Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nami niweze kuchangia kwenye hii Wizara ya Mambo ya Ndani. Nimesikiliza karibu wazungumzaji wote, Wabunge wote wa pande zote mbili kwa maana ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ambao ndiyo wengi, lakini pia na Wabunge wa CHADEMA na CUF na wengine waliochangia wanazungumzia sana suala la maslahi kwa maaskari wetu kwa maana ya Polisi, Zima Moto, Magereza na Uhamiaji, wamezungumza vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze Wabunge wote kwa jinsi walivyowapigania maaskari wetu kwa maana ya kutaka kuongeza mishahara. Siyo jambo baya, lakini nakuwa na hofu kidogo na hofu yangu hii labda naomba inawezekana ikaondolewa na Bunge hili kupitia kiti chako kwa sababu wakati mwingine haitakiwi tuwapende maaskari kwa maneno tu, kwa kuzungumza tu, leo ndiyo siku tunayojadili bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani, na leo hapa inaonekana fedha zinazoombwa ni bilioni 921.2.

Mheshimiwa Spika, wakati wa kujadili bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani, pamoja na mambo mengine Wabunge kazi kubwa inatakiwa pia tujadili namna ya kuongeza mishahara ya maaskari wetu. Nashauri, kama kweli tunayozungumza kwamba tunawapenda maaskari na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ndiyo wengi zaidi na ndiyo wanaweza wakapitisha akidi, hebu tufanye maamuzi hapa leo hii kwamba maaskari wetu waongezwe mishahara leo na mishahara hiyo angalau ianzie shilingi milioni mbili kwa askari mmoja na kuendelea kima cha chini na baada ya hapo kila askari apewe angalau gari nzuri ya kutembelea, kila askari apewe nyumba bora na baada ya hapo mambo yaweze kwenda vizuri kwa Jeshi la Polisi.(Makofi)

MBUNGE FULANI: Siyo kwa maneno.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, tusiende kwa maneno.

SPIKA: Mheshimiwa Haonga, kama kweli husemi uongo kwa nini hukuleta hoja mahsusi kwa ajili hiyo. Unajua kabisa kwamba hayo unayoyasema Kanuni hatuwezi kuyafanyia kazi, unajua kabisa. Kwa hiyo kwa nini hukuleta hoja mahsusi ukajenga hoja kwa ajili ya jambo hilo.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, mimi najua, wewe ni mzoefu sana na Bunge hili unaweza ukatuongoza vizuri, kwa sababu jambo lenyewe lina maslahi mapana ya maaskari wetu tukalijadili hapa, kwa sababu CCM ni wengi tuongeze maaskari wetu mishahara milioni mbili mbili wapate magari, wapate fedha kwa sababu wao ni wengi zaidi. Kwa hiyo naomba… (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa cheap politics haikusaidii, lazima ufuate Kanuni za Bunge. Haya nipe Kanuni ya kuweza kufanya hilo unalolisema maana yake unawadanganya askari nchi nzima kwamba Bunge hili linaweza hilo unalolisema, instantly nipe kuhusu utaratibu sasa. Nifungulie ni mahali gani!

MBUNGE FULANI: Ipo, kuna page inayozungumzia mishahara.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, with due respect, naomba niseme kwamba, tunapokuwa tunaijadili bajeti, bajeti hii hapa tunaweza tunakafanya…

SPIKA: Nimekwambia nipe Kanuni gani.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Tunaweza tukafumua bajeti, tukaifumua then baada ya hapo tukajadili kuboresha maslahi ya maaskari wetu.

SPIKA: Mheshimiwa Haonga kaa chini! Kaa chini, unachofanya ni uchochezi tu. Taratibu za Kibunge zinafahamika, kama kweli una nia hiyo ungeleta katika utaratibu wa kawaida. Tunazungumza habari ya jeshi hapa, unachochea wanajeshi, ilete katika utaratibu wa kawaida, kama kweli wewe ni Mbunge serious ili lifanyiwe kazi. Pita kwenye Kamati ya Bajeti kule na kadhalika, maana yake mnavyosema namna hii mnawafanya watu waamini kwamba Wabunge hawa hawawatakii mema askari, hivi na hivi, kitu ambacho si kweli hata kidogo.