Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, Serikali iliondoa maduka ya duty free yaliyokuwa yakitumika kutoa huduma kwa watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwepo Polisi, Magereza, Zimamoto na kadhalika na imeleta utaratibu wa kulipa kiasi cha fedha kama mbadala wa duty free.

Hata hivyo, watumishi wa Uhamiaji wamekuwa hawalipwi licha ya kuwa nao ni sehemu ya vyombo vya ulinzi na usalama. Hali hii inaleta hali ya unyonge hasa kwa kuzingatia kuwa kazi zao ni za ulinzi na usalama. Nashauri Serikali ione umuhimu wa kuwajumuisha Uhamiaji ili na wao wapate huu unafuu.

Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa gari ya polisi kati ya Dodoma na Iringa. Barabara ya Dodoma – Iringa hivi sasa inatumiwa na magari mengi ya mizigo, abiria na binafsi. Hata magari ambayo ni transit kati ya Tanzania na nchi za jirani yanatumia barabara hii ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Cairo-Johanesburg. Pamoja na umuhimu huu, hakuna huduma ya gari la polisi hali ambayo ni hatari sana, hasa inapotokea ajali ambayo ina majeruhi wanaohitaji huduma ya haraka. Pamoja na kuwa siyo jukumu la Jeshi la Polisi kubeba majeruhi lakini uwepo wa gari unasaidia kufika eneo la tukio kutoa msaada wa kiusalama.

Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 19/4/2019 (Ijumaa Kuu) nilipata ajali kati ya Chipogolo na Mtera. Nawashukuru sana Askari wa Kituo cha Chipogolo, pamoja na usafiri wa kuunga-unga walifika kutoa msaada. Nikiwa eneo la ajali, nilishuhudia magari ya viongozi wakiwemo Wabunge, Mawaziri na mengine ya Serikali yakipita na ndipo nilipobaini kuwa barabara hii inahitaji kuwezeshwa hasa kwa vyombo vya usafiri walau katika Kituo cha Chipogolo (upande wa Dodoma) na Migori (upande wa Iringa).

Mheshimiwa Spika, naamini aina yoyote ya gari itawasaidia. Nasema haya nikiwa ni mhanga wa hali halisi kwa sababu baada ya ajali ambayo haikuwa na madhara kwa maana ya majeruhi, ilituchukua zaidi ya saa zima kupata msaada wa lifti ya gari. Sasa nilijiuliza ingekuwaje au inakuwaje pale ambapo kumetokea majeruhi wanaohitaji msaada wa haraka? Naamini hata kupitia wadau, Jeshi la Polisi wanaweza kupata msaada wa gari.