Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia hii hoja iliyopo mbele yetu. Pia naomba nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa Mambo Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Kangi Lugola pamoja na Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa hotuba hii ambayo wameiandaa.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, naomba niwapongeze Askari Polisi wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kuitetea na kuilinda nchi yetu. Hali kadhalika nawapongeza Majeshi ya Magereza, Idara ya Uhamiaji, NIDA na Jeshi la Zimamoto tunaelewa wanafanya kazi yao nzuri pamoja na ufinyu wa bajeti iliyopo, pongezi zao sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kujitahidi kuboresha ustawi wa Jeshi la Polisi kwa kuona umuhimu kwanza wa kuboresha ukarabati wa Chuo cha Taaluma cha Polisi, Dar es Saalam, lakini pia na ujenzi wa nyumba za Jeshi la Polisi pamoja na Askari Magereza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kuhusu suala la usalama barabarani nikirejea ukurasa wa tisa hadi wa 10 katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Imebainisha kwamba sasa hivi ajali zimepungua kwa asilimia 38, napongeza hatua hiyo. Sambamba na hilo, naomba nichukue fursa hii kuiomba Serikali yangu Tukufu kuona umuhimu sasa wa kuipitia Sheria ya Usalama Barabarani kwani bado ina upungufu mwingi na upungufu huu iwapo kama utaondolewa ina maana kwamba tutawalinda wananchi wetu waweze kuepukana na vifo pamoja na ulemavu wa kudumu.

Mheshimiwa Spika, naungana na maoni ya Kamati yangu, na-declare interest mimi ni mjumbe wa Kamati hii, kwamba kuiomba Serikali iharakishe marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168 kwani hatuoni sababu kwa nini inachelewa. Kwa sababu tukirekebisha sheria hii kuna baadhi ya mambo ambayo yanaweza yakaleta tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nataka kujua, kwa nini Serikali imechelewesha kuleta marekebisho ya sheria hii, kwa sababu sasa hivi kumekuwa kuna matumizi ya teknolojia na baadhi ya madereva wetu wamekuwa hawafuati Sheria za Usalama Barabarani kwa sababu wanaendesha vile vyombo vya moto huku wakitumia simu. Kwa hiyo wanapokuwa wakitumia simu hizi ina maana kwamba umakini wao katika kuendesha vyombo hivi unakuwa ni mdogo sana. Kwa hiyo kama ikipatikana Sheria ina maana kwamba itawabana hawa madereva ambao ni wazembe na itasaidi kupunguza ajali.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo katika kurekebisha sheria hii, naamini kabisa hili suala la kiwango cha kilevi ambalo liko katika sSheria ya nchi yetu kwamba madereva wanaruhusiwa kuwa na asilimia 0.08 ya kiwango cha kilevi. Je, kwa nini Serikali isione umuhimu sasa wa kubadilisha kiwango hiki ili kiwe asilimia 0.05 ambacho kinaendana na kiwango cha kimataifa chini ya World Health Organization. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa 17 wa hotuba hii, Waziri amezungumzia kuhusu kuongeza rasilimali watu na fedha na kubainisha kwamba, kuna baadhi ya maaskari wamehitimu mafunzo. Ningependa kujua, Je, katika mafunzo haya kuna jicho la kijinsia? Ni wanawake wangapi ambao wamepata fursa ya kwenda katika mafunzo haya na kupandishwa vyeo katika maeneo mbalimbali. Kwa sababu naamini kabisa sote tunafahamu kwamba nchi yetu imeridhia matamko mbalimbali ya kuhakikisha kwamba usawa wa kijinsia unakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa kuna malalamiko ya baadhi ya Maafisa au Polisi (askari) wa kike ambapo wakipangiwa mafunzo na ikitokea bahati nzuri wakawa wajawazito…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Muda hauko upande wako Mheshimiwa Toufiq.

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)