba/uchache wa Vituo vya Polisi na nyumba za askari. Katika Jimbo la Moshi Vijijini, sisi wananchi wa Jimbo hili, Kata za Uru Kusini, Shimbwe, Uru Kaskazini na Uru Mashariki wamejenga kituo kikubwa cha kisasa sana cha Class ā€˜Cā€™ na kimekamilika. Nilishamuarifu Mheshimiwa Waziri juu ya kukamilika kwa kituo hiki nikimuomba aje kukipokea na kutambua mchango wa wananchi hawa wa zaidi ya Sh.100,000,000. Naomba wakati Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake atuambie ni lini atakuja kupokea kituo hiki.

Mheshimiwa Spika, kwa maombi yangu kwa niaba ya wananchi ninaowawakilisha TANAPA (KINAPA) wameunga jitihada hizi za wananchi na kujenga nyumba kwa ajili ya askari watakaohudumu katika kituo hiki, nayo imekaribia kukamilika. Jitihada kama hizi zilishafanyika pia katika Tarafa ya Kibosho ila sasa uhudumiaji wa kituo hicho ambacho kilijengwa katika Kata ya Okaoni leo kinahitaji ukarabati na huduma nyingine kama gari la uhakika kutokana na ukubwa wa eneo linalohudumiwa na kituo hicho.